Ngurumo: Watashinda kwa sifa za kijinga?

Mzito Kabwela

JF-Expert Member
Nov 28, 2009
18,857
7,615
MWAKA 2005 nilipokataa kumuunga mkono mgombea urais Jakaya Kikwete, katika harakati zake za kuusaka urais kupitia CCM, nilitoa sababu kadhaa kwa wote walionijia kuniomba niwaunge mkono.

Kwanza, nilisema hakuwa bora miongoni mwa wote waliokuwa wamejitokeza kupitia CCM. Nilipompima na wenzake 10, niliamini kwamba CCM kingeweza kupata mgombea anayefaa zaidi. Bahati mbaya, wagombea wengine 10 hawakuwa wamejiandaa kama yeye na mtandao wake. Akawashinda. Lakini leo sote ni mashahidi kwamba Ikulu imempwaya!

Pili, niliwaambia kwamba sitamani tena kuongozwa na rais kupitia CCM. Kwamba wakati ulikuwa umewadia tuanze kufikiria kukipumzisha chama hicho ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka yote ya uhuru wa Tanzania; na ambacho Katibu Mkuu wake wa zamani, hayati Horace Kolimba, aliwahi kusema bila woga kwamba hakina dira wala mwelekeo. Akafa akiwa anahojiwa na vikao vikuu vya CCM!

Tatu, hata alipokuwa amepitishwa Kikwete kugombea kupitia CCM, nilisisitiza kwamba hara rekodi ya utendahi uliotukuka. Nilitazama miaka zaidi ya 20 aliyokuwa amekaa serikalini, nikachunguza kote alikopita na nayadhifa alizopata; nikaridhika kwamba hakuacha nyayo za mafanikio yanayotosha kuwashawishi Watanzania kwamba anafaa kuwa rais wa Tanzania.

Nikawaambia kwamba lakini kwa kuwa sasa inaelekea urais wa Tanzania umeanza kuchakachuliwa, anaweza kushinda na kutawala. Na ndivyo ilivyotokea. Akashinda.

Lakini hata kabla hajashinda, miongoni mwa watu waliokuja kwangu kumnadi na kuomba "msaada" wangu, ni wanahabari waandamizi niliokuwa nawaheshimu sana. Baada ya mjadala mrefu, huku wakisisitiza kwamba iwe iwavyo Kikwete ndiye angekuwa rais, niliwapa kigezo cha kumpimia uwezo.

Nilitafuta kigezo kinachohusu taaluma yetu. Nikasema kwa sababu wao walikuwa wakimnadi Kikwete kama "rafiki wa wanahabari na vyombo vya habari" njia ya kumpima ni moja tu – kiwango cha urafiki wake kwetu.

Wakati huo tulikuwa tumekamilisha rasimu ya muswada wa sheria ya uhuru wa habari kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali, zikiwamo MISA Tanzania, UNA Tanzania, Chapter 19, na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Marekebisho hayo yalijiegemeza katika mahitaji ya kisasa na ushauri wa Tume ya Nyalali kuhusu sheria mbaya zinazofaa kufutwa au kurekebishwa tangu 1992; tukapendekeza namna ya kuziboresha na kutengeneza sheria moja itakayorahisisha na kuboresha mawasiliano ya umma.

Serikali ya Rais Benjamin Mkapa ilipopewa rasimu hiyo, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ikaiweka kabatini na kuendelea na kazi zake kama kawaida. Dharau!

Mashabiki wa Kikwete waliitumia fursa hii kama turufu ya kuonyesha ukatili wa serikali ya Mkapa na Sumaye, na kwamba Kikwete alikuwa anapigana kuingia Ikulu ili kurekebisha tabia za namna hii.

Sikuwaamini. Nilijua hiyo ilikuwa lugha ya ushawishi kwa wanahabari ili wamuunge mkono mtu wao. Nikawaeleza kwamba kipimo change cha ufanisi wake na urafiki wake kwetu ni kama atakubali kuipitisha sheria hiyo ili kujenga mazingira ya kiutu ya kufanyia kazi na kuwasiliana.

Niliwaambia kwamba iwapo itapita miaka miwili hajaipitisha sheria hiyo, naye atakuwa kama hao anawashutumu, au atakuwa mbaya kuliko wao.

Kwa mbwembwe, waliniambia kwamba akiingia tu madarakani, hiyo ndiyo itakuwa kazi yake ya kwanza. Hakika, walijidanganya wenyewe; maana leo hii ni mwaka wa sita tangu Kikwete aingie madarakani, sheria mbaya zilizopingwa mfululizo kwa miaka ipatayo 19 sasa, bado zinafanya kazi ya kuwasaidia watawala kutunyanyasa.

Miaka mitatu iliyopita, baada ya wadau wa habari kumsukuma Kikwete atimize ahadi yake hiyo, serikali yake ikaagiza rasimu iliyokuwapo ichakachuliwe, yachomolewe mambo kadhaa na kuingizwa mengine yatakayolinda masilahi ya watawala.

