Niinue(ni), niwekeni salama

Captain Donor

Member
Jul 24, 2022
13
19
Black Panther: Wakanda Forever.

Lipi linakujia kwenye fikra zako ukijaribu kuiwaza Afrika bila ya mipaka? Afrika ambayo haitafsiriwi tena na tukio la kihistoria lililotokea Berlin mnamo mwaka 1884 mpaka mwaka 1885.

Binafsi nikianza kuwaza kwenye fikra zangu naliona bara lenye maendeleo ya kupigiwa mfano na mataifa nje ya Afrika, bara linaloweza kuzitatua changamoto zake lenyewe bila kutegemea misaada kutoka WB na kwingineko, bara linaloweza kutafuta suluhu dhidi ya baa la njaa kwa watu wake pamoja na vita za wenyewe kwa wenyewe, bara lenye siasa zinazoendana na mazingira yetu wenyewe. Hayo na mengine mengi ya kuvutia ndiyo ninayoyawaza ninapoifikiria Afrika bila ya mipaka ya kikoloni.

Tunaweza kuthubutu bila kuchoka kuiwaza Afrika tunayoihitaji na siyo bara lenye nchi zilizojitwalia uhuru bandia kutoka kwa nchi zilizotutawala Waafrika na kutuachia maumivu ambayo ni ngumu kuyasahau. Licha ya ukweli huo unaoumiza nilipata kusikia msemo mmoja usemao, "Hakuna mtu hatari kama yule ambaye anaijua vyema historia yake".

Ni ukweli kwamba historia mbaya ya ukoloni barani Afrika pamoja na madhara tunayoendelea kupitia mpaka leo haiwezi kufutika lakini inatutosha kuweza kutufungua macho na kuuona ulimwengu katika uhalisia wake na kutuwezesha kuitengeneza dunia ambayo Mama Afrika anapata heshima anayoistahili na kutodharaulika tena.

Niinue (ni) ni theme song inayohusu maombolezo ya kifo cha Black Panther (Shujaa na mlinzi wa Wakanda) na Mfalme T'challa ambao pia kwa upande wa pili wa shilingi unayaenzi maisha ya muigizaji Chadwick Boseman aliyeigiza uhusika wa King T'challa kwenye Captain America:Civil War(2016), Avengers: Endgame (2019) na Black Panther ya kwanza mwaka 2018. Wimbo ulioandikwa na Ludwig Göransson; Robyn Fenty; Ryan Coogler na Temilade Openiyi(Tems) na kurekodiwa kwa sauti ya mwanamuziki mashuhuri duniani, Rihanna.

Mandhari ya mwanzo kabisa tunayojifunza katika filamu hii ni Kifo. Pumzi ya mwisho ni uhalisia ambao haukwepeki, kila kiumbe hai kinachoishi katika ulimwenguni ni lazima kitakufa. Filamu inaanza na mazishi ya aliyekuwa mfalme na Black Panther wa Wakanda, King T'challa.

Ukiwa kiongozi mzuri kwa watu wako utaigusa mioyo ya watu wengi na utapendwa na wengi na mchango wako katika jamii utakumbukwa na kuendelea kuenziwa na wengi baada ya kifo chako. Kifo cha Chadwick Boseman kinatoa mafunzo mengi na kimebadilisha mengi hata kwenye muendelezo wa Black Panther.

Muendelezo wa pili umeakisi zaidi uongozi na maisha ya mfalme T'challa na unatoa taswira halisi ya ugumu uliopatikana kwa kutaka kutenganisha uhusika huo na muigizaji Chadwick Boseman ambaye alifariki kwa ugonjwa wa saratani ya utumbo mpana mnamo tarehe 28 Agosti mwaka 2020.

Hivyo kumpelekea Muandaaji bwana Ryan Coogler kuchukua uelekeo tofauti ambao ndio umetupatia muendelezo mwingine wa Black Panther. Uhusika wa King T'challa imebidi ufe na Chadwick Boseman, alikuwa ni mfalme T'challa kwenye filamu na kwenye maisha halisi kwa kila mmoja.

Uwajibikaji ni mojawapo ya ujumbe muhimu tunaoupata kutoka kwenye filamu hii, scene inayofuata baada ya mazishi ya King T'challa ni Kamati ya mahojiano ambapo anaonekana Malkia Ramonda (Angela Bassett), mke wa King T'chaka na mama wa King T'challa na Binti mfalme Shuri akiulizwa maswali na yeye akijibu kwa kujiamini sana na kueleza juu ya kifo cha mwanaye King T'challa na jinsi ambavyo mawakala wa Kimarekani walivyovamia Wakanda na kutaka kuiba madini ya Vibranium ambayo yanapatikana Wakanda pekee na kuweka wazi juu ya hofu yake dhidi ya tamaa ya taifa la Marekani kutaka kujinufaisha kisilaha kwa kutaka kutumia madini hayo ambayo inahatarisha usalama wa kidunia.

