nasrimgambo
JF-Expert Member
- Jan 10, 2017
- 1,898
- 2,459
NGADA!
Frank alimkazia macho kaka ake, na kuvimbisha uso wake, na kukaza sauti, na kumwambia tena na tena.
“usim ‘shoot’, achana nae”
“Aroni, achana nae ushampiga, kaumia, achana nae, tusepe ‘home’”
Wakati huo kaka ake alikuwa kashikilia bunduki mikonomi mwake. Uso kauvimbisha kwa hasira huku kanyoosha mikono iloshika bunduki kumuelekea Dullah aliyekuwa kasimama mbele yao, huku damu zikimvuja mdomoni, na huku kachoka taabani kutokana na kipigo alichopewa na huyo kaka ake Frank, Aroni.
Ilikuwaje mpaka kufikia hatua hiyo ya Aroni kudhamiria kabisa kumuua Dullah?
Jibu la swali hilo ni simulizi ndefu, nayo kuisimulia yaanza kama ifuatavyo;
Frank Sultan, alikumbuka vitu vingi vya udogoni mwake, miaka hiyo ya 2000. Kipindi hicho baba ake mzee Sultan alipokuwa hai.
Enzi hizo nyumbani kwao waliishi kwa furaha sana, wakiwa yeye Frank, pamoja na kaka yake, yani huyo Aroni na mdogo wao wa kike Lulu, pamoja na wazazi wao, bwana Charles Sultan na ‘Mrs’ Salome Sultan.
Waliishi kwa furaha sana nyumbani kwao mitaa ya huko Kimara, na maisha yao yalijaa kumbukumbu nyingi za kufurahisha ikiwamo ‘picnic’ na ‘dinner outs’ za kifamilia, sikukuu za krismasi na mwaka mpya na kumbukumbu nyenginezo tele.
Ila, mambo yalianza ingia doa pale ilipotukia siku ambayo mzee Sultan alipogundulika ana kansa ya utumbo. Kwa ujasiri mzee wa watu na mkewe walijaribu kupambana na hilo janga na kuanza kufuatilia popote pale palipo na tiba ya janga hilo.
Ndugu na jamaa walijitahidi kuonesha ushirikiano, na Bi. Salome alijitahidi kuwa jasiri ili kuwatia watoto zake moyo wa matumaini na wasiingie katika hali ya huzuni.
Ila wakati ukawadia na mzee huyo akaaga dunia na nyuma akaacha mkewe na watoto zake watatu aliokuwa akiwapenda sana.
Sasa Salome aliyekuwa mama wa nyumbani enzi za mumewe yu hai akawa ndiye mchumaji na mlezi wa familia.
Hali ya maisha ikawa si ile waliyoizoea tena katika hiyo familia yao. Mambo yakabadilika. Baba hakuwapo tena, hakukuwa na pesa ya pikniki wala ‘family dinner outs’. Magari ya nyumbani ikabidi yageuzwe taksi na moja likaingia ubovu likawa limeegeshwa kwenye uwa wa nyumba hadi likaharibika zaidi. Bi Salome hakuwa tena na ratiba za saluni kuseti nywele na hakuitwa tena kwenye vikao vya kamati za ‘vitchen party’ na ‘send off’ za majirani zake wa huko Kimara
Familia yao ikawa ya mama ahangaike na biashara ya kuuza chakula pale kwa utingo wa magari ya abiria katika stendi ya Ubungo, ndiyo familia ipate pesa ile na kugharimu gharama zote za maisha.
Kwa bahati nzuri sana, ofisi aliyokuwa akifanya kazi marehemu mzee Sultani ikajitolea kuwa itawasomesha Frank, Aroni na mdogo wao Lulu hadi watakapomaliza, hivyo kwa nafasi hiyo wakawa na uhakika wa kuendelea kusoma katika shule zao za ‘private’ walizokuwa wakisoma toka awali kabla umauti haujampata baba yao.
Hapo sasa ndio Frank alikumbuka vizuri, kuwa mambo yakaanza kwenda mrama hata zaidi.
Katika hali isokuwa ya kawaida, Aroni, mtoto wa kwanza na mkubwa katika familia na aliyetegemewa na mama ake kuwa akifanya vizuri darasani basi ataweza siku moja kuigomboa familia yao toka lindi la umaskini waliouingia na kurejesha familia kule kwenye maisha bora waliowahi ishi hapo zamani, akaanza kufanya vibaya darasani.
Salome alishtuka sana kuona jinsi mwanae anafanya vibaya darasani, ilhali Aroni wake huyo alikuwa ni mtu wa ‘top five’ katika kila ripoti toka chekechechea hadi la saba.
Hatimaye na mtihani wa kidato cha nne Aroni akafeli kabisa na kukosa sifa za kuchaguliwa kwenda kidato cha tano na hata chuo kwa ngazi ya cheti.
Bi. Salome alichanganyikiwa sana kwa matokeao hayo ya mwanae. Yeye mama mtu alilia kwa uchungu kuliko mwanae aliyefeli. Katika wiki hiyo ya matokeo ya kidato cha nne, bi Salome nusura agongwe na gari katika eneo la Ubungo mataa, na kumfanya aonekane kama kachanganyikiwa na wavukaji wengine wa barabara katika eneo hilo la Ubungo, huku dereva alomkosakosa kumgonga aliyekuwa baba mtu mzima aliyekosa ustaarabu akamrushia matusi ya nguoni, “ we mama pambavu zako unakalisha makalio** njiani badala ya kuvuka tuta kusinya na magari ufe punguani wewe”, hivyo ndivyo alisikika dereva huyo akimtukana bi. Salome hapo Ubungo.
