Ndoa ya Marekani na nchi za Ulaya mashakani

Mr Hero

JF-Expert Member
Jun 11, 2015
5,540
7,455
Marekani yadaiwa kuishinikiza EU makubaliano TTIP
Vyombo vya habari vya Ujerumani vimefichua kuwa Marekani imeushinikiza Umoja wa Ulaya kuafiki makubaliano ya biashara ya TTIP, kwa kutishia kuzuwia mauzo ya magari yake iwapo hautofungua soko lake za bidhaa za kilimo.


Shirika la utetezi wa mazingira la Greenpeace lilitoa nyaraka hizo kwa gazeti la Süddeutsche pamoja na vituo vya utangazaji vya Ujerumani WDR na NDR, kabla ya kuzichapisha kwa wingi muda mfupi uliopita.

Greenpeace inasema nyaraka hizo zinawakilisha theluthi mbili ya maandishi ya muswada wa makubaliano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya - maarufu kama TTIP, kutokana na duru ya karibuni ya mazungumzo yaliyofanyika mwezi Aprili, na zinahusu masuala kadhaa kuanzia mawasiliano ya simu hadi kwenye chakula na kilimo pamoja na vikwazo vya kibiashara.

"Tunazichapisha nyaraka hizo kwa sababu mchakato mzima wa mazungumzo ya TTIP hauna uwazi katika namna inayoshtua kweli. Haitajadili siri zozote za kibiashara, lakini kuhusu ulinzi wa mazingira na walaji, na pia haki za ajira za zaidi ya watu nusu bilioni barani Ulaya," alisema Stefan Krug kutoka Greenpeace.


Baadhi ya nyaraka za makubaliano ya TTIP zilizochapishwa na Greenpeace.

Vitisho vya kukwamisha biashara ya magari

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Marekani imetishia kuzuwia juhudi za kurahishisha uuzaji wa magari ya Ulaya nchini Marekani iwapo Umoja wa Ulaya hautokubali kuruhusu mauzo ya bidhaa zaidi za kilimo kutoka Marekani, liliandika gazeti la Süddeutsche na vituo vya televisheni vya WDR na NDR.

Hatua hiyo itakwamisha juhudi za Umoja wa Ulaya za kuwalinda walaji dhidi ya vyakula vilivyokuzwa kwa njia za kijenetiki na nyama inayotengenezwa kwa kutumia homoni. Mtaalamu wa sheria ya kimataifa Markus Krajewski kutoka chuo kikuu cha Erlangen - Nuremberg anazungumzia tatizo la makubaliano hayo.

"Tatizo kubwa kwa maoni yangu, ni kwamba TTIP yanaweza kuwa makubaliano, yanayoingilia pakubwa uhuru wa udhibiti wa ndani, ambayo pia yanabinya kwa sehemu mchakato wa kidemokrasia wa utungaji sheria au yumkini kuufanya usiwezekane."

Matumaini ya kufikia muafaka

Wajumbe wa majadiliano kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya walisema siku ya Ijumaa baada ya mazungumzo mjini New York kuwa bado wana matumaini ya kuyakamilisha mazungumzo ya TTIP mwaka huu licha ya upinzani mkali, uchaguzi nchini Marekani na kura nchini Uingereza kuhusu hatma ya nchi hiyo ndani ya Umoja wa Ulaya.


Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na rais wa Marekani Barack Obama (kulia) wanapigana ila makubaliano ya TTIP yanasainiwe kabla Obama hajatoka madarakani.

Makubaliano ya TTIP yamekumbana na upinzani mkali kutoka kwa umma barani Ulaya na pia nchini Marekani, ambako matamshi ya kupinga biashara huru yamepata umaarufu miongoni mwa wagombea kutoka vyama vyote vikubwa kuelekea uchaguzi mkuu Novemba mwaka huu.

Rais Barack Obama ameifanya biashara kuwa suala muhimu kwenye ajenda yake katika miezi hii iliyosalia kwenye uongozi wake na alishinikiza makubaliano yafikiwe wakati wa ziara yake nchini Ujerumani wiki iliyopita, wakati akihudhuria maonyesho ya kimataifa ya kiviwanda mjini Hanover pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afpe,ebutv


Source DW
 
Back
Top Bottom