Msimamo wa Malkia Ramonda ni kwamba Vibranium itabaki kuwa ni hazina na mali ya Wakanda pekee. Hii inanikumbusha taifa ambalo lina madini ya pekee ambayo hayapatikani pengine popote ulimwenguni lakini ilikuwa inashika nafasi ya tatu duniani kwa kuuza madini hayo!. Nchi za Afrika bado zina safari ndefu sana katika kipengele cha Uwajibikaji.

Umuhimu wa teknolojia, muendelezo wa Black Panther unatufunza jinsi ambavyo teknolojia inaweza ikatupa majibu ya maswali mengi tunayoweza kujiuliza na kutupatia suluhu ya mambo mengi yanayotutatiza katika kufikia malengo yetu kwa mtu mmoja mmoja na hata taifa kwa ujumla.

Shuri ni binti jasiri ambaye amebobea katika masuala ya teknolojia na mdogo wake King T'challa, kifo cha kaka yake kilikuwa ni pigo kubwa mno kwake na haikuwa rahisi kukubaliana na uhalisia huo na hata kufikia hatua ya kutaka kujaribu kuyarudisha mapigo ya moyo ya kaka yake ili tu aweze kumrudishia uhai lakini kwa bahati mbaya au nzuri teknolojia pia haina majibu kuhusiana na kifo.

Katika moja ya mahojiano yake na Mfalme wa Tolocan(Namor), Shuri aliweka wazi sikitiko lake na kuvunjika moyo kwa kushindwa kuzuia kifo cha kaka yake licha ya ujuzi mkubwa alionao kwenye tech.

Lakini kupitia teknolojia hiyo hiyo aliweza kutengeneza heart shaped herb kutokea kwenye masalia ya DNA za kaka yake, heart shaped herb ni juisi itokanayo na mmea ambao unaaminika kuwa ni zawadi kutokea kwa Miungu ya Panthers. Na juisi hiyo akinywa mtu ambaye hana sifa basi anapoteza maisha mara moja kutokana na nguvu iliyo nayo na jinsi inavyofanya kazi mwilini baada ya kuinywa.

Hivyo ndivyo ambavyo aliweza kuwa Black Panther baada ya kaka yake King T'challa na kuweza kuirudishia Wakanda amani na matumaini mapya mara baada ya kumshinda Namor aliyedhamiria kuiangamiza kabisa Wakanda kisha kuingia vitani na Dunia nje ya Wakanda na Tolocan.

Nguvu ya swali kwanini, "How is never important than why". Badala ya kujiuliza ni vipi utafanya kitu fulani kwanza jiulize ni kwanini unataka ufanye. Kwasababu ukijua ni kwanini unataka ufanye basi ni rahisi kujua ni vipi utafanya kitu hicho.

Kwanini nchi za Afrika bado ni tegemezi? Kwanini serikali nyingi za nchi za kiafrika zinakosa uwajibikaji katika masuala muhimu yanayohusu watu wake? Kwanini hivi, kwanini vile ni mwanzo mzuri wa kuanza kupiga hatua za kujikwamua kutokea kwenye hatua moja hadi nyingine na kuendelea mbele zaidi kifikra na kimaamuzi pia.

Mwishoni mwa mapigano makali kati ya Shuri na Namor, Shuri alikuwa na uwezo wa kumuua Namor lakini hakufanya hivyo kwasababu kisasi chake kwa Namor hakikuweza kuwa na uwiano sawa na amani ya jamii yake ya Wakanda na pia amani na uzuri wa Tolocan pia ambao alivutiwa nao sana.

Hatimaye Tolocan na Wakanda zimekuwa ni washirika na siyo maadui tena. Laiti kama viongozi wa Afrika wataweka mbele maslahi ya Uafrika wetu zaidi ya maslahi yao binafsi basi Afrika itakuwa bara lenye nguvu mfano wa Wakanda. Kwa pamoja tunaweza kuiinua Afrika.

FB_IMG_1668164490473.jpg
 
Interesting. .
Nimependa unauliza maswali na unayajibu mwenyewe nikakosa hata Cha kujibu. Ila naweza sema shukran tumejifunza kitu. .
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom