Ndege asiyewindwa akinasa aliwe?

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,476
39,995
Wa kijiji nimetinga, na swali nawapangia,
Magwiji toka Iringa, wa Tanga naulizia,
Na wa pwani mnotunga, fanya hima kujibia,
Ndege asiyewindwa, akinasa aliwe?

Ametoka bwana Kombo, keenda zake kuwinda,
Mtego kaweka chambo, ni kwale anawawinda,
Kashinda huko kitambo, huku roho yamdunda,
Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?

Mtego ukafyatuka, sauti ikasikika,
Ndipo Kombo akaruka, na kisu akakishika,
Mtegoni akazuka, kuona kilonasika,
Ndege asiyewindwa, akinaswwa aliwe?

Kunasa kanasa Kanga, kwale amenusurika,
Kwale kaula mpunga, kisha akapeperuka,
Makosa kafanya kanga, mtegoni kashikika,
Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?

Ndipo Kombo kaudhika, aliyemtaka karuka,
Jambo Kanga analika, ngoma iko kupikika,
Kwale alitamanika, mtegoni kaponeka,
Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?

Ndiposaa nauliza, Kisu kimlambe kanga?
Nini kitamtuliza, mtani kutoka Tanga,
Kombo anajiuliza, amuachilie Kanga?
Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?

Kaditamati natama, natama nikatuwama,
Nilichotaka kusema, kukisema nimesema,
Kompyuta ninazima, kwenye fikara nazama,
Ndege asiyewindwa, akinaswa aliwe?

Na. M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)
Buzuruga Chini.
 
Wakijiji wajua mengi kama wa ujiji,
Washio kitunda sio wote wala matunda,
Kama adhuru au hamna udhuru,
Akikamatwa aliwe.
 
Mzee mwanakijiji, njaa ina tabu yake,
Imewashinda magwiji, na yao tele makeke,
Sembuse ndo mwindaji, mwenye njaa na upweke?
Yataka kuhangaika,ili kumponya kanga

Kombo kapata kiwewe, kumkosa huyo kwale,
Hali yake ielewe, aibu usoni tele,
Usisubiri ambiwe, umesikia kelele,
Yataka kuhangaika, ili kumponya kanga.

Kombo amejisahau, lawama anazimwaga,
Kwa mithali na nahau, huku anajikanyaga,
Funzo analidharau, abeba asichotega,
Yataka kuhangaika, ili kumponya kanga

Mtego hauchagui, yeyote inakamata,
Ndege hilo hatambui, awe mbuni au bata,
Wenyewe hauchambui, ajaye unamkata,
Yataka kuhangaika, ili kumponya kanga.

Kombo hili atambue, kwale anavojitapa,
Ili ajikakamue, asithubutu kuapa,
Aibu hii ajue, na namna ya kukwepa,
Yataka kuhangaika, ili kumponya kanga


Twavuna tuliyopanda, kwenye maisha jamani,
Ndivyo walivyotufunda, wahenga toka zamani,
Yale tunayoyapenda, tuyape yake thamani,
Yataka kuhangaika, ili kumponya kanga

 
Back
Top Bottom