Mwanamke aolewa na wanaume wawili
2004-06-17 16:28:04
Na Mwandishi wetu
Mume wa pili kashtukia dili, alipofuatilia akakuta mume mwenza kajaa tele kama pishi la ubwabwaZawadi Kapambwe, Kibaha.
Ukisikia anja ya nyani kula hindi bichi, basi ni kama hii alivyocheza mwanamama huyu ambaye aliweza kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja na akawa anawafanyia zamu za kulala bila kugundulika.
Hata hivyo kama Waswahili wanavyosema kuwa njia ya mwongo ni fupi na siku za mwizi ni arobaini, basi mume wa pili wa mwanamke huyo ameshtukia dili hiyo hatari na kukimbilia kortini kutaka atenganishwe na mwanamke huyo laghai.
Sekeseke lenyewe liko hivi:
Miaka kadhaa iliyopita mwanamama Lucy Alfred
aliolewa kwa ndoa ya kanisani na mume anayefahamika kwa jina la Osmund Chiwalo aishiye huko Morogoro na kubahatikana kupata watoto wawili.
Baada ya ndoa waliishi kwa raha mstarehe na mumewe huku wakipanga hili na lile kuboresha maisha yao.
Lakini mara shetani mbaya alimwingia mwanamama huyo kichwani na akaamua kuukimbia mji kasoro bahari na kujitoma Bongo, kwenye Jiji lililojaa raha na karaha.
Baada ya kutinga Bongo, mwanamama huyo akanasa kwa Mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania ajulikanaye kama A.K.Kamuhabwa.
Penzi likawa penzi na wawili hao wakakubaliana kufunga ngoa takatifu ili waishi maisha ya utimilifu ya mume na mke.
Baba wa watu bila kujua hili wala lile akaanza maisha ya ndoa na mwanamama huyo laghai ambaye alimwapia mzee kutowahi kuolewa wala kuwa na mtoto.
Sasa dili limebumbuluka na sakati kutinga kizimbani.
Mwanajeshi huyo ndiye amemburuza kizimbani mkewe akitaka talaka yake ili kila mmoja aanze kivyake vyake.
Kesi hiyo ya aina yake imefunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo Mkuza, Kibaha.
Mbele ya hakimu Andrea Sekimanga Mwanajeshi huyo amedai kuwa mwanamke huyo kabla ya kufunga naye ndoa alimwambia kuwa hana mume na wala hajawahi kuolewa.
Afande huyo akaendelea kusema kuwa lakini baada ya kuanza maisha yao ya ndoa, alishangaa mkewe safari za Morogoro haziishi.
Akasema alipomuuliza kulikoni kwenda Moro kila kukicha, mwanamama huyo akamfunga kamba kuwa huko kuna watoto wa marehemu dada yake ambao ameachiwa awatunze.
Hata hivyo Afande huyo akasema machale yalimcheza na kuanza kufuatilia ili kujua siri iliyojificha.
Akasema katika kufuatilia ndipo alipobaini mkewe kuwa na mwanamume mwingine tena waliyefunga naye ndoa na kuwepo kwa watoto wawili.
Mwanajeshi huyo akasema katika uchunguzi wake, alikwenda mpaka katika kanisa walilofungia ndoa ambapo alithibitishiwa na Padri aliyewafungisha ndoa kuwa mwanamama huyo ana ndoa halali.
Baada ya kupata uhakika kuwa mke niliyemuoa ni mke wa mtu, nikamueleza na kumpa talaka ili arudi kwa mume wake lakini aligoma huku akieleza kuwa hawezi kurudi kwa mumewe wa kwanza kwa madai kuwa jogoo wake mgumu kuwika, akasema afande huyo.
Akaendelea kuieleza mahakama kuwa baada ya kuona mkewe amegoma kurudi kwa mumewe, aliamua kumfungulia kesi mahakamani kwa kuhofia usalama wake baina yake na mume mwenza.
Baada ya afande huyo kumalizika kutoa maelezo yake na mwanamke huyo kupata nafasi ya kutoa maelezo yake, hakimu Sekimanga ametoa uamuzi wa shauri hilo.
Katika uamuzi huo amemtaka mwanamama huyo kurudi haraka kwa mumewe wa kwanza.
Hata hivyo mwanamama huyo aligoma kabisa akidai kuwa bwana huyo jogoo wake hawiki. Hoja hiyo hata hivyo iligonga mwamba.
Hakimu pia amempa ruksa mwanajeshi huyo kuoa mke mwingine wakati wowote atakapotaka.
SOURCE: Alasiri