Nikifa msinitafute kaburini - Makwetta | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nikifa msinitafute kaburini - Makwetta

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Oct 21, 2009.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Oct 21, 2009
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  [​IMG]


  INAPOBIDI kusifu huna budi kufanya hivyo, na pia una wajibu wa kukosoa ili kuweka mambo sawa.

  Umaarufu wa mtu unapimwa kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na kudumu muda mrefu katika eneo fulani la utawala kwa kuwa hiyo ni alama ya kukubalika, kupendwa na kuheshimiwa na jamii husika.

  Jackson Makwetta ni miongoni mwa wabunge wa siku nyingi mkoani Iringa na Tanzania kwa ujumla, ambao hadi leo bado wapo kwenye ulingo wa siasa.

  Lakini pia ni miongoni mwa mawaziri waliofanya kazi katika Wizara nyingi, na amekuwa Mbunge tangu mwaka 1975.

  Alianza kuwawakilisha wananchi wakati wilaya ya Makete na Njombe zikiwa pamoja, akashika wilaya ya Njombe, mwaka 1980 wilaya hizo zilipomegeka na wilaya ya Makete ikapata Mbunge, Ntuntemeke Sanga ambaye sasa ni marehemu.

  Mbunge huyo aliendelea kushika ubunge wilaya ya Njombe kabla ya kugawanyika kuwa majimbo matatu, Njombe Kusini ambayo sasa mbunge wake ni, Anne Makinda,na Njombe Mashariki ambayo mbunge wake ni Yona Kevela, yeye (Makwetta) anaongoza jimbo la Njombe Kaskazini.

  Katika majimbo yote matatu, Jimbo la Njombe Kaskazini bado ni kubwa kwa eneo na idadi ya watu, hivyo ameshapeleka ombi kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ili jimbo hilo ligawanywe, kuwe na jimbo la Makambako na Lupembe.

  Anaonyesha wazi ana mapenzi na mwelekeo wa kugombea jimbo la Lupembe ambako ni asili yake, au ndugu na jamaa wengi wanaishi huko, yata yeye wazazi wake waliishi huko.

  Makwetta,ameanzisha mengi wakati wa ubunge wake, anathubutu kujisifu kuwa kama Mungu ataamua 'aondoke' katika uso wa dunia hii, watu ambao hawatakuwa wamesikia au kupata habari za kifo chake wasikimbilie kwenda makaburini kuona kaburi lake, wawaulize wananchi aliowatumikia, watawaeleza mchango wake kwa umma.

  Makwetta anajivunia mchango alioutoa kwa wananchi wa Makete na Njombe, ndiyo maana siku si nyingi zilizopita wananchi wa Makete walimpa zawadi ya lori moja la mbao kuonyesha kuthamini mchango wake mkubwa katika kuhimiza upandaji wa miti ulioziwezesha wilaya hizo ziwe na miti mingi ya mbao na kuongeza utajiri wa wilaya hizo.

  Anapofika Makete hasa Njombe anatambulika kuwa ndiye mwanzilishi wa kampeni ya upandaji miti, miaka ya 1980. Kampeni hiyo imempa sifa za kudumu miongoni mwa wakazi hao wa wilaya hizo mbili ambao asili yao ni moja,Nyumbanitu.

  Kwa nafasi hiyo ya ubunge wa Njombe Kaskazini, alianzisha Mashirika la Maendeleo ya Elimu wilaya ya Njombe, (NDDT), shirika hilo lilianza kujenga shule za sekondari, zikiwamo Mtwango, Uwemba, Kifanya, Wanging’ombe na nyingine ambazo hadi leo zimekuwa nguzo ya elimu wilayani Njombe.

  Pamoja na kuendeleza elimu, vijana wengi waliosoma katika shule hizo leo ni 'watu wakubwa' serikalini, na ifahamike pia kwamba, Makwetta ndiye aliyeanzisha mtindo wa kutengeneza mabango ya kuonyesha shule zilipo kwa kujenga kwa matofali.

  Baada ya kuwekwa Njombe, vibao hivyo vilienea katika maeneo mengine,hivi sasa imekuwa 'fasheni' kuona vibao wa shule za msingi au sekondari vilivuojengwa kwa matofali vipo kando ya barabara.

  Zamani vibao hivyo vilitengenezwa kwa kutumia mbao au miti,sasa vinajengwa kwa matofali, alianzisha mtindo huo wakati akiwa Mbunge na kiongozi wa shirika la elimu wilayani Njombe.

  Ametumia muda wake mwingi kuhimiza elimu, katumia elimu na maarifa yake kuhakikisha kuwa wilaya hiyo inakuwa mstari wa mbele katika elimu lakini pia inakuwa kinara wa wanafunzi wake kufanya vizuri katika elimu nchini.

  Atakumbukwa kwa mengi, hasa katika muda wake wote akiwa Mbunge, alikuwa anatumia muda wake mwingi kuhimiza elimu na kuelimisha umma wa Tanzania, si kwa kuwa Waziri wa Elimu, pia amekuwa Waziri katika Wizara nyingine tisa.