Wadau walipoitazama rasimu mpya ambayo serikali ilikuwa inajiandaa kuipeleka bungeni, wakagundua vimechomekwa vipengele vichafu kuliko hata sheria hizi mbaya tunazopinga. Wakaikataa.

Baada ya mabishano ya muda mrefu, serikali na wadau wakakubaliana inadaliwe miswada miwili - mmoja ukihusu haki ya kupata habari, na mwingine ukihusu utoaji wa huduma za habari – ili zitungwe sheria mbili ambazo zitasimamia uhuru na haki ya habari nchini.

Hata baada ya jitihada zote hizo za wadau, serikali ya Kikwete bado imegoma kupeleka miswada hiyo bungeni.

Mwaka jana mwanzoni, nilimhoji Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwanini serikali yake inagoma kupelela miswada hiyo. Akaahidi mbele ya wahariri, ofisini mwake Ikulu Dar es Salaam, kwamba serikali ingepeleka miswada hiyo katika kikao cha Aprili 2010.

Pinda alidhani anatudanganya sisi, kumbe alikuwa anajidanganya. Hadi leo, imepelekwa miswada mingi – tena mingine ya hovyo tu – na zimetungwa baadhi ya sheria zisizotafitiwa na zisizotekelezeka, lakini serikali ya Kikwete imegoma kutunga sheria zinazoboresha mawasiliano ya umma, na kufuta sheria kandamizi.

Katika mazingira haya haya, bado wapambe wa Kikwete wanapata uajsiri wa kumpa sifa za kijinga eti ametoa uhuru wa habari. Kigezo wanachotoa, eti anavumilia kukosolewa na vyombo vya habari.

Ajabu ni kwamba hata yeye ameingia katika kundi hili la sifa za kijinga. Nilimsikia mwezi uliopita akihutubia makada wa CCM (walioitwa wazee wa Dar es Salaam), akadokeza kwamba yeye si dikteta kwa sababu magazeti yanamkosoa, na bado wanaomkosoa wanaendelea kuwapo tu!

Hii ni kauli ya mtu anayetamani kuwapoteza wanaomkosoa, lakini bado ana dhamiri hai; anaogopa matokeo.

Kwa vyovyote vile, wanahabari wamesherehekea miaka 50 ya uhuru wakiwa watumwa wa sheria kandamizi.

Na wanaompa JK sifa hizi za kijinga, hawajatafiti na kugundua uhuni wa serikali unaoendelea chini chini dhidi ya wakosoaji wa serikali. Hawataki kuhoji sababu ya jeuri na ukaidi wa serikali kukataa kutunga sheria nzuri na kuondoa mbaya.

Hawataki kutambua kwamba yaliyotokea katika ufisadi wa EPA, Richmond, Meremeta, Tangold, Deep Green na mwingine, yaliitisha serikali kwamba iwapo wananchi watatungiwa sheria safi za kuwasiliana na kupeana habari, dola hii dhalimu itaanguka kirahisi, na mapema kuliko ilivyodhaniwa.

Ni wazi, Kikwete na wenzake wanachelewesha sheria hizi kwa kuwa wanataka kufaidi siku chache walizobaki nazo madarakani. Kama apendavyo kusema mzee Ndimara Tegambwage, watawala wanafunika nyuso zao kwa viganja kama nyani, wakidhani hatuwaoni.

Mashabiki wa sifa za kijinga hawataki kujiuliza kwanini CCM na serikali wanakula njama kuwafukuza wanafunzi wa vyuo wanaodai haki zao kwa sauti.

Hawajaeleza kwanini CCM na serikali wanapanga kuua uhuru wa kuwasiliana, na kujumuika, kwa kupiga marufuku mikusanyiko ya wananchi wanaokerwa na mwenendo wa serikali katika masuala kadhaa.

Inawezekana wanajipendekeza kwa watawala. Maana katika hali ya kawaida, mtawala yeyote anayeboresha mazingira ya utendaji wa kazi fulani, hatafanya hivyo kwa tabasamu na utashi binafsi tu; bali kuwa kujenga mazingira ya kisheria ya kulinda uhuru, haki, na wajibu wa raia na serikali.

Ni upuuzi kumpa JK sifa za kijinga, au kujaribu kusisitiza kwamba Rais Mkapa alikuwa mbaya kuliko huyu wa sasa katika suala la uhuru wa kujumuika na kuwasiliana.

Chini ya Rais Mkapa, kuna watu walishambuliwa kwa maneno makali, vitisho, na hata kuvuliwa uraia. Kuna vyombo vya habari vilifungiwa. Vingine vilifutwa kabisa.

Rais Mkapa alipopata fursa aliitumia naye kurusha vijembe, na kulumbana na wakoasoaji wake.

Chini ya Rais Kikwete, kuna mabadiliko ya utendaji, si ya mfumo. Wakosoaji wa Kikwete wameendelea kuandamwa. Tofauti iliyopo sasa ni kwamba Kikwete mwenyewe hafoki, wala halumbani nao; lakini anayosema dhidi ya wanaomkosoa yanawasaidia vibaraka wake na makachero kuwaandama kisirisiri.

