Nawaombeni msaada na Mola atawalipa | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Nawaombeni msaada na Mola atawalipa

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by abdulahsaf, Aug 24, 2012.

 1. a

  abdulahsaf JF-Expert Member

  #1
  Aug 24, 2012
  Joined: Aug 31, 2010
  Messages: 859
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 0
  [​IMG]
  Asalamu Alaykum.
  Naomba nilete hii makala muisome muone jinsi maradhi yanavyowatesa viumbe wa Mungu, Mwenyeenzi Mungu Mkubwa mtoto anateseka anasikitisha na kuhuzunisha na huwezi kutupa jicho mara mbili kumtazama na umasikini umemsogeza hadi hapa alipofikia Subhanallah.

  "Mama watoto Skuli wananiuliza mbona ngozi yangu ipo hivi" Ndivyo anavyoanza kusema Mtoto Nairat Khamis Ali alipokuja katika ofisi za Mwananchi Zanzibar kwa ajili ya mahojiano.
  Nairat mwenye umri wa miaka 7 Mkaazi wa Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba amelazimika kukatisha masomo yake ya Nursery (Chekechea) kutokana na ugonjwa wa ngozi alioupata na kumsumbua kwa muda sasa akisumbuliwa tokea akiwa na miaka miwili.

  Nairat ni mtoto mcheshi na mwenye kuongea sana ambapo matumaini yake ni makubwa ya kupata elimu na kuendelea kusoma lakini anasema ikiwa atapata nafuu ataendelea na masomo yake.

  "Nataka mie kusoma lakini naumwa sasa hivi nikitibiwa na nikipona nitarudi zangu skuli na pia nilikuwa nasoma chuoni na najua kusoma Quraan lakini sasa hivi ndio nimekuja Unguja kwa kutafuta dawa" alisema Nairat huku akiwa ameinamisha uso mwake chini.
  Unapomuona Nairat unajua kama ni mgonjwa na anasumbuliwa na maradhi ambayo bado hawajajua ufumbuzi wake wala dawa kutokana na kuwa kwanza ngozi yake imepiga weusi na imefanya mabaka lakini pia ukimuona machoni utaona vidonda ambavyo vimezunguka katika mdomo wake na katika macho ambapo tayari macho yake yameshaathirika na kuanza kupoteza nuru.
  Pia Nairat mdomo wake umejaa vidonda na anashindwa kula kutokana maumivu na kuchonotwa anapotia chakula mdomoni na hivyo muda mwingi hukaa na njaa kwa kuogopa maumivu. Kutokana na kuwa na vidonda ndani na nje ya mdomo wake, Mama Mzazi wa Nairat aitwaye Khadija Mohammed mwenye umri wa miaka 30 na mwenye watoto wanne anasema usiku kucha Nairat analia na kuugua kutokana na maumivu.

  "Wallahi mwanangu usiku yuwalia tu kwa maumivu na hapo nyuma nilikuwa nikimpa dawa angalau akilala lakini dawa zimeniishia kwa kuwa sina pesa" alisema kwa masikitiko Bi Khadija ambaye ana watoto wawili wenye matatizo kama hayo na kuongeza kuwa.
  "Kula hawezi kwani akitia chakula tu yuwalia asema aumia lakini maji ndio achwa sana"

  Kwa mujibu wa Bi Khadija ambaye amefuatana na watoto wake wawili ambao wote ni wagonjwa amesema analazimika kununua dawa za kupunguza maumivu shilingi 70,000 na kumpatia mwanawe huyo dogo. Mbali ya Nairat mtoto mwengine ni Bisambe (25) ambaye pia ana ugonjwa wa ngozi kama wa Nairat na anasumbuliwa na hivi sasa ameacha masomo kutokana na kuhangaikia matibabu na watoto wengine ni Yussra (5) na Abdul (2) ambapo wawili hao wadogo bado hawajaathirika na ugonjwa huo. Mwenyeenzi Mungu awaepushe na hao wengine awape tiba ya uhakika wapumzike na mateso wayapatayo inshallah.

