Ipo hivi;
Mnapooana, mali mnazopata kwa kushirikiana hizi zinaitwa
mali za familia/ndoa (matrimonial properties), hizi ni mali zinazomilikiwa na wanandoa kwa kuwa walishirikiana katika upatikanaji ama uchumaji wa hizo mali, humilikiwa kwa uwiano, labda asilimia 50 kwa 50 au 10 kwa 90 nk, yaani humilikiwa kutokana na kiwango cha uchangiaji wa mali hiyo kwa kila mwanandoa. Inapotokea mgogoro uhusuo mali hizi, kila mwanandoa hupaswa kuonesha ni namna gani na kwa kiasi kipi alishiriki uchumaji/upatikanaji wa mali hizo.
Hizi matrimonial properties hazihusiki chochote na watoto,
ni mali za wanandoa tu, watoto si wanandoa. Mwanandoa mmoja anapokufa, mali hii hubaki kuwa ya wanandoa (yaani ya marehemu na mwenza wake aliyebaki) kwa uwiano uleule waliomiliki mali. Kama marehemu alikuwa na wosia, basi mgawo wa mali alitakiwa kugawa mali hiyo kwa sehemu tu ya alichokuwa anamiliki katika mali hiyo, mfano kama nyumba ilimilikiwa nae kwa asilimia 50, basi wosia wake utagawa mali yote aliyomiliki (asilimia 50) kwa warithi wake, ambapo mke na watoto na wazazi wa marehemu au hata watu wengine watakuwa ndio wanufaika. Mfano nyumba ina vyumba 4, uwiano wa umiliki ni 50% kwa 50% basi mali ya marehemu hapa ni vyumba 2, hivi tu ndiyo vinapaswa kujadiliwa katika mirathi, viwili vingine ni mali ya mwanandoa aliyebak. Izingatiwe kuwa huyu mke aliyebaki naye atastahili kupata sehemu ya hivyo vyumba 2 vya marehemu ukiachana na vile vyumba vyake viwili vya nyumba hiyo.
Marehemu kama hakuacha wosia juu ya mgawo wa mali yake basi ndipo mtu huomba mahakama imteue kuwa msimamizi wa mirathi ya mali za marehemu, napo ni kwa asilimia 50 tu ya mfano. Kutokana na familia zetu kutopenda kuwa na wanasheria wa familia au hata wa kutoa huduma wakati wa tukio tu, basi familia hizi pindi anapokufa baba huamua kujadili mali za familia kama mali
za marehemu pekee kwa ukamilifu, mfano nyumba nzima huonekana kama ni ya mrehemu pekee. Matokeo yake mjane hujikuta anaporwa mali anayomiliki au hupewa sehemu anayomiliki tayari, yaani unamiliki gari halafu mtu anasema wewe tunakupa gari hili kama mirathi yako. Hili ni kosa japo sio la kisheria lakini hufanya mgawanyo mzima kuwa batili.
NINI KIFANYIKE?
- Familia zijizoeshe kuwa na wanasheria wa familia, wataokuwa wanawashauri mambo ya kisheria wakati wote. Mnaweza hata kukubaliana nae mkawa mnalipa fedha ndogo tu, mfano shilingi elfu 50 kwa mwezi (kwa kuzingatia uchumi wetu wa kati) kwa mambo yasiyokuwa kesi mahakamani, hii itawasaidia sana kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na wanafamilia kupata uelewa wa mambo kama haya.
- Wanandoa wanapochuma mali pamoja waziandike katika wosia wa pamoja (mutual /joint will) , wosia ambao automaticaly humpa umiliki wa mali za familia mwanandoa hai aliyebaki pale mwenza wake anapofariki dunia na zaidi wosia huu humfanya mwanandoa aliyebaki kushindwa kubadilisha chochote katika wosia huo, hivyo hbaki kama walivyokubaliana na marehemu.
- Serikali kama itabadilisha mtaala wa elimu, basi izingatie kuweka iweke hata kwa ngazi ya uelewa wa msingi (basics) elimu ya mambo haya ya ndoa na mirathi maana ndiyo tunayokutana nayo kila siku katika maisha yetu.
Sajo