Ndoto inayotesa kichwa changu

cyrax

Senior Member
Mar 12, 2017
105
88
HII NDOTO INANIUMIZA KICHWA.

Nililala nikaota, sikumbukagi ndoto ninazoota lakini hii ya leo ninaikumbuka vizuri na inanikosesha raha; NATAKA KUWA MUASI WA MASUMBWI naweza kuita ndoto yangu hivyo maana ndivyo nilivyoota.

Nimeota nilikuwa kwenye uwanja wa masumbwi nikiwa mpenzi na shabiki wa mchezo huu na nitakuwa bondia siku moja. Tofauti ya mchezo huu wa masumbwi na masumbwi nyingine ni kupigana kwa timu kila bondia ana timu yake na marefa wana timu yao pia ingawa anayewalipa ndiye wanayemshabikia; balaa gani hili? tulikuwa wengi kila mapambano yalikuwa mengi, kila pambano na taji lake ingawa macho na ya mashabiki wengi ilikuwa katika pambano moja kubwa kuliko yote. Ukubwa wa pambano hili ulitokana na ukubwa wa mabondia wao na timu wanazochezea kuwa na upinzani wa jadi.

Mmoja wa mabondia hao alijivika umaarufu wa kushinda mapambano mengi makubwa kuliko wenzake waliomtangulia lakini kubwa zaidi ni pambano alilopigana miaka kadhaa nyuma ambalo wanasema alishinda raundi za mwanzoni kwa ponti za marefa ingawa mimi sikuwepo kwenye pambano rafiki zangu waliohudhuria wanasema refa alimsaidia kwa kugonga kengele haraka huku mpinzani wake akiwa na nguvu za kupigana, wanasema raundi za pambano zilipunguzwa na kuwa 6 badala ya 12 pia inasemekana refa alitoka kwenye timu ya walioshinda.

Jambo lingine lilofanya pambano lile kuwa kubwa zaidi ni majingambo ya timu iliyoshinda pambano lilotangulia kuwa katika mapambano ya mazoezi na kirafiki washindani wao walikimbia uwanja kwa kuwaogopa hivyo walijitwalia utawala wa mchezo wa ngumi kwa kipindi chote na waliamini watashinda katika pambano hili pia.

Katika ndoto yangu mchezo wa mwisho ulionekana kiwa na hamasa na shauku kubwa zaidi kwa sababu timu iliyoshindwa pambano la miaka kadhaa iliyopita na mapambano mengine ya urafiki na mazoezi walijiapiza kushinda raundi za mapema zaidi kwani walisema kuwa marefa waliwahujumu katika mashindano yaliyotangulia. Hiyo haikutosha pambano hili walibadilisha bondia wa shindano la mwisho ambaye hakuwahi kishindwa katika mapambano madogo na ya kati aliyopigana.

Alishinda mapambano ya mazoezi, alishinda riadha, alishinda kuogelea alishinda hata mitihani ya darasani pia, kubwa zaidi inasemekana akiwa katika mazoezi yake alipigwa kwa vyuma sio ngumi kama ilivyozoeleka, akafa, akazikwa na mashairi na hotuba kuwa marehemu ameoza ananuka zikaandikwa watu walilia, mimi nililia pia lakini tofauti kidogo na wenzangu sikulia na mtu mwingine zaidi ya chupa ya pombe yangu yenye pilipili na uchungu kama gongo, machozi yalipotoka niliyakusanya nikayanywa tena kilikuwa kiapo changu kuwa sitalia tena machozi yaliyobaki nilichanganya kwenye pombe yangu kali nikaiweka kwenye jokofu “hii watainywa siitaki tena” nilisema.

Marehemu aliyezikwa siku nyingi alifufuka siku chache tukiwa kwenye maandalizi ya mapambano makubwa ya ridhaa ingawa inasemekana wanalipwa na mabondia na timu zao wanajilipa wenyewe, aah! Wewee nani kasema, alikwambia nani? Nilisema kwenye timu ya pili inayotaka ubingwa kwa mara ya kwanza mimi kazi yangu ni kubandika matangazo watu waende ulingoni kushangilia na kutaja majina ya mabondia wa timu yangu kwa watu wasiowajua na kisema sifa zao ingawa kocha hanijui na timu yangu hainilipi. Naipenda na niliapa kuishangilia na kuipigania kwa kiapo cha kifo changu, nitakufa nikiipenda timu yangu labda nitakufa siku nikiichukia.