Kwa maombi na sala bi Salome alimuomba mungu amshike mkono, amnyanyue, amfute machozi, ampe tumaini, azulu nyumba yake na familia yake kama anavyozulu na kubariki nyumba nyengine na familia nyenginezo.
Ila mambo waala hayakwenda kama dua zake kwa mungu alivyozipangilia, ndio kwanza ‘picha la matatizo yake likaanza kunoga’
Kwanza Aroni akagoma kurisiti, “maisha si lazima, kusoma, mimi nitatoboa kivingine, shule nitakupotezeea tu hela yako mama”, hiyo ndiyo kauli ambayo Aroni alimpa mama yake.
Kauli hiyo ilimpa mama ake wakati mgumu na hasira moyoni.
“Unafeli shule, hutaki kurisiti. Halafu wewe mtoto wa kiume tena mkubwa ninae kutegemea. Unadhani utafanya nini cha maana katika maisha yako, utaishia kuwa mpiga kiwi wa viatu vya wezio watakao kuwa wanaenda ofisini, wewe mpumbavu”, aliongea Salome huku machozi yakimlengalenga.
Kwa shingo upande Aroni akajiunga na shule ya kurisiti. Ila bado hakunyooka. Chanzo kikiwa, marafiki. Hao marafiki zake wapya, walikuwa kundi la ajabu sana. Siku moja bi Salome akaitwa shuleni hapo ambapo Aroni alikuwa akisoma na akaelezwa na walimu kuwa Aroni anatumia madawa ya kulevya na kuwa jopo la rafiki zake shuleni hapo wengine washatimuliwa shule kwa tabia ya utumiaji.
Maelezo hayo ya walimu yalimtia simanzi isio kifani, aliona kuwa Aroni anamkatisha tamaa, “Hakya mungu utatafuta pa kukaa Aroni, hakya mungu, yani mimi mama ako natafuta riziki kwa shida na unaona dhiki zetu katika familia lakini bado unatia ujinga huko shuleni badala ya kufanya vizuri upige hatua”, aliongea bi Salome akimwambia Aroni waliporejea nyumbani huku machozi yakimtoka.
Na hiyo haikuwa mara ya mwisho kuitwa shuleni kwa Aroni, kwa maana kwa mara ingine ya pili bi Salome aliitwa shuleni kwa Aroni. Safari hii akakuta kesi kuwa Aroni alikuwa kampiga mwalimu na alithibitika kuuzia wezie bangi na tena alihusika katika kesi ya kushikashika wanafunzi wezie wa jinsia ya kike bila heshima kwenye maungo ya mwili, hivyo basi uongozi wa shule ukaamuru afukuzwe shule.
Bi Salome akaingia simanzi ya kulingana na mfiwa, hilo lilikuwa ni pigo la aina yake, ambalo hakuliona likija. Aroni alikuwa anamkatisha tamaa mama yake kabisa.
Mambo wala hayakuishia hapo, ‘picha likaendelea’. Wakati sasa yupo nyumbani baada ya kutimuliwa shule Aroni akaanza uraibu wa madawa ya kulevya, bangi na aina nyenginezo za madawa. Akaanza sasa na kubadilika hata tabia, akaanza kuwa mkimya, akaacha kujichanganya na watu, muda wote kachooka, muda wote macho mekunduu.
Mbaya zaidi kwa kuwa alikuwa hana la maana alilokuwa akifanya, akaanza na tabia mbaya ya wizi. Akiona mia tano imesahauliwa sebuleni kwao, kabeba, akikuta ndani kuna chenye thamani, iwe kiatu, kikombe kipya ama chochote, ikawa ni halali yake, alikibeba na kwenda ‘kukipiga bei’.
Siku moja mama ake alipigiwa simu kuwa Aroni yu hoi anakimbizwa hospitali baada ya kuzirai kutokana na kuzidisha matumizi ya madawa ya kulevya, kwa maana utumiaji wa bangi kidogo kidogo ukageuzwa ukawa utumiaji wa ‘cocaine’ na mchanganyiko wa madawa mengine.
Salome alipofika hospitali pamoja na mwanae Frank kumuona Aroni walishuka sana moyo. Frank alisimama akimtazama kaka yake aliyelala kwenye kitanda cha humo wodini hospitali. Frank aliona jinsi Aroni alivykuwa kachoka, kakonda, mdomo umelegea kabisa, aliona jinsi kaka yake alivyokuwa na muonekano wa kiteja kabisa, hata haikumuhitaji mtu kuuliza ikiwa Aroni alikuwa ni mraibu wa madawa ya kulevya, uteja wake ulionekana kwa macho mara moja.
“Hivi kweli wewe ni kaka yangu mimi?”, Frank alimuuliza Aroni
“Hivi kweli wewe ndiye Aroni, shujaa wangu, kaka yangu”
“Nakumbuka enzi tukiwa wadogo nilikuwa nakutazama wewe na kuiga kila kitu ulichokuwa ukifanya”, “nakumbuka jinsi ulikuwa ni wewe ukifanya vizuri darasani, mpirani kiwanjani, ukiwa na sifa tele, ukapendwa na kila mtu mtaani, na mimi mdogo wako nilikuwa natamani kuwa kama wewe, Aroni”, “Ila sasa Aroni yule wa mfano amekwenda wapi, umebaki wewe, Aroni teja, Aroni wa ajabu, Aroni wa kuogopwa kwa wizi na mambo ya hovyo”, Frank aliongea maneno hayo kwa uchungu mwingi huku machozi yakimlenga, wakati huo Aroni mwenyewe alokuwa akiongea nae ndio kwaanza alikuwa hajitambui kwa maana alikuwa bado hajazinduka toka huko kuzirai alikozirai kutokana na kuzidisha uraibu. Wakati Frank anaongea maneno hayo mama yake, bi Salome alikuwa kakaa pembeni ya kitanda cha Aroni, huku kamshikilia Aroni, macho yake yakiwa mekundu kwa kulia, na alihuzunisha, sasa bi Salome alikuwa kakonda, kaisha kabisa, alikuwa ni mwanamke aliyejaa uchungu mwingi, hata haikuhitaji mtu kuuliza kulijua hilo, maumivu yake ya moyoni yalijidhihirisha usoni na mwilini kwa jinsi alivyokondeana na kuchoka.