Ndani ya miaka sita ya Kikwete, vipo vyombo vya habari vimefungiwa. Mwaka jana, ilipitishwa amri isiyoandikwa, ya chini chini, kuzuia usajili ya chombo chochote cha habari hadi uchaguzi mkuu upite.

Baadhi yetu ni mashahidi jinsi ambavyo tumekuwa tunasumbuliwa, tunashambuliwa na kuandamwa na serikali ya Kikwete kwa sababu ya maandishi yetu.

Chini ya serikali hii, wapo waandishi wameshambuliwa moja kwa moja; wengine wamemwagiwa tindikali. Wapo waliokatwa mapanga na waliolishwa sumu. Ipo mipango mingi michafu ya serikali hii iliyopanguliwa kwa nguvu za Mungu na kwa msaada wa Wasamaria wema.

Na sasa tunaendelea kushuhudia, kwa mara ya kwanza, wakosoaji wa Kikwete wakifikishwa polisi na mahakamani kama mkakati wa kuwadhoofisha. Walianza na wanasiasa; sasa wameanza kuingia hata kwenye vyombo vya habari.

Ni mkakati wa makusudi, na wa muda mrefu, unaolenga kunyamazisha sauti zinazozungumza kisichowafurahisha watawala.

Tulishasema huko nyuma, na ni hitaji la kihistoria tu, kwamba hata wakitukamata sote wakatufunga na kutuua, wataibuka wengine wakali kuliko sisi; watachukua hatua kali kuliko hizi zinazowatisha watawala.

Nguvu yetu ni moja. Hatutetei masilahi yetu binafsi, bali ya wanyonge walio wengi wanaoishi maisha ya taabu kwa sababu ya hila. Yetu si kauli ya wakosoaji tu, ni kauli ya Mungu! Ole wao wanaoshindana naye kwa mitutu ya bunduki, polisi na magereza.


Watashinda kwa sifa za kijinga?
 
Hongera sana bro ngurumo,tumekuelewa sana...mungu akubariki ila kumbuka vita hii si lele mama bt "no retreat no surrender" kwa hii serikali dhaifu.
 
Kweli nimekubali, Bro.ngurumo, ni ngurumo ,hivi watawala wetu hawayasikii haya au wanaziba masikio kwa pamba tuu kazi ni kucheka cheka tuu?napita nitarudi...
 
Kweli nimekubali, Bro.ngurumo, ni ngurumo ,hivi watawala wetu hawayasikii haya au wanaziba masikio kwa pamba tuu kazi ni kucheka cheka tuu?napita nitarudi...

Wanamsoma na kumsikia kwa sana Ndugu. Watawala wetu ni kama Jiwe. Unalijambia lipo kimya kama halisikii, kumbe limesikia!
 
My brother, my chief. Always u have been a role model in logical analysis, taking things and thinking about them in a bigger picture, extra miles, extreme beyond...writing of the people, for the people and by the people...the voice of the commoners, whom majority of them their voices could not be heard by the rulers. Hujawahi kulewa sifa za kile unachokifanya. Maana unao wajibu wa kijamii kufanya ukifanyacho na Watanzania wanayo haki ya kukuona ukifanya hivyo wakati wote.

Many of us will try to do the same, stepping and fitting ourselves in ure shoes. I wish the journos in our mainstream media could fall suit in analytical reporting and feature writing, to serve no body else but the society
 
Ansbert Ngurumo, I salute you. Makala hii imendikwa kwa ufasaha iliojaa ushahidi wa matukio. Ngurumo amebobea na anaandika bila woga tatizo mawazo mazuri kama haya hayafanyiwi kazi na watawala. Kwangu mimi hii makala ningeweza kuiweka katika makala bora tatu za mwaka 2011
 
Hongera Ngurumo kwa uchambuzi wa kina na umahiri wa hali ya juu. Vijana Watanzania wengi wanajiunga na wazalendo jasiri kama Ngurumo na kwa hakika tutasonga mbele. Siku za dhuluma, uonevu na umaskini zitakoma. Mshikamano wa hawa ni muhimu.
 
Mimi nilibadili uamuzi wangu wa nani nimpigie kura 2005 baada ya kumsikiliza JK alivyokuwa anatoa hotuba,
 
Brother Ansbert heshima kwako. Kwa uchambuzi huu, hakika sina budi kukuvulia kofia. Kalamu zote zingeandika hivi, sijui kama watawala wetu wangekenua meno wanapokutana na wananchi. Mungu akubariki na kukutia nguvu na kuweka ulinzi juu yako. Binafsi nimekata tamaa na kikwete. Sioni anachofanya cha maana zaidi ya kuzunguka dunia na kukaribisha wageni maarufu nchini kana kwamba ndiyo kazi tuliyomtuma. Ninachofanya kwa sasa ni maombi tu ili Mungu atuwezeshe tumalize salama na huyu Dr wa heshima na tupate kiongozi makini wa kutuondoa kwenye lindi hili kubwa la umaskini.
 
Back
Top Bottom