Bwana! Marehemu alifufuka akawa hai inasemekana alipofungua mdomo tu alisema “nitapigana pambano kuu nitapigana” Loh! “Marehemu nani kakwambia hayo? Ni kweli lakini nafasi ya mpiganaji wa pambano kuu tumempa mwingine” kocha alisema na marehemu aliyefufuka akasema tena nitapigana! Na nitashinda.

Haa! Watu walishangaa, walikuvunja, wakakuua, tulilia tukakuzika na hata sasa tunalia wewe ndo unafufuka uatapigana vipi? Marehemu akasema nitapigana na nitashinda nipeni pambano na mliyemchagua. Kocha alikubali marehemu akapigana na bingwa wetu na akashinda tukamwita shujaa wa ushindi wetu. utakuwa mwendawazimu ukikataa marehemu asipigane pambano kuu la mwisho.

Marehemu akatoka nje tukaenda kumuangalia pia nilienda ingawa tofauti na wengine waliobeba vitambaa ya kufuta machozi yao ya furaha mimi nilibeba chupa yangu ya pombe kali iliyochanganyika na machozi niliyomlilia marehemu alipokufa, nililia tena kisha nikaweka machozi yangu kwenye chupa yangu ya pombe, “watainywa sitainywa tena” nilisema. Watu walikuwa wengi, vitambaa vilililoa machozi na barabara zilijaa mate ya kushangilia baada ya kulia kwa furaha.

Ajabu timu ya pili walipinga marehemu asitoke nje siku ile kwani wao walikuwa wanampongeza marehemu wao aliyekufa ambaye alishinda mapigano yaliyopita kwa damu na machozi. “marehemu wenu asitoke leo maana sisi tunampongeza wa kwetu na kama mtamtoa huyo leo kwetu msije hatuwataki” walisema kwa hasira looh! Marehemu aliyefufuka alitoka nje na marehemu aliyekufa alipongezwa, akaagwa, akazikwa na akaoza kisha akatoa harufu ingawa alizikwa na harufu hiyo ilitukera wote.

Mganga akasema hiyo harufu ni machozi na jasho la mabondia aliopigana nao kwa kisu badala ya ngumi, damu waliifuta kwenye sakafu na nguo zake wakachoma moto ingawa walishau maji ya damu wakayamwaga chini badala ya kuyanywa yakachanganyika na lile jasho na machozi, damu ikawa ndani ya jasho na machozi na ndio inayonuka.

Manabii wakainuka kanisani wakasema siyo harufu ile ni manukato, alikuwa mtu mwema na Mungu amempokea wakatoa unabii mpya kuwa Mungu amemteua bondia wa timu shindani ambaye ni bingwa mtetezi kuwa mrithi mahala pake wakatoa laana kwa jina la Mungu wao kuwa atakayesimama kupigana na bingwa mtetezi awe kama marehemu aliyekufa tofauti iwe harufu yake mungu asiipokee na inuke zaidi. Hawakuishia hapo wakafanya mazoezi kupigana mapambano madogo ya utangulizi loh!

Kituko kikainuka baada ya kumpokea marehemu aliyefufuka timu pinzani wakasema marehemu hafai kupigana sio mwanadamu ni mzimu utatafuna mabondia wote na kunywa nyama na damu za watoto wa mashabiki wote uwanjani ebo! Wakasema marehemu gloves anazotumia kupigana hazijatengenezwa na timu yetu zinatoka nje, zina vyuma na laana ya damu na harufu ya maiti ya ufu wake. Haa! Sawa tuko tayari atutafune atumalize sisi na watoto wetu kama akishinda tunachotaka ashinde, tushinde na tushangilie ushindi.

Vita ya pambano na homa yake ikaanza refa akasema mabondia wanaotaka kupigana waandike majina yao na timu wanazotaka yeye na wenzake wataitisha mapambano yaanze. Ajabu ni kuwa baada ya mabondia wetu kuandika majina refa akakataa kuyapokea wenzake ambao ni wafanya usafi na walinzi wa ulingo wakaambiwa waangalie mabondia wa timu yetu wasilete fujo.

Tukarudi nyumbani baada ya kuandika majina na mengine yakakataliwa mimi sikulala wakati mabondia wakijiandaa na pambano nilienda kwenye jokofu langu nililolificha mchangani nikatoa chupa yangu ya pombe kali na macho lakini awamu hii ilikuwa chungu zaidi nililia kisha nikacheka na baadae nikalia tena machozi nikayaweka kwenye chupa yangu ya pombe, jasho llilotokana na kucheka nililiweka kwenye chupa pia. Watainywa! Nilisema tena.