Basi, taratibu Frank akageuka na kutoka humo wodi alimolazwa kaka yake na akaondoka huku machozi yakimtoka, akimuacha mama yake kakaa hapo pembeni ya kitanda alicholazwa Aroni, Frank aliondoka hapo hospitali huku akilia kwa uchungu, hata watu alokuwa akipishana nao wakawa wakimshangaa kwa jinsi machozi ya uchungu yalivyo mtiririka.
...............................
“Frankiiii, uko wapi wewe”, ilisoma meseji iloingia kwenye simu yake Frank, meseji yenyewe ilitoka kwa Recho. Recho alikuwa ni mwanafunzi mwezie Frank, walisoma wote chuoni CBE, ambako walikuwa wote ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza wakisomea shahada.
“Nakupigia, hupokei simu zangu, nakutumia meseji hujibu, mbona unanifanyia hivyo wewe, haya bwana, ila sio vizuri hivyo”, ikasoma hivyo meseji ya pili ambayo Recho alimtumia Frank. Wakati Frank akisoma meseji hizo alikuwa kwenye daladala akirejea huko kwao Kimara akitokea hospitali kumuona Aroni. Hakutaka kujibu hizo meseji, ila alizisoma na kucheka jinsi Recho alivyolalamika kutaka kujibiwa meseji zake.
Frank alimpenda sana Recho, na Recho alimpenda sana Frank, na hivyo mara moja tangu waonane na kujuana hapo chuoni CBE, wakaanza uhusiano. Recho alikuwa msichana mzuri, mrembo, mwenye akili sana darasani, mpole, katulia japokuwa alikuwa yuko ‘very social’ hadi ikamkera Frank baadhi ya nyakati. Kwa maana binti huyo ambaye kwao walikuwa na uwezouwezo wa kifedha ‘kimtindo’, alipenda sana kuhudhuria ‘party’ na ‘clubs’ kila alipopata nafasi na kila mara alipokwenda huko sehemu za starehe alikuwa akipenda kumbeba Frank waende wote, ila tatizo likawa Frank hakupenda kwenda huko kwenye klabu za usiku na ‘party’ za mara kwa mara. Kwasababu, kwanza Frank alijiona kuwa hakuwa na pesa za kuhudhuria huko kila mara, halafu pia Frank hakupenda jinsi ambavyo kila wakienda huko ni Recho ndo alikuwa akitoa fedha ya kufanyia lolote wawapo huko.
“Kwahiyoo, wewe hupendi kwenda ‘party’ kwasababu, hutaki kugharamiwa na mimi?”, Recho alimuuliza Frank, swali hilo katika siku moja, “ndiyo”, alijibu Frank na kumtazama Recho machoni,
“Ok, isiwe shida, hatutaenda tena kwenye ‘parties’,”
“si hivyo tu, kwenye party na kwenye klabu tuache kwenda, kwasababu kwanza sina fedha za kwendea huko, wewe pesa hizo unazoendea huko kama zimekuzidi sana nipe mimi kwa maana nina matumizi makubwa ya pesa ila ndo hivyo sina”, aliongea Frank, na kumchekesha Recho.
Mbali na Recho, Frank alikuwa na rafiki yake aliyeitwa Talib. Walishibana kwelikweli na rafiki yake huyo, kwa maana walisoma wote shule ya msingi na sekondari na wakaja kukutana tena chuo kikuu
Ila tafauti na Frank, Talib alikuwa ni ile aina ya watu waliopenda kuiga na kujaribujaribu kila jipya lililoingia mjini miongoni mwa vijana. Tabia yake ya kuigaiga, haikuwa nzuri na ingeweza kumponza hata Frank akawahi kumuonya rafiki yake huyo kuwa , tabia ya kuigaiga itampeleka pabaya.
Siku moja Frank alienda kutembelea hosteli alikoishi Talib. Kufika huko akakuta rafiki yake huyo na wezie wa hosteli hiyo wameshikilia bangi wanavuta.
Frank alimtazama rafiki yake jinsi alivyokuwa akifurahia ‘hiyo kitu’. Frank aliona jinsi Talib na wezie wa hostelini hapo walifurahia kuvuta hiyo bangi.
Kichwani mwake Frank, ikamjia sura ya kaka yake. Ikamjia taswira ya kaka yake enzi anaanza kuvuta bangi. Frank akawaza na kukumbuka jinsi kaka yake alianza kuvuta bangi hivyohivyo kidogo kidogo ila hatimaye akajiingiza kwenye uteja wa ‘cocaine’.
Mara ghafla taswira ya kaka ake ikamtoweka kichwani na Frank akawa akiwaangalia tena Talib na wana hosteli wezie walichokuwa wakifanya. Ghafla hasira zikampanda Frank na akavimbisha uso na kumtazama Talib, ambaye nae alimuona Frank jinsi alivyomtazama na hata akajishtukia na kuweka bangi zake chini na kuacha kuvuta.
