Niliyoyakuta LUSHOTO yanasikitisha

Elli

Platinum Member
Mar 17, 2008
55,499
86,035
Wapendwa nawasalimu wote na kuwapa pole kwa mpigo katika kipindi hiki ambacho kwa uzembe tena Taifa linalazimika kuombolezea Maisha ya ndugu zetu huko Zanzibar, poleni na MUNGU awaerehemu. Amen.

Wiki iliyopita nilikua Lushoto-Tanga mahali nilikokulia nikajifunza na tamaduni za kule hivyo kupewa hata heshima ya kujitambulisha kama mmoja wa wana-Lushoto. Huko niliona mengi lakini haya matatu yalinigusa sana na kuona ni vyema niyaweke hapa jamvini kwa ajili ya kumbusho la vizazi vijavyo.

Moja: Nilishuka Mombo (barabara kuu ya Arusha na Mchepuko wa barabara ya Lushoto) kukiwa na jua kali la jioni nikaanza safari ya kupanda milima kwenye bara bara nzuri kama zulia zuri na jeusi ambako Macho huvutwa na vilima na mawe yaliyoning'inia kando ya bara bara huku yakikukonyeza kwa utani na ucheshi wa kukutisha kukuangukia, hii ndio barabara ambayo Wakoloni waliamua kuyaacha mawe haya macheshi yaipendezeshe LAKINI mita mia kadhaa kutoka Mombo nikashtuka baada ya kuona mawe haya baadhi yao "yakilia" kutokanana kile kilichoitwa labda Ubunifu wa binadamu, mara nikaona michoro ya matangazo ya biashara yamechorwa kwenye mawe yale na mawili yalisomeka hivi..'' Rosmin Hostel; Accomodation....." na jingine lilihusu kifua kikuu likisomeka hivi "TB inatibika, Wahi hospitali". Hakika la pili yake sikuwa na taabu nalo sana lakini hili la kwanza katu sikukubaliana nalo kwa sababu zipo kanuni na njia sahihi za kutangaza biashara na sio hii ya kuharibu nature kwa kisingizio cha ubunifu uwao wowote ule. Naomba wana mazingira hili liwe ajenda pia ikiwa ni pamoja na michoro ile kule Iringa na Singida.

Pili; unapopanda Lushoto ile bara bara network yake iko chini sana na hivyo nyakati za nyuma yapata miaka kama mitatu sasa kulikua na ujambazi wa kuvamia magari sana na kuhatarisha mali na maisha ya watu; hivyo kikawekwa kuzuizi cha polisi LAKINI kizuizi hiki kimegeuka kijiwe cha Polisi-askari hawa kuganga njaa kwa kusimamisha kila gari na kudai kitu kidogo, tulifika eneo hili askari mmoja akiwa kakaa kwene stuli, akasimamisha gari nilimokuemo aina ya Noah na kumtaka dereva ashuke/ateremke kwenye gari amfuate pale alipo; kwa wanafahamu jiografia ya bara bara hii watakubaliana na mimi kuwa ni hatari zaidi ya Kitonga kwani ni nyembamba sana na chini ni bonde kubwa sana; cha ajabu dereva akashuka na kumfuata huku tukiwa tumebaki wenyewe kwene gari nikajiuliza hivi hand-break ikifyatuka hapa tutatpona kweli? Nikaliacha hilo kama lilivyo.

Tatu; Kufika Lushoto nusura machozi yanitoke ni baaada ya kuona misitu na mapori mazuri ambayo yalihifadhi "ubikira" wa ardhi ile yamechinjwa chinjwa kwa ulafi wa kugawana viwanja; sina ubishi wala upinzani nalo ila kwa "maendeleo" yale ya kujenga kila mahali ukidhani ndio maendeleo tunajijengea kaburi ambalo hatutaweza kurudi nyuma tena; bahati mbaya sana sana sikuwa na kamera but I wish ningeweka picha hapa kama ushahidi wa uharibifu mkubwa wa mazingira.

Ombi langu; naomba tusaidieane kuitunza rasilimali hizi ambapo sasa hata maji yamekua yanapatikana kwa shida Lushoto....Lushoto yaweza kuwa kivuli/taswira ya mengi yanayotokea sehemu kubwa ya nchi; je wewe uliona lipi na wapi? Asanteni
 
Back
Top Bottom