  Baadhi ya wizara ambazo majina yamebadilika lakini wakati huo ziliitwa maji, Nishati na Madini, Sayansi Teknolojia, Elimu ya Juu, Elimu na utamaduni, ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Kilimo na Chakula, Ulinzi na Usalama, na Mawasiliano na Uchukuzi na wizara nyingine.

  Anajisifu kuwa amefanya mengi kwa ajili ya jimbo lake na Njombe Kaskazini, maeneo mengi hata baadhi ya vijiji kuna umeme, kuna maji, kuna barabara zinazopitika wakati wa kiangazi hata kama nyingine wakati wa masika hazipitiki.

  Amewahimiza wananchi kujenga nyumba bora na za kisasa, kampeni ambayo inaendelea kuwa kila mwananchi anatakiwa awe na nyumba ya matofali ya kuchoma hata kama anaezeka kwa nyasi, baada ya muda mfupi 'apige' bati.

  Makwetta ni Mwenyekiti wa kupigania Mkoa wa Njombe, Katibu wa juhudi hizo ni Mbunge wa Makete, Dk. Binilith Mahenge. Kampeni ambazo kuna kila sababu kukubalika kwa kuwa wananchi wa wilaya ya Njombe, Ludewa na Makete ni wamoja kwa asili.

  Amepigania mambo mengi, amefanikiwa katika masuala mengi,ana kila sababu ya kujivunia ushindi aliopata katika kusaidia au kuhimiza maendeleo. Anasema, hapiganii kupata mafanikio ya vitu vya dunia, anachotafuta ni utumishi wa kutuka kwa umma.

  Anasema, kama ni kutafuta maslahi binafsi, wakati wake umepita, kilichobaki ni kusaidia wananchi wanaohitaji zaidi huduma na msaada wake katika kusaidia umma wa Tanzania.

  Makwetta, licha ya kugawa baadhi ya vitabu alivyonavyo nyumbani kwake, kwenye shule mbalimbali ikiwamo Ikuna, katika tarafa ya Makambako, bado ana mpango wa kufungua maktaba kwa ajili ya vijana kutoka maeneo mbalimbali kwenda kusoma.

  Nimeshuhudia huko nyumbani kwake Hagafilo, nje kidogo ya mji wa Njombe kuelekea Songea, maktaba yake ilivyosheheni vitabu vya kiada na ziada ambavyo, ni vigumu kuvipata lakini yeye amevitunza na kuviweka katika mpango mzuri wa kutumika kwa ajili ya vijana.

  Makweta ni mwalimu si wa kufundisha tu, bali kwa ajili ya juhudi zake za kutunza vitabu, kuhifadhi taaluma na kutoa elimu kwa watu wengine watakaopata nafasi ya kwenda kusoma nyumbani kwake.

  Anasema, ikibidi kupumzika hana tatizo, lakini si kupumzika kwa sababu kuna mtindo wa kupokezana vijiti bali ni kwa sababu atakuwa mtu ameandaliwa kupokea kijiti. Atatoa kijiti kama mtu aliyeandaliwa kupokea ataweza kudumisha ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

  Atakayepokea kijiti, lazima awe mkereketwa wa maendeleo ya jimbo hilo,lililosheheni rasilimali nyingi zikiwamo za miti ya mbao, chai, mahindi, mboga za majani, nyanya na bidhaa nyingine.

  Hata hivyo, pamoja na msimamo wake wa kukabidhi kijiti, anaamini kuwa kama NEC ingeridhia maombi yake ya kugawanywa majimbo bado angeweza kuendelea kutumia taaluma yake kusaidia wananchi.

  ‘Yakale ni dhahabu,’ pamoja na upungufu wa hapa na pale kama binadamu, Makwetta ametoa mchango mkubwa katika kipindi cha miaka zaidi ya 30 ya ubunge wake na zaidi ya Wizara kumi alizotumikia katika nafasi ya uwaziri. Ameacha alama mioyoni na nyusoni mwa watu hasa katika elimu na kilimo.

  Makwetta alizaliwa Juni 15, 1943 wilayani Njombe mkoani Iringa, amesoma shule ya msingi Mdandu, shule ya kati Uwemba, kidato cha kwanza hadi sita alisoma katika Shule ya Sekondari Minaki iliyopo wilayani Kisarawe, Pwani, na shahada ya kwanza na pili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amefundisha Mpwapwa sekondari na katika Chuo cha Mzumbe Morogoro.


  http://www.habarileo.co.tz/makala/?n=3812
   
 2. Gudboy

  Gudboy JF-Expert Member

  #2
  Oct 21, 2009
  Joined: Aug 14, 2009
  Messages: 799
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 33
  hongera sana kwa yote mazuri uliyoyafanya ina onyesha una uzalendo wa kweli na wananchi wako waliokuchagua na nchi kwa ujumla, tungekua na viongozi wengi wa mfano wako toka enzi hizo nadhani tungekua tumesonga sana mbele katika maendelea hasa ya kilimo elimu nk. ila wengine ni ubinfsi ndio umewajaa, wao wanawaza kurudisha pesa alizotumia wakati wa kampeni basi. Hongera sana na Mungu akuweke ili uendelee kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla
   
Loading...