Kwa hasira Frank akatoka ndani ya hosteli, nyuma yake Talib akamfuatia hadi nje.
“Hivi mnajua mnachokifanya?”, Frank alimuuliza Talib kwa hasira, “mnachezea akili zenu”, “mnatafuta ukichaa ilhali ninyi ni wazima”, Frank aliendelea kuongea kwa hasira na kumfokea Talib, “Acheni upuuzi washkaji, acheni upuzi, Talib, acha upuzi”
“ kaka yangu, kaka yangu mimi, Aroni unamfahamu Talib, na unafahamu kuwa kawa kama chizi, kama chizi kisa hayo mabangi ambayo baadae akachanganya na ma ‘cocaine’ na madawa mengineyo”, aliongea Frank, sasa hasira zake zikaambatana na kulia.
“Kawa kama chizi, si wa kutegemewa kwa lolote, kisa ni hayo madawa, leo hii Talib nakuja hostelini kwenu ndugu yangu nakukuta na wewe umeshikilia ‘weed’ unavuta na wale wapuzi wezio, wote akili zenu fupi”, “unajua nini mdau, wewe kama unavuta hayo mabangi nenda kavute ila nakwambia hiyo ni hasara kubwa sana, na unanisikitisha rafiki yako, inanitia uchungu, iwaje kaka yangu kaharibikiwa na madawa na leo hii nakuona rafiki yangu unaanza ulimbukeni wa kuiga iga matumizi ya kitu hicho cha hovyo”, alimaliza kuongea Frank, kwa uchungu na kuondoka na kumuacha Talib akimuangalia.
Kwa hasira Frank aliondoka hapo hostelini kwa kina Talib na kuingia kwenye kituo cha mwendokasi. Akiwa hapo kwenye kituo, ili kupanda basi kurejea kwao Kimara, mara simu yake ikaita. Kuicheki, ilikuwa ni mama yake anayepiga, haraka akapokea, mara akawa akisikia kilio cha mama yake simuni.
“mama, kuna nini huko?”, alihoji Frank,
“Hivi unaweza amini, Aroni kaondoka sober, yupo hapa nyumbani, kwanza dawa zenyewe keshaacha kutumia, hivi ninakwambia inasemekana kaanza upya urafiki na yule rafiki yake anayeuza madawa, yule anayeitwa Dullah”, aliongea bi. Salome, huku akilia.
“mama mama tulia nakuja nyumbani nisubiri nakuja”, alisema, na kuingia ndani ya basi la mwendo kasi.
Ni ugomvi mkubwa mkubwa sana ambao Frank aliukuta nyumbani kwao. Wapita njia na majirani wote waliusikia ugomvi ulokuwa ukiendelea ndani mwao. Bi Salome alikuwa kamjia juu Aroni, kwa upuuzi wake alokuwa akiuleta kwenye familia.
“pumbavu sana wewe, unanikatisha tamaa na kunitia hasira, hivi huoni gharama ninazoingia kujaribu upone, ili uwe na akili za binadamu sio kuwa na akili za kizezeta”, “nimehangaika sana Aroni, mimi mamako, makanisa nimemaliza kutaka kukuombea na hadi kwa waganga nimefika kutafuta kukugomboa toka kwenye majanga uliyojiingiza, ila la!, mpuzi wewe huelewi kiasi cha magharama ninayo poteza na jinsi moyoni ninaumia”, alifoka Salome, huku mkononi kashikilia mwiko akitaka kumpiga nao Aroni.
Frank alikuwapo mahala hapo, akimuangalia kaka ake kwa uchungu na hasira, wakati huohuo, Lulu, mdogo wao alikuwapo pia hapohapo akimuangalia jinsi mama ake alivyofoka kwa hasira huku machozi yakimlenga pia.
“Nimechoka nakuomba toka kwenye nyumba, hii”, bi Salome alianza kumfukuza Aroni, na kisha akaelekea chumbani kwa huyo Aroni na kutoka humo na begi lake la nguo na kufungua mlango na kutupa begi nje na kumgeukia kwa hasira na kuanza kumsukuma nje ya nyumba, “toka , toka sikutaki kwangu unanitia hasira, toka kaa huko kwa wahuni wezio”
Wakati huo Aroni mwenyewe sasa akaanza kulia, “niende wapi mama, niende wapi, usiku huu unaoingia”
“nenda huko kwa hao wanokuvutisha madawa, maana ndo unawathamini kuliko mimi mama ako mzazi niliyekuzaa na ninae kuangaikia”, aliongea mamake kwa hasira na kumfukuza toka sebuleni na kumtoa Aroni nje ya nyumba usiku huo.
Frank na Lulu wakawa wamebaki wakimtazama mama yao jinsi alivyokuwa akirejea ndani baada ya kumfukuza Aroni.
Mara Frank, akatoka ndani ya nyumba na kwenda huko nje, hadi mahala ambapo Aroni alikuwa kasimama na begi lake la nguo, “utaenda wapi usiku huu”, Frank alimuuliza kaka ake, huku hasira zikimpanda na huku akimuangalia kwa kuvimbisha uso.Ghafla Frank akajikuta kamrushia kaka ake ngumi moja nzito shavuni, “unanitia hasira Aroni, unanitia hasira. Mimi nilidhani kwa kuwa umeenda kule wanakoita ‘sober’ basi sasa ungenyooka na kuacha huu upuzi wa mihadarati ila ndio kwanza unarejesha urafiki na rafiki zako wabovu na kuacha dawa za sober, na wewe unakoelekea utarudi tena kuwa mraibu uliyechoka kama kipindi kile unaenda huko ‘sober’”, aliongea Frank kwa hasira.