  "Hawa watoto wawili tokea wadogo wamepata ugonjwa huu na nimejaribu kutafuta tiba lakini unajua tena ukiwa masikini huna pesa basi unashindwa …muda mrefu nilikuwa nataka kuja Unguja lakini nikishindwa na hiyo pesa" alisema Bi Khadija.
  Mama huyo anasema awali watoto wake walipopata maradhi hayo yalianzia kidogo kidogo na kuanza kuwapa katika hospitali za huko huko Pemba na baadae alilazimika kuja Unguja baada ya madaktari kumshauri lakini hata alipofika hapa alitakiwa kwenda Dar es Salaam ambapo anasema ameshindwa kutokana na fedha.

  "Bado mnahangaika kwanza nniambiwa nende Wete nakwenda sepata dawa ..tena napata ntu aniambia nende Wete haya nenda huko napata dawa lakini neshindwa na pesa za kununulia dawa hata hapo nlipopata nikanunua na weanza kutumia na hepata nafuu na baadae nekwenda huko ChakeChake pia nishindwa na pesa" alisema kwa huzuni.

  Mama huyo anasema mbali ya kuhangaika huko Pemba akashauriwa kuja Unguja na kutafuta matibabu ambapo alilazimika kumuchisha mwanawe skuli na kuja hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo alipatiwa dawa na kushauri ende katika hospitali ya Kikatoliki iliyopo Machui ambapo alipata matibabu.

  "Nilipelekwa Machui nepata dawa lakini sikuweza kuendeleza kwa kuwa zimenishinda sekuwa na fedha za kutosha" alisema Bi Khadija huku akiwaangalia watoto wake machoni. Baada ya kuonekana na madaktari na hospitali ya Mnazi Mmoja kushindwa kumtibu walimshauri Mama huyo kumpeleka mtoto wake Dar es Salaam na kumtaka atafute shilingi millioni mbili kwa ajili ya matibabu.
  "Madaktari walinambia nitafute shilingi millioni mbili lakini takia nimeaambiwa hivyo hadi leo hii sijapataa taaa shilingi" alisema kwa masikitiko Bi Khadija.

  Katika kuhangaikia matibabu ya watoto wake hao nasa huyo mdogo Nairat, Bi Khadija alisema amekwenda ofisi ya Mufti Zanzibar na kupewa fomu za kuombea misaada kwa wafadhili na watu mbali mbali lakini bahati mbaya licha ya kuhangaika mwezi mzima wa Ramadhani lakini hajafanikiwa kupata hata shilingi. Anasema alipokwenda hospitali Madaktari walimshauri ajitahidi kupata fedha ili mtoto wake huyo atibiwe kwani atakapochelewa hali itazidi kuwa mbaya zaidi na itashindikana kufanyiwa matibabu kwa kuwa atakuwa ameshaathirika ikiwemo jicho lake lenye mtoto ambalo linahitaji kufanyiwa operesheni.

  Hata hivyo Bi Khadija anawaomba watu wenye imani na watoto wake hasa huyo mdogo wamsaidie fedha kwa ajili ya matibabu ili kuweza kunusuru maisha ya mtoto huyo ambaye kwa sasa anapata maumivu makali hasa nyakati za usiku na haifahamiki yanayotokana na nini. Tunahitaji kupata ushauri wa wataalamu wa afya na tunawaomba wenye uwezo wa kuwasaidia hawa watoto watuelekeze nini tufanye. Lakini pia kwa wale wenye uwezo wa fedha hata kama wana shilingi elfu tano (5,000) basi nawaomba wasisitize kuwasiliana nasi kwa kutuletea msaada wa tafadhali.

  Anuwani zetu ni:
  Salma Said,
  P. O. Box 1442,
  Tel: +255 (024) 223 5219
  Mobile: +255 777 477 101
  E-mail: muftiiy@yahoo.com

  Hassan Mussa Khamis
  Mobile: +44 7588550153
  email: hassan.mussa@gmail.com
  United Kingdom

  Kumbuka kutoa ni moyo na sio utajiri na haba na haba hujaza kibaba lakini unapotoa fedha yako haipotei bali bure unamkopesha Mwenyeenzi Mungu na bila ya shaka utaikuta huko wendako inshallah.

  Salma Said
  [​IMG][​IMG][​IMG]

  Related Posts
   
 2. PhD

  PhD JF-Expert Member

  #2
  Aug 24, 2012
  Joined: Jul 15, 2009
  Messages: 3,819
  Likes Received: 818
  Trophy Points: 280
  Tuhamasishane tutoe kwa moyo
   
Loading...