Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,417
Kwanza naomba nikiri kwamba mimi ni suriama niliyechanganya damu ya Kinyamwezi.
Kule Unyamwezini ni Ujombani kwangu kwani Babu wa Babu yangu mzaa mama ni Manamba wa Kinyamwezi Mkata Mkonge aliyepelekwa kwa nguvu kwenye mashamba ya Mkonge kabla ya kuwa mwanakijiji na baadaye kuwa mkulima hodari na mmiliki wa mashamba huko mkoani Tanga baada ya kukoma kwa ukoloni.
Kuna jambo moja najiuliza na nimekuwa nikijiuliza kwa miaka mingi sana.
Hivi hawa ndugu zangu Wanyamwezi mbona Mkoa wao unachechemea sana kimaendeleo tofauti na Mkoa wa Kilimanjaro?
Kwa nini naufananisha na Mkoa wa Kilimanjaro na si kwingineko?
Naufananaisha kwa sababu ya kushabihiana kwa fursa kuanzia Kilimo cha mazao ya Biashara na Elimu.
Hebu ngoja nifafanue zaidi:
Tabora ni mkoa ambao ulikuwa na shule za sekondari bora kabisa na vyuo mbalimbali vya elimu tangu ukoloni na shule hizo zimetokea kutoa viongozi wengi kitaifa hususan Shule za Tabora Boys na Tabora Girls
Ukija kwenye Kilimo wote tunajua umaarufu wa zao la Tumbaku mkoani Tabora pamoja na mazao mengine ya bishara na yale ya chakula. Ufugaji wa Nyuki ni eneo lingine linaupa mkoa huu umaarufu wa pekee na bado hatujazungumzia misitu na upasuaji wa mbao ambapo Tabora imekuwa ikitumika kama chanzo cha uzalishaji wa samani za ndani na zile za maofisini. Lakini pia Mifugo mkoa huu una mifugo ya kutosha ikiwa kwenye orodha ya mikoa yenye wafugani wengi.
Ukweli ni kwamba mkoa huu hauna kisingizio kwa kuwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na mikoa mingine hususan Kilimanjaro.
Kwa upande wa mkoa wa Kilimanjaro wengi tunajua kwamba mkoa huu unaongoza kwa maendeleo kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mikoa mingine. Nakubali kwamba kielimu mkoa huu umepiga hatua kubwa wenyewe katika kuboresha elimu na kwa upande wa kilimo mkoa huu zao kuu tangu ukoloni lilikuwa ni Kahawa pamoja na mazao mengine ya biashara na yake ya chakula.
Iwapo utailinganisha mikoa hii haitofautiani sana kwa upande wa elimu na rasilimali nyinginezo.
Swali pasua kichwa ni hili la Tabora kuwa nyuma sana Kimaendeleo.
Kwa utafiti wangu mdogo nimegundua kwamba wakati wenyeji wa Kilimanjaro hususan Wachaga wana kawaida ya kurudi makwao kila mwaka ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo mkoani kwao na pia kila mmoja kukimbilia kujenga kwao hata kama awe mbali kiasi gani. Kwa ndugu zangu wa Tabora wao wakishaondoka kwao kwenda kutafuta maisha wanakuwa waloewezi huko walikokwenda. Kwao maisha ni popote, hawakumbuki kurudi makwao. Wakirudi ni kuhuduria misiba.
Siajabu kukuta Mnyamwezi akiwazika wazazi wake ugenini mahali alipolowea, wakati kwa wachaga jambo hilo ni matusi kwao. Kule Uchagani kila mtoto katika familia hususan wa Kiume lazima apewe kiwanja na wazazi wake ndani ya eneo la familia. Kwa hiyo hata aende wapi lazima ahakikishe amejenga nyumbani ambao akifa lazima azikwe kwenye mji wake.
Kama akifa kabla ya kujenga shughuli za msiba na mazishi yatafanyikia kwenye mji wake. Hiyo ndiyo heshima kwa mtoto wa kiume. Hivyo ule utaratibu wa kurudi nyumbani kila mwishoni mwa mwaka unaleta ushindani miongoni mwao pale anapoonekana mtoto wa jirani kajenga nyumba yake au kawajengea wazazi wake nyumba ya kisasa. Na huu ushindani umesababisha hata kule Moshi vijijini kuna nyumba za ghorofa na nyingine zikiwa na swimming pool. Nadhani kwa Tabora vijijini yatakuwa ni maajabu ya Dunia.
Hebu tujiulize hawa wenzetu ni nani kawaroga?
Maana kama ni wasomi wako wengi tena wa kiasi cha kutosha na kama ni kupata nafasi serikalini walishika nafasi kubwa kubwa tangu ukoloni hadi sasa. Je sababu ni nini?