“Nilipokuwa mdogo nilikuwa nakuona jembe, nilikuwa nakuona jembe langu Aroni. Nilikuwa najivunia nina kaka. Ulikuwa mfano wangu katika kila kitu. Ulikuwa unafanya vizuri darasani ulikuwa ndio kigezo changu cha kufanya vizuri kwenye kila kitu. Ila ona sasa jinsi uliyokuwa sasa. Teja, teja la unga” alilia Frank, “teja la unga, kaka yangu ni teja la unga”
“Hivi Aroni unajua kuwa kama ungekuwa hujajiingiza katika huu upuzi wa madawa leo hii ungekuwa ushamaliza chuo, pengine una ajira, pengine hata ushaoa na una familia yako, bimana wezio uliosoma nao saa hizi wana maisha na familia zao, wanafanya mambo ya maana. Ila ona wewe ulichofanya katika maisha yako umekuwa teja, teja la unga”
Maneno hayo yalimliza Aroni sasa, akili yake ikafunguka sasa,na akaona ilikuwa kweli, yeye alikuwa mfano mzuri sana kwa mdogo wake hapoo zamani, alikuwa hodari katika kila kitu, mprani, darasani, utanashati yani kila kitu ambacho Frank aliiga huko utotoni ilikuwa ni kwasababu alimuona Aroni anafanya kiufanisi na aliona jinsi kaka ake alivyopendwa, ila sasa haikuwa hivyo tena, Aroni aligeuka na kuwa teja, mtumia ‘ngada’, dawa za kulevya, Aroni alikuwa teyari ni teja la unga.
Mara Frank akafuta machozi yake na kujikaza, na kuanza kuongea kwa mkazo, “’you need to learn the hard way my brother’, kwanza kabisa usikanyage nyumbani mama hakutaki, usije mtia presha mama yangu, hakutaki kabisa nenda kwa hao wauza unga wezio, maana ndo unawaona wa maana”, alimaliza kuongea Frank na kurejea ndani mwao na akafunga mlango kwa komeo. Ili Aroni asiingie tena ndani kwa usiku huo.
Moja kwa moja aliporejea ndani mwao, akaelekea sebuleni ambapo mamake alikaa akiangalia taarifa ya habari.
“njoo hapa Frank, kaa hapa karibu yangu”, aliongea mama ake, na Aroni akaenda kukaa karibu na mama ake.
Mara mama ake akatoa karatasi mbili za mitihani iliyosahihishwa. Ilikuwa ni mitihani ya Lulu. Mmoja wa hisabati mwengine wa kiingereza. Huo mtihani wa kiingereza alikuwa kapata themanini na ule wa hisabati alikuwa kapata ishirini na tano ya mia.
“Lulu anaanza kunipanda kichwani. Si wa kupata ishirini na tano hisabati mimi nafahamu akili zake, ana uwezo mkubwa kuliko huu kimasomo, analeta ujinga”, aliongea bi Salome, na Frank akabeba hizo karatasi hadi chumbani kwa Lulu na kumkuta akiongea na simu.
“wanaofeli darasani ndio siku zote mabingwa wa kuongea kwenye simu na kuchati”, aliongea Frank na kumshtua Lulu ambae akakata simu aliyokuwa akiongea nayo.
“Kwanini unapata hisabati ishririni na tano, tena hesabu rahisi kama hizi?”
“na kwanini huombi msaadaa kwangu nikusadie kukufundisha kama nilivyokwambia ufanye, matokeo yake ndio haya hesabu za ‘form two’ unazifeli wewe mtu wa ‘form three’, aliwaka Frank.
“sasa mimi naona kwanza hiyo simu yako inakupotezea muda, hebu ilete”, Frank akampokonya mdogo wake simu, na huku mdogo wake akilalamika arudishiwe simu yake. Mara simu hiyo ikaanza kuita.
Frank kuitazama namba inayoita, ilikuwa imeandikwa jina ‘baby darling’.
Lulu kwa kuelewa tu aliyekuwa akipiga ni nani akampokonya kaka yake hiyo simu kisha akakata simu na kuendelea kulalamika, eti kwanini Frank alikuwa anapenda kushika simu za watu.
Frank akaanza kumuwakia, “Hivi unajua wewe uko form three, hujakanyaga ngazi yeyote kielimu”, “halafu badala ya kusoma, unaongea na mpuzi gani sijui huyo kwenye simu, huna maadili kabisa”
Mara simu ikaita tena, safari hii Frank akampokonya Lulu hiyo simu, na kusoma mpigaji, na ilikuwa ni namba ileile iloandikwa jina, ‘baby darling’.
“huyo ni rafiki angu, Sule ananipigia achana na simu yangu”, alilalamika Lulu.
Frank hakuiacha hiyo simu, sasa akaipokea na kuongea kwa vitisho, “Haloo, wewe jamaa ambaye unaitwa Sule, tafadhali sana kaa mbali na Lulu. Kaa mbali, acha mazoea ya kijinga na kipumbavu kabisaa, muache Lulu asome na afanye mazuri kwenye masomo yake. Na hii iwe mwanzo na mwisho kumpigia kwenye simu ama sivyo utachezea moto wa kuukalia mbali, tumeelewana?” “unatazama mieleka, nakuuliza unatazama mieleka, kule kuna staili ya kuvunja mtu kiuno inaitwa RKO, sasa dogo tulizana, utalazwa kwa kuumizwa mifupa, kaa mbali na Lulu, alifoka Frank na kumtisha kabisa huyo kijana aliyeitwa Sule kwa mikwara ya aina yake, kwenye hiyo simu, kisha akakata hiyo simu.