Wakati nikiwa nimeshika chupa yangu ya pombe alikuja kichaa mwenye akili akanimbaia “pombe kali haiwekwi kwenye jokofu atakayeinywa atachelewa kulewa na muda itakapopanda kichwani atazima au atakufa kabisa” shhh! Nyamaza wewe nina jambo langu naelewa ninachofanya sitainywa mimi na atakayeinywa sitaki alewe mapema nataka anywe chupa yote iishe kisha alewe upendo wa ushindi atakaopata kwenye pambano la mwisho nilimwambia.

Siku ya kuitisha majina ikafika refa akaanza vibweka kama mke wa mitara ratiba ikawekwa wazi mabondia wakafika kila mtu na timu yake. Mistari ya foleni ikapangwa muda ukawekwa waandishi wakaja walinzi na wapiga deki wa ulingo wakafika pia, ala! Nilishangaa kwa mstuko hawa walinzi sio siku ya pambano wamefuata nini hapa na hawa wapiga deki ni nini wanafanya na sio siku ya pambano? Ni ajabu kweli.

Wakati mabondia wakiwa kwenye pambano maajabu yakaanza “waandishi mnaruhusiwa kupiga picha na kutangaza matukio ya bingwa mtetezi tu! Na nyie wapiga deki hamruhusiwi kusafisha timu yoyote zaidi ya bingwa mtetezi mlinzi mkuu alisema. Kamera zilivunjwa vinasa sauti vilitupwa chini ghafla msururu mkubwa wa magari ya walinzi ukatokea mbio sio za mchezo kuna mabondia wamejisajili kucheza pambano na wametoka nje hili sio pambano la kimataifa tunawatafuta kwa kukiuka kanuni. Amaa! Ajabu kweli mbona mapigano yaliyopita walipigana au wamezaliwa upya? Nilijiuliza.

Vibweka hivi tukiwa tunasubiri zamu ya bondia wetu ifike tangazo likasikika “kikosi cha walinzi kinapambana na wizi wa kutumia silaha wapiganaji wenu ni washukiwa wa kuaminika tunawahitaji kwa mahojiano” ebo! Magaidi wote wanatoka katika timu yetu ajabu hii. Waliiba lini tuliuliza kwa mshangao? Mwaka uliopita taarifa tumeiona leo kwenye mafaili yetu. Ama! Taarifa ya wizi mmeletewa leo hamkuijua kabla au mnaifanyia kazi leo? Tuliuliza kwa mshangao, Tunaifanyia kazi leo kwa weledi na umakini mkubwa.

Haukupita muda mrefu mojawapo ya mabondia aliyekuwa anaandika jina lake akapigiwa simu kuna mabondia watekwa hawatakuja kukamilisha usajili wa pambano. Shida hii taarifa ikatolewa na walinzi na wapiga deki “hawajatekwa wamekimbia pambano maana tutawapiga raundi ya kwanza” haa!

Walinzi mna timu pia mnalinda uwanja au m bingwa mtetezi na timu yake? Ajabu baadhi ya mabondia wa timu yetu hawakuonekana tena taarifa zinasema kuwa waliondoka , walichukuliwa hawajarudi hawajui walipo ila watarejea waliorejea wamepigwa kabla ya kupigana labda walipigana wakapigwa sijui.

Vibweka vya marefa vilinichosha nikaifuata chupa yangu ya pombe kwenye jokofu “nikajiapiza kuwa watainywa nitakuwa muasi na kuwanywesha hii pombe.

Niliamka usingizini kwa mstuko mkubwa sana nasogelea jokofu langu ninywe maji nipoze roho ebo! Sio hivyo tena chupa yangu ya pombe kali iliyochanganyika na machozi na jasho naikuta imejaa tele maji ya ubaridi yanatiririka, haijawa barafu ila imepoa tayari kwa kunywa. Maneno niliyojiapiza kwenye ndoto yangu yanajirudia baada kuona ile chupa NITAKUWA MUASI.

Nafungua mitandao ya kijamii kwenye simu yangu nakutana na taarifa zenye uhalisia wa ndoto niliyoota! Nimekuwa nabii? Au mganga? Inawezekana ndio sababu nimekumbuka vizuri ndoto niliyoota pambano limekaribia vibweka vya marefa, walinzi na wapiga deki wa timu ya bingwa mtetezi ni zaidi ya nilivyoviona kwenye ndoto.

Chupa yangu imejaa watainywa sitainywa mimi! Awamu hii sitakuwa mshangiliaji au mpambe nitakuwa mpiganaji ingawa sitapigana na bondia yetote wa timu pinzani nitapigana na refa na walinzi wake na nitamshinda.
 
Back
Top Bottom