Sakata la OBC: Asasi za Kiraia zafungua kesi ya kikatiba

jamadari

JF-Expert Member
Feb 13, 2010
295
92
Mashirika manne yasiyo ya kiserikali, yamefungua kesi ya kikatiba ambapo walalamikiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Ngorongoro, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kampuni ya uwindaji ya Ortello Business Corporation (OBC) kwa kukiuka haki za msingi za wakazi wa vijiji vinane vilivyopo eneo la Hifadhi ya Wanyama ya Loliondo, wilayani Ngorongoro.

Mashirika hayo kwa pamoja Pastoralists Indigenious Non-Governmental Organisations (PINGOs), Ngorongoro Non-Governmental Organisation Network (NGONET), Ujamaa Community Resource Team (UCRT) na Legal and Human Rights Centre (LHRC), yamefungua kesi hiyo katika ofisi ya Msajili Mahakama Kuu Arusha juzi, ambapo imepewa namba 15 ya mwaka 2010 na wamewasilisha chini ya ombi la dharura.

Yameiomba mahakama kuwaamuru walalamikiwa kuacha mara moja na kusitisha kabisa unyanyasaji, kuwaondoa wakazi hao kwa nguvu katika maeneo yao, udhalilishaji, ubaguzi, kuchoma moto maboma na mali zao.

Pia wanaiomba mahakama imwamuru malalamikiwa wa tatu ambaye ni OBC kuacha mara moja na kusitisha kabisa mpango au mipango yoyote ya kuanzisha vitalu au ukanda wa uwindaji wanyamapori katika eneo la hifadhi.

Mashirika hayo pia yanaiomba mahakama kumwamuru mwekezaji OBC kuondoa mtandao wa mawasiliano wa kigeni aliojiwekea, kusitisha uendeleshaji wa kiwanja cha ndege katika hifadhi na huduma zake.

Aidha, wameomba mahakama iwaamuru walalamikiwa kulipa gharama za kesi hiyo na pia wameomba kupewa nafuu nyingine yo yote ambayo mahakama hiyo itaona kuwa wanastahili kupewa.

Hati ya mashtaka inasema suala lililopelekea kufungua kesi hiyo ni kufuatia ukiukwaji wa haki za msingi na wajibu chini ya Sheria ya Haki za Msingi na Utekelezaji wa Wajibu ya 1994, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 na kuhusu uvunjifu wa ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wamezitaja Ibara hizo kuwa ni ya 12, 13, 14, 15, 16(1),17(1), 18, 21(2),24, 27, 28, na 29(20 ambavyo walalamikiwa wanadaiwa kukiuka kwa wakazi wa vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Olorien-Magaiduru, Arash, Oloipiri, Malambo, Piyaya na Maaloni ndani ya eneo la Hifadhi ya Wanyama ya Loliondo (LGCA).

Mawakili wanaotetea mashirika hayo, Daimu Halfani, Clarence Kipobota na Fulgence Masawe, kwa pamoja wanadai kuwa kuanzia Julai 4, mwaka jana, wakazi wa vijiji hivyo, waliondolewa kwa nguvu katika maeneo yao pasipo kuzingatia misingi ya haki za binadamu na kitendo chochote cha kuendelea kuwaondoa watu hao ni kinaenda kinyume na Ibara ya 14, 16(1), na 24 ya Katiba.

Wanadai pia barua iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro yenye kumbukumbu namba DC/NGOR/D.8/20/23 ya Mei 18, 2009 ikidai kuwa ni halali, imekwenda kinyume na Ibara ya 13(1) ,(4), (6) (a), 17(1) na 29(2) ya Katiba.

Mawakili hao pia wamedai kuwa wanavijiji hao wanayo haki ya kuishi, kukaa, na kutumia maji na ardhi hiyo kwa ufugaji kama iliyoanishwa katika Sheria ya Uhifadhi ya Wanyamapori ya 1974, Sheria ya Ardhi ya 2002, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) 2002, na Ibara 17(1) na 24(1) za Katiba.

Wamedai pia kitendo cha serikali kumruhusu mlalamikiwa OBC kujenga kiwanja cha ndege ndani ya eneo la makazi ya wanyama, ujenzi wa nyumba za kudumu na za muda katika eneo hilo na kutumia mtandao wa Kiarabu ndani ya Tanzania kwa kuizuia mitandao ya Tanzania kufanya kazi eneo hilo la LGCA ni uharibifu wa raslimali za taifa, utaifa, amani na usalama wa nchi na hivyo ni kinyume na Ibara ya 18(c) , 27 na 28(1) za Katiba.

Wametaja madai mengine kuwa ni matumizi ya Polisi wa Kutuliza Ghasia, vyombo au taasisi nyingine yoyote ya serikali kuwanyanyasa na kuwasumbua, kuwabagua wakazi wa eneo hilo katika haki yao ya msingi ya kufuga na kufanya kazi katika maeneo hayo inapingana na Ibara ya 13(1)(3)(6(e), 14, 15(1), 16(1), 17(1), 18©, 22(1) na 29(2) za Katiba.

CHANZO: NIPASHE
 
Hivi majuzi Januari 5 mwaka huu gazeti la Raia Mwema liliandika habari kuhusu Ripoti ya tume iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga likidodosa ripoti hiyo kuzilemea NGO's zinazojihusisha na maisha ya wafugaji, ukiisoma (bofya hapa)utagundua kwamba hata wataalamu wanaotegemewa na nchi yetu ni tatizo kwa maendeleo yetu, kwamfano tume hiyo ya Shaban Malipula inashawishika kuona kwamba kiasi cha dollar milioni 2.7 kilicho changiwa na kampuni ya uwindaji ya OBC kwa kipindi cha miaka 13 ni kikubwa sana kwa maendeleo yetu bila kutafiti kwamba kwa kipindi hicho kampuni hiyo imesafirisha wanyama wenye thamani ya dollar ngapi?? Kwa kifupi kiasi hicho ni sawa na kuachia tani moja ya karanga kuondoka nchini nasisi kupewa kopo moja la peanut butter.

Tuzinduke waTZ, nchi inakwisha, tuliowapa dhamana wamekunja mikono kisa wameshiba kakopo kamoja ka peanut butter...
 
Back
Top Bottom