“Kwanza naondoka na hii simu yako, ukae usome, na kwakweli itabidi nimwambie mama yako upuzi wako unaoufanya na hii simu, hutakiwi hata kuwa nayo”, aliongea Frank na kutoka humo chumbani mwa Lulu.pamoja na simu yake asimrudishie tena hiyo simu hadi afaulu mitihani yake.
..................................
Usiku wa siku hiyo Aroni alikuwa hana pengine pa kwenda zaidi ya kwa msichana mmoja aliyeitwa, Tunda. Yeye Aroni na Tunda walikuwa na ukaribu wa ajabu sana, hata ilishangaza watu kwa nini walikuwa karibu hivyo bila ya kuwahi kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Halafu Tunda mwenyewe alikuwa ni ‘girlfriend’ wa Dullah, ambaye alikuwa rafiki wa Aroni, na huyo Dullah pia ilisemekana kuwa ni muuza madawa ya kulevya na huo ulikuwa ndio ukweli.
......................
Siku iliyofuatia Frank alikuwa yupo kantini ya chuoni kwao CBE, pamoja na Recho na Talib, ndipo Recho alipomuambia Frank kuwa usiku wa jana yake alimuona Aroni mitaani kwao na kwamba alimuona kwenye nyumba ya jirani yao aliyeitwa Tunda. Mara moja Frank akaelewa kuwa Aroni alikuwa yupo kwa Tunda, ‘demu’ wa Dullah anayesikika chinichini kuwa ndiye anayeharibu vijana wezie mtaani kwa kuwauzia unga.
“Halafu yule Tunda na huyo bwanake anaitwa Dullah hawana sifa nzuri mtaani”, aliendelea kuongea Recho.
............................
Jioni ya siku hiyo kwenye taarifa ya habari, ilisomwa habari kuwa mkuu wa mkoa katangaza vita dhidi ya utumiaji na uuzaji dawa za kulevya na kwamba utapita msako wa nyumba hadi nyumba na kwamba watatia ndani anayeuza na anayetumia dawa za kulevya.
Taarifa hiyo ilimkumbusha Frank juu ya kaka yake na akachukua simu yake na kuisaka namba ya kaka yake. Namba yenyewe aliisevu jina ‘my brother’ na iliambatana na picha ya Aroni.
Wakati Frank anataka kumpigia simu Aroni, Aroni mwenyewe alikuwa yuko kwa Tunda, sebuleni wakipiga stori na soga za hapa na pale na kutafuna bisi huku wakiangalia muvi moja ya kuchekesha sana hadi ikaisha, basi wakabaki wakikumbushiana ‘scene’za muvi hiyo na kucheka zaidi.
Mara wote wakawa kimya, kwa kukosa cha kuongea zaidi. Ndipo mara Tunda akaanza kuongea, “unajua nafurahi jinsi ambavyo watu wa ‘sober’ wamejitahidi kukusaidia, ijapokuwa bado hujapona kabisa ila hakika endelea kuwaona na kufuata matibabu yao, ukiendelea naamini utaacha uteja. Na nakuomba usiache dawa wanazokupa”, aliongea Tunda na kumtizama Aroni, na Aroni akamgeukia Tunda, na akashangaa jinsi Tunda alivyokuwa akimuangalia.
“Ningekuwa wewe, ningeacha urafiki na watu kama Dullah”, aliendelea Tunda, “ni mtu mbaya sana, anaharibu watu”, aliendelea Tunda.
“Dullah ana hela, ndiye ananilipia kodi na ninaishi pazuri, ila si mtu mzuri hata kidogo, hana utu, anauza unga na yu radhi kufanya lolote kutetea biashara yake hiyo”, aliendelea Tunda na Aroni akiwa anamsikiliza.
“Hivi unajua ni Aroni ndiye alianza kukuchanganyia unga kwenye bangi, hadi ukawa unavuta bangi zenye madawa, hadi matokeo yake ukaingia kwenye uraibu wa kokein’, aliongea Tunda na kumvumbua macho Aroni.
“Si mtu mzuri yeye yu radhi kuharibu mtu ili awe mteja wa bidhaa yake inayo haribu watu akili na kuwaharibia maisha yao”, alimaliza kuongea Tunda, huku Aroni akibaki kaduwaa na kutafakari maneno hayo. Kumbe chanzo cha uraibu wake kilikuwa ni Dullah, ambaye yeye Aroni alimchukulia kama ‘mwana’.
Mara mlango wa nyumba hiyo ukaanza kugongwa, na Tunda akinuka kwenda kuufungua. Na kumbe aliyekuwa akigonga likuwa ni Dullah.
Maneno ya Tunda yalikuwa yamemuingia Aroni vilivyo, hivi kwamba akawa kakaa kwenye kiti katulia akitafakari kuwa mnyama hatari aliyesababisha yeye aingie kwenye janga la madawa alikuwa sasa kaingia humo ndani.Aroni akaona hakukuwa na haja ya kujenga amani yeyote na huyo Dullah.
Aroni akajikuta kamtolea Dullah jicho moja kali la kiuadui, na mara moja Dullah akaelewa kuwa hapakuwa na amani mahala hapo.
