[h=1]Nilikataa uchungaji nikawa mkuu wa wachawi- 6....[/h]
ILIPOISHIA
Kesho yake (Jumapili) nilikwenda katika Kanisa la Huduma ya Neno la Upatanisho iliyopo Bustani ya Edeni Kitunda, Kivule, Dar zamani ikijulikana kama Matembele ya Kwanza kwa lengo la kufanya nilichoelezwa kule kuzimu.
Niliingia kwenye huduma hiyo nikamkuta mtumishi wa Mungu Askofu na Nabii, Nicolaus Suguye akihubiri madhabahuni. Nilijaribu kurusha dawa zangu ili kumdhohofisha lakini haikuwezekana.
SASA ENDELEA
Niliamua kurudi nyumbani ili nikajipange upya. Nilikwenda kwenye makanisa mengine kwanza kujaribu kama dawa nilizopewa zinafanya kazi kweli ama la!
Jumapili moja niliingia kwenye kanisa na mtumishi anayejiita askofu mwenye wafuasi wengi. Niliwakuta waumini wachache wanapanga viti kwa ajili ya ibada.
Nilikaa kwenye kiti cha nyuma kama muumini kisha nikachukua dawa yangu na kuanza kunuiza maneno mazito ili kila atakayeingia ndani ya kanisa hilo awe na usinginzi na umeme ukatike ghafla.
Lengo la kukata umeme ukatike ni kuviharibu vyombo vya muziki wanavyotumia pamoja na kipaza sauti cha askofu.
Ibada ilipoanza, kama kawaida walifanya maombi ambayo hayakuwa na athari zozote kwangu. Askofu alisimama kwa ajili ya mahubiri, asilimia kubwa ya waumini walianza kusinzia.
Macho yao yalikuwa mazito hasa, nilifanikiwa kuwanasa wenye imani haba. Wakati askofu anahubiri nilifanya maarifa ya kukata umeme na kufanikiwa kuviunguza vyombo vya muziki na kipaza sauti alichokuwa anakitumia.
Niliondoka baada ya kuona nimefanikisha adhma yangu. Jumapili iliyofuata nilikwenda tena kwenye Huduma ya Neno la Upatanisho kwa Askofu na Nabii, Nicolaus Suguye.
Nikiwa ndani ya huduma hiyo nilishangaa, Suguye alitambua kama nipo ndani na kusema:
‘Naona leo wachawi wamekuja kutujaribu, leo watapeleka salamu kuzimu kwamba, huduma hii inaongozwa na mtumishi anayemtumikia Mungu wa kweli.'
Kama kawaida, alianza kuhubiri kwa ujasiri wa ajabu pamoja na kujua mimi nipo ndani. Baada ya mabubiri ilifuata zamu ya maombezi na hapo ndipo nilijuta kwa nini niliingia ndani ya huduma hiyo.
Muda wote wa mahubiri mwili wangu ulikuwa unachomwa chomwa na vitu kama sindano. Wakati wa maombezi nilishangaa kuona nimetoka mbele kana kwamba naenda kuombewa.
Aliposogea kwangu, alinyoosha mkono wake kuelekea kwenye kifua changu. Niliona naungua kwa moto, nikaanguka chini na kupoteza fahamu. Nilipozinduka sikuwa na nguvu za kichawi tena, nikajikuta nasema:
‘Nisamehe Mtumishi wa Mungu, nilikataa uchungaji nikawa mkuu wa wachawi na hapa nilifika kukudhohofisha kihuduma lakini nimeshindwa.'
Kauli hiyo iliwashtua waumoni wengi baada ya kuwasimulia jinsi nilivyokuwa nafanya kazi ya kuwapulizia dawa ili wapate usinginzi.
Baada ya kuombewa nilirudi nyumbani nilipofikia. Usiku wa manane, yule babu aliyenisimika kuwa mkuu wa wachawi alikuja kwa njia ya kishirikina akiwa amekasirika na kusema:
‘Kwa nini umeamua kutusaliti? Tulikwambia ukiona kanisa ambalo halina nguvu ya Mungu ingia, ila usiingie kama unaona kuna upinzani mkubwa.'
Akiwa anasema hayo, sikujua alipatwa na kitu gani, kwani nilimsikia akipiga kelele za kuomba asamehewe akiahidi kuwa, hatanisumbua tena. Aliponyamaza alipotea kimiujiza.
Msomaji huu ni mkasa wa kweli alionisimulia Steven Soso ambaye sasa ameokoka baada ya jaribio la kutaka kummaliza nguvu za huduma Askofu na Nabii, Nicolus Suguye.
Watu wengi mmekuwa mkinipigia simu kutaka kujua kama mkasa huu ni wa kweli ama ni wa kutunga. Namba ya simu ya Soso ni 0713 271 850. ''MWISHO''