Sasa ni wakati wa kuanza upya ATCL
27th May 2010
Maoni ya katuni
Jana katika ukurasa wa kwanza wa gazeti hili kulikuwa na habari iliyosema ‘ATCL ni bomba linalofuja fedha' ikieleza taarifa zilizotolewa kwenye kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na ofisa kutoka Hazina jinsi Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limekuwa mzigo.
Ofisa huyo tunayethubutu kusema kuwa ana ujasiri, alisema wazi kwamba ATCL imekuwa ikijiendesha kwa hasara kubwa, huku ikitegemea kupewa fedha kutoka Hazina kwa ajili hata ya kulipa mishahra na gharama zake nyingine za kiuendeshaji kama vile ada na malipo mengine ya kisheria.
Kauli hiyo tunaiona kuwa ni ya kuthubutu kwa sababu Ofisa huyo anajua vilivyo kwamba serikali imekuwa na mtazamo tofauti na huo alioutoa juu ya ATCL. Serikali na kama alivyosema Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, imekuwa na msimamo kwamba wanataka kufufua ATCL na kwa sasa wanaitafutia mbia, ingawa inajua fika kwamba kwa kiwango cha madeni ilicho nacho ATCL itakuwa ni kazi ngumu sana kumpata mwekezaji au mbia wa maana hasa ikizingatiwa kwamba mashirika mengi ya ndege duniani kwa sasa yako kwenye msukosuko mkubwa kiuchumi.
Tunajua kwamba ni fahari kwa taifa kuwa na shirika lake la ndege, lakini fahari hiyo ni lazima iwe na maana, kwani kuwa na shirika mzigo kama ATCL ambalo halijiendeshi lenyewe hata kumudu gharama zake muhimu achilia mbali kutoa gawio kwa serikali, haina maana; ni hasara; ni matumizi mabaya ya rasilimali za umma kwa maana ya kodi za wananchi ambazo zingeweza kuelekezwa kwenye mambo mengine muhimu zaidi.
Hakuna asiyejua historia ya ATC kabla ya kuwa ATCL; tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini kumekuwa na juhudi kubwa za kuvunja nguvu ndogo ya ATC iliyokuwapo, kwanza ilikuwa ni kuiunganisha na AJAS ambayo ilishindikana, lakini baadaye ikauzwa kwa Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) hadi miaka michache iliyopita ndoa hiyo, ambayo haikuwa na manufaa kwa ATCL, ilipovunjwa.
Kwa maelezo mengine ATC na sasa ATCL imepita katika mabonde na vikwazo vingi kwa muda mrefu; imetengenezewa mikakati ambayo kwa hakika haijikiti kutazama ni wapi tulikosea, ndiyo maana kila hatua inayochukuliwa kwa nia ya kuiokoa badala ya kuwa neema inakuwa ni balaa zaidi ya awali.
Kwa wastani kwa muongo mmoja na nusu sasa tunaweza kusema wazi na bila hofu yoyote kwamba ATCL imeshindwa kubadilika kuwa shirika la umma linalojiendesha kwa ufanisi uliokusudiwa na kwa maana hiyo kweli iwe fahari ya Tanzania kama yalivyo mashirika ya ndege ya mataifa mengine ulimwenguni.
Sisi hatuna kinyongo chochote na ATCL ila tunaumwa na kuona uchungu wakati taifa hili linashindwa kuwa na shirika la ndege linaloweza kutimiza wajibu wa kusafirisha raia wake hata kama ni ndani ya mipaka yake tu achilia mbali safari za kimataifa. Watazania wamekuwa wanajiuliza tena na tena ni kwa nini tunaendelea na utaratibu huu wa kukumbatia kitu ambacho kimekwama? Ni kwa nini basi tusianze upya kwa kuzingatia mazingira mapya, changamoto za sasa na kujielekeza katika utendaji unaowekewa malengo ili tuwe na shirika linalojiendesha kwa ufanisi na kuleta tija?
Kwa maoni yetu msimamo wa serikali kisera wa kutaka bado kuibadili ATCL hii kwa kutafuta wabia, hakika tutapata matatizo tu; hatusemi haya tukiichuria ATCL, ila tunasema hayo kwa kuwa njia pekee ingekuwa ni kukubali yote yaliyotokea, kuivunja ATCL na badala yake kuanza upya.
Tuanze kuliunda upya kwa kuzingatia mambo mengi, kwanza changamoto za sasa na mbinu za sasa za kuendesha mashirika ya ndege, kuwa na damu mpya ya watendaji ambao wanatambua maana na umuhimu wa kujiwekea malengo, wajue kwamba bila kuzalisha faida ya kujiendesha shirika hilo haliwezi kuwa na nafasi katika sekta hiyo.
Utaratibu wa kuendelea kuchota kodi za wananchi na kutoa kwenye mashirika yasiyojiendesha yenyewe ni utaratibu uliopitwa na wakati. Kama vishirika vidogo vya ndege vinajiendesha kwa ufanisi mkubwa tena ndani ya Tanzania ni balaa gani inaifanya ATCL nayo isifanye hivyo pia? Tukatae kuendelea kuidekeza ATCL, imeshindwa na sasa tuanze upya, inawezekana!
CHANZO: NIPASHE