Ila sasa, Dullah mwenyewe mahala hapo aliingia akiwa anawaza majanga yake mengine kichwani, alikuwa anatafutwa na polisi katika msako mkali dhidi ya wauza unga. Na Dullah aliamini kuna rafiki ake kamsnichi na kumtaja kwenye vyombo vya sheria kuwa yeye ni muuza unga. Hivyo kwa jicho alilopigwa na Aroni akahisi kitu kibaya sana, alihisi kuwa ni Aroni ndiye aliyem’snichi’ kwa polisi hata akawa katajwa kutafutwa na askari.
“Hapa umekuja kufanya nini. Kwa mwanamke wangu, snichi mkubwa wewe.”, aliingea Dullah kwa hasira. “Mimi sifikirii mtu mwengine yeyote anayeweza kunifanyia usnichi kwa askari ili nikamatwe kwa kuuza madawa, zaidi yako wewe snichi, ni wewe tu munafiki mmoja, Aroni”, maneno hayo yalimtoka Dullah yalimshangaza Aroni, kwasababu hakumsnichi mtu kwa polisi wala mahala popote, kwake zilikuwa shutuma mpya kabisa kuzisikia na wala hakufanya hivyo. Ila nae alikuwa na hasira na Dullah, mtu ambaye sasa alibaini kuwa ndiye chanzo cha yeye kutumia madawa.
Kilichofuata baina yao ilikuwa ni ugomvi mkubwa na kushikana mashati, Aroni akimshutumu Dullah kuwa alimuwekea madawa kwenye sigara, bangi na vinywaji na akamfanya aanze uraibu wa vitu hivyo hatimaye akawa teja wa unga, naye Dullah akaja juu kwa kashfa kibao, hasa akihisi na kumkashifu Aroni kuwa ni snichi aliyemchongea kwenye vyombo vya uslama akamtwe kwa kuuza unga, ugomvi ulikuwa mkubwa hadi Tunda akawaingilia kati na kuwaweka pembeni waache kugombana na kutulia.
Mara simu ya Aroni ikawa inaita na aliyekuwa akipiga alikuwa ni Frank. Aroni alipokea simu hiyo ili aongee na mdogo wake, ila ugomvi na kelele alizokuwa akifanya Dullah zikafanya washindwe kuongea kwenye simu kwa mana Dullah alikuwa anafoka kwa sauti sana na huku akiapia kumfanya Aroni kitu kibaya sana. Aroni akakata simu.
Kwa kelele alizozisikia Frank kwenye simu moja kwa moja akaelewa huko aliko Aroni si salama. Hivyo kwa kuwa hapakuwa mbali na mitaa ya kwao akaamua kutoka usiku huohuo kwenda huko kuona kulikoni.
“Wewe ni zaidi ya mnyama, muuza unga usie na utu. Ni wewe ndiye uliyekuwa ukichangaya madawa kwenye sigara na bangi, na vinywaji, lengo lako likiwa kuongeza idadi ya waraibu wa madawa yako”, Aroni alimwambia Dullah kwa sauti ya juu huku kamvimbia sura.
Mara moja Dullah akaelewa ni Tunda ndiye aliyemuambia Aroni ukweli huo, kitu ambacho kilimtia hasira Dullah na kuanza kuongea na ujinga mwengine aliouwaza kichwani, “kwanza kwanini Tunda unajenga mazoea na huyu mpumbavu mmoja, wewe huyu atakuwa ni bwanako wewe Tunda wewe, una tabia za kimal*ya wewe”, matusi hayo ambayo sasa Dullah alianza kuyatoa kwa Tunda yalimfanya binti huyo nae kupanda hasira, hivyo Aroni na Tunda wote wakawa wamemjia juu Dullah na kumtia hasira zaidi.
Matokeo yake, Dullah kwa hasira akaelekea droo ya kabati dogo lililokuwamo humo ndani sebuleni na kutoa bunduki na kuwanyooshea Tunda na Aroni eti akitaka kuwaua.
Wakati hayo yakiendelea humo ndani Frank alikuwa kashafika kwenye nyumba hiyo na alikuwa kaukaribia mlango wa kuingia ndani ya nyumba hiyo na hivyo akaweza kusikia sauti za Tunda na Aroni na sauti ya Dullah akifoka kuwa atawaua wote wawili, Tunda na Aroni.
Frank alipata hofu sana. Na moja kwa moja akachukua simu yake, na kubofya namba ya kuita askari wa maeneo ya huko Kimara, namba ‘112’, kisha akapiga.
Wakati huo ndani ya nyumba ya Tunda gomvi likaendelea kunoga,
“nawapiga risasi ninyi mbwa wawili mfilie mbali, wewe Aroni ni snichi, na tena itakuwa unatoka na huyu Tunda, mana ukaribu wenu umekuwa ukinipa mashaka, ila siku yako imewadia nitakuulia mbali wewe na huyo Tunda”, aliongea Dullah kwa kejeli na kuunyosha mkono wake vizuri. Huku Tunda na Aroni wakiwa wamejaa wasiwasi na mchanganyiko wa hasira walikuwa wamemtolea macho, wakiwa hawaamini kuwa Dullah alidhamiria kweli alichokuwa akiwatishia kuwafanya na hiyo bunduki yake.
Ila ghafla na kwa haraka sana bila ya yeyote humo ndani kutarajia, Aroni akawa kamrukia Dullah na kumkamata mkono wake uloshika bunduki kwa mikono yake miwili na wakaanza kukurupushana hadi bunduki ikamtoka Dullah mkononi, kisha Aroni akamkamata Dullah na kumtupia ngumi nzito ya uso, hivi kwamba akampasua na kumtoa damu, kabla Dullah hajakaa vizuri, Aroni akmrushia ngumi ya pili na kumfanya tena kutema damu na akaanguka chini na akawa akijitahidi kujiinua kwa kupiga magoti.
