Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,809
- 15,443
Je kuna mtu yeyote katika familia yako au ukoo wako ambaye ni kero kwako? Unadhani huyo jamaa yako anayekukera anasababisha kushusha ari yako ya utendaji wako kazini kwa kuwa unapokuwa unafanya kazi anakujia mawazoni mara kwa mara?
Kumbuka tu kwamba, unaweza kutembea na mkeo au mumeo kichwani mwako kutwa nzima. Unaweza kutembea na kero za shemeji yako wifi yako, dada yako au kaka yako, mama yako au baba yako kwa mwaka mzima, kila siku kero. Kero zake zinazunguka kichwani mwako kama vile ndizo pekee zilizoko hapa duniani na hakuna kingine cha kuwaza.
Kama hiyo ndiyo hali uliyomo, huko peke yako. Hata Leonard Felder, mtunzi wa kitabu cha When Difficult Relatives Happen to Good People. Anajua vizuri sana kuhusu kero hizi za ndugu na jamaa zetu wa karibu. Felder katika utafiti wake aliwauliza wanaume kwa wanawake 1,358 kuhusu hali katika familia zao na akakuta zaidi ya asilimia 70 kati yao wanao jamaa ambao wanawachanganya akili kwa kuchochea ugomvi katika familia zao.
Hii ina maana kwamba, hata sisi huenda kati ya kila watu kumi, ambao ni jamaa zetu, kuna saba wanaotuchanganya akili. Dr. Felder anatahadharisha kuhusu mambo matano kuwa ni dalili kwamba, matatizo ya nyumbani yameanza kukuathiri kisaikolojia na kimwili.
Je katika familia yako kuna mtu yeyote ambaye ana tabia ya kukupinga au anayekupa ushauri mkali mkali wa kukudhalilisha au anayekupa ushauri mkali wa kukudhalilisha na afanyapo hivyo anakukumbusha hali yako mbaya ya kifedha au ubaya wa umbo na muonekano wako?
Kuna wakati unajiona umechoka kimwili au kuwa katika hali mbaya kutokana na mazungumzo machafu yaliyopita au tatizo ambalo bado halijatatuliwa kati yako na mwanafamilia mwenzio? Unakumbana na hali hiyo baada ya mazungumzo ya simu au baada ya kutembelewa na mmoja wa ndugu zako wakorofi, na ili kupunguza mawazo unajiingiza katika ‘kulakula' , unywaji wa pombe, utumiaji wa dawa za kulevya au mambo mengine yafananayo na hayo?
Je kuna wakati unajikuta huna fedha au huna furaha kwa sababu unajaribu kumsaidia mwanafamilia ambaye haoneshi shukurani zozote kwa msaada unaompa? Inaweza kuwa msaada wa mawazo, fedha, au ukarimu wowote wenye lengo la kumfanya ajihisi vizuri. Je, kisirisiri ungependa familia yako ingekuwa isiwe na migogoro kama ilivyo sasa, au ingekuwa ni familia ambayo mnasaidiana wenyewe kwa wenyewe?
Endapo dalili kama hizi unazo, kuna namna mbili ya kukabiliana nazo. Ya kwanza na ya kawaida ni kukataa. Kwa mujibu wa Dr. Felder, watu walio wengi wanajaribu kudharau kwamba kuna mambo yanachanganya akili katika familia zao. Kwa upande mwingine kuna njia bora ya kukabiliana na hali hii. Kutumia mbinu zilizothibitishwa kwa kuboresha uhusiano wa familia.
Kuliko kuyaacha matatizo ya kifamilia yaendelee na kukuathiri kisaikolojia, kuna hatua ambazo unaweza kuzichukua ikiwa ni pamoja na:
1. Kujenga uhusiano bora zaidi na wanafamilia ambao unadhani ukiwa nao unakuwa na amani.
2. Unaweza kumuomba mmoja wa wanafamilia ambaye anaheshimika sana kuzungumza kwa niaba yako siku ambayo unakuwa na mzozo wa kifamilia na mmoja wa watu wakorofi sana katika familia yenu
3. Badala ya kumruhusu mtu kukuchukulia kama Busati la kukanyagia mlangoni, simama imara lakini kwa ukomavu. usimjibu kwa hasira anapokuudhi, njia ya kiutu uzima na yenye nguvu ni kujiwekea mipaka. Unaweza kuwa na huruma, lakini ukawa imara.
4. Kama jamaa yako ni mkorofi sana usijiwekee matarajio makubwa sana kwamba, atakubali kukaa kiti kimoja kirahisi. Badala yake Felder anapendekeza kujiwekea matarajio madogo.
5. Kuna watu wengi wakorofi, ambao hawataki kukubali ukweli wa udhaifu wao. Mara nyingi ni watu wasiojiamini na ambao wamejaa hofu na mashaka na chuki za maudhi ya huko nyuma kutoka kwa watu waliowaamini sana, wawe wazazi au wapenzi. Kama una mume, mke au ndugu wa aina hii ni vigumu sana kumsaidia ili abaini kasoro zake. Kwani kwa kadiri unavyojitahidi, ndivyo unavyoharibu, kwani unawatisha zaidi na kuwafanya waamini kwamba, wewe una matatizo. Lakini wanachoshindwa kukiona ni ukweli kwamba, wenyewe huwa wanakorofishana na kila mtu wanayekuwa naye karibu. Hapa usikubali kuumizwa bure!
6. Kumbuka jambo moja muhimu sana kwamba huwezi kumbaadili mtu hapa duniani, kama yupo mtu unayeweza kumbadili, basi ni wewe mwenyewe. Kwa hiyo ndugu na jamaa wakorofi, wapenzi na wapendwa wakorofi, huwezi kuwabadili labda wenyewe watake kubadilika. Hii ina maana kwamba, inatakiwa wewe kubadilika. Kubadilika kuliko bora ni kuwaacha hao wakorofi waishi kwenye dunia yao wenyewe waitakayo bila kukuhusisha.