Mara Tunda akaikumbuka ile bunduki iliyolala chini na akamshtua Aroni, “okota bunduki yake, ataiokota atuue, iokote”, na hivyo Aroni akaiokota bunduki na kisha akamnyooshea Dullah, tayari akijiweka vizuri amfyatulie risasi, mara mlango wa nyumba ukafunguliwa na wote wakageukia mlango kuona nani anaingia, kumbe alikuwa ni Frank, Frank aliingia humo huku anatetemeka, kwa hofu na uoga. Na huku macho kayatoa kwa Aroni, akiwa kashtuka kuona kile ambacho kaka yake alidhamiria kukifanya, yani ‘kumuulia mbali, Dullah’.
Frank alielewa vyema kuwa kitu ambacho kaka yake kadhamiria kufanya kingeweza kumgharimu sana, pengine kuliko jinsi ambavyo matumizi ya madawa yalivyomuharibia dira ya maisha kwa wakati huo.
Frank akamkazia macho kaka ake, na kuvimbisha uso wake, na kukaza sauti, na kumwambia tena na tena, “usim ‘shoot’, achana nae, Aroni, achana nae ushampiga, kaumia, achana nae, tusepe ‘home’”, Wakati huo kaka ake akiwa kashikilia bunduki mikonomi mwake. Uso kauvimbisha kwa hasira huku kanyoosha mikono iloshika bunduki kumuelekea Dullah aliyekuwa sasa kasimama mbele yao, huku damu zikimvuja mdomoni, na huku kachoka taabani kutokana na kipigo alichopewa na Aroni.
“Ukimpiga risasi utaenda jela, utafungwa, itakugharimu wewe, itamgharimu mama, Lulu na mimi pia, achana nae”, aliongea Frank, huku Aroni akawa anakaza vizuri mikono yake tayari ‘kumshutulia mbali’ Dullah ili aanguke afe hapo hapo ndani mwa Tunda.
“Huyu mpumbavu ndie chanzo cha majanga mengi niliyopitia. Rafiki adui. Rafiki aliyekuwa akinichanganyia, madawa kwenye sigara vinywaji na hatimaye kwenye bangi na kisha nikajitumbukiza kwenye uraibu wa kokeini”, aliongea Aroni kwa uchungu.
Mara Dullah akataka amvamie Aroni na kumpokonya bunduki, hapo Aroni akamsukuma kisha akampa teke moja la kiuno na kumuangushia sakafuni, kisha akanyooshea bunduki hiyo, pembeni tu ya kilipo kichwa cha Dullah na kurusha risasi hapo na kuwashtua kweli Dullah, Frank na Tunda, kwa muda mfupi walidhani Aroni kaua mtu kweli, ila kumbe hakuwa kamuua alimtisha tu, kwa kufyatua risasi sentimeta chache tu toka kichwa cha Dullah kilipokuwa hapo sakafuni.
“Nimepigia simu polisi wako njiani, wanakuja, hivyo achana nae usimuue”, aliongea Frank kumwambia Aroni.
Dullah alishtuka, hakufikiri kuwa usiku huo angeweza kudakwa na polisi, ambao alikuwa anawaepuka asikamatwe nao.
“safi sana, nyang’au wewe leo utaenda lala selo. Na kwa vile ‘ushasnichiwa’ utafungwa tu.”, aliongea Aroni, kumwambia Dullah aliyekuwa .
Na muda si mrefu king’ora cha polisi kilisikika na polisi wakawa wamefika nje ya nyumba hiyo ya Tunda na kuizingira, wakiwa na silaha za kujihami kwa maana Frank aliwaita hapo kwa kuwaambia kuna mharifu mwenye silaha ya moto aliyekuwa akitishia kutoa uhai wa watu”.
Basi polisi wakawazoa Dullah, Tunda, Aroni na Frank hadi kituoni, na Dullah akaswekwa ndani. Na kwa vile alikuwa na kesi ya kutuhumiwa kuuza dawa za kulevya ikawa ngumu kwake kupata dhamana kwa maana hakuna mtu wa karibu yake aliyejitolea kumdhamini kwenye kesi kama hiyo.
Basi miezi kadhaa baadae, Dullah akahukumiwa kwenda jela miaka kadahaa.
...........................
Basi, miaka kadhaa ikapita hadi naye Aroni, akaachana kabisa kabisa na matumizi ya dawa za kulevya huku akifanya kazi ya kuhudumu katika ukumbi mmoja wa sherehe. Lulu mdogo wao wa kike akahitimu chuo kikuu na kuajiriwa kama wakili katika moja ya makampuni ya msaada wa kisheria jijini. Naye Frank akawa kaajiliwa wizarani kwenye mambo ya kuvutia uwekezaji , kitengo chake kilimfanya aende sana nje nchi mara aende China, mara Dubei, mara London.
Mama yao, Salome nae akang’ara tena kama enzi zile baba yao bado yu mzima. Sasa unaambiwa mama yao alirudishwa tena kwenye ligi ya wamama wa mtaani kwao huko Kimara, waliokuwa wakimpotezea uanakamati katika maandalizi ya harusi na ‘send off’ za mtaani sasa wakamkumbuka na kuanza kumualika tena, na yeye akawapotelezea mbali kwa kuwaona wote ni ‘masnichi’, waliomtenga kipindi yuko kwenye gharika na wanaojitia kumjuajua mno kipindi kheri zimerejea tena kwenye maisha yake.
MWISHO......