wakuu nimejaribu kupitia tangazo la SUMATRA kuhusu bei mpya za nauli lakini sjaelewa kiasi halisi cha nauli kutoka mkoa moja hadi mwingine kwa sasa.
SUMATRA yatangaza nauli
mpya za Mabasi Ya
Mikoani.......Nauli za Daladala
Hazitabadilika
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na
Nchi kavu jana imetangaza nauli mpya za usafiri
ambapo Mabasi ya abiria ya masafa marefu
nauli zake zikipungua huku daladala nauli
zikibaki vile vile.
Akitangaza Viwango hivyo vipya vitakavyoanza
kutumika tarehe 30 mwezi huu Mkurugenzi Mkuu
wa SUMATRA Gilliadi Ngewe alisema baada ya
mchakato wa kupanga bei kukamilika, bei za
mabasi ya Masafa ya mbali zimeshuka kwa
asilimia 5.8 hadi 7.8 kwa kilometa kulingana na
daraja la basi.
Ngewe amesema kuwa mabasi ya daraja ya
chini yamepungua kutoka shilingi 34.8 hadi 34
kwa kilometa, Daraja la kawaida toka shillingi
46.1 hadi 42.5 kwa kilometa na daraja la kati
toka shilingi 53.2 hadi 50.1 kwa kilometa huku
dalalada zikishuka kwa shillingi 23 lakini kwa
usumbufu wa chenji Nauli zitabaki vile vile.
Kwa Upande wa wamiliki wa daladala kupitia
kwa mwenyekiti wao Sabri Mabrouk wao
wanataka nauli iongezeke toka 400 ya sasa
mpaka 600.
------
TAARIFA KWA UMMA
NAULI ZA MABASI YA MASAFA MAREFU NA
MIJINI
1.0 UTANGULIZI
Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2014 bei ya
mafuta yatumikayo katika vyombo vya usafiri
wa abiria nchini ilianza kushuka. Kufuatia
kushuka huko kwa bei, Mamlaka ya Udhibiti
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)
ilikuwa ikipokea wito wa kupitia upya viwango
vya juu vya nauli ambavyo viliwekwa na
Mamlaka mwezi Aprili, 2013. Hivyo SUMATRA
ikaamua kuandaa mikutano ya wadau kwa lengo
la kukusanya maoni kuhusu haja ya kurekebisha
viwango vya nauli zilizopo.
Aidha, tarehe 09 Machi, 2015, Baraza la Ushauri
la Watumiaji wa Huduma Zinazodhibitiwa na
SUMATRA (SUMATRA Consumer Consultative
Council (SCCC)) liliwasilisha kwa Mamlaka ya
Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA) maombi ya kushusha nauli za
mabasi ya masafa marefu na mijini. Katika
maombi hayo Baraza liliainisha sababu za
kuomba punguzo hilo kuwa ni kushuka kwa bei
za mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi
mapya kutoka asilimia 25 hadi 10; punguzo hilo
lilianza Julai, 2014.
1.1 MAOMBI
1. Usafiri wa Mijini: Katika usafiri wa mijini,
maombi yalikuwa ni kupunguza nauli kwa
asilimia 25; hivyo kwa njia yenye umbali wa
kilomita 10, nauli iliyopo sasa ya TZS 400
ilipendekezwa kushushwa hadi kufikia TZS
300.
2. Usafiri wa Masafa Marefu: Maombi yalikuwa
ni kushusha nauli iliyopo kwa kilometa moja
anayosafiri abiria katika basi la kawaida
kutoka TZS 36.89 hadi TZS 28.05; punguzo
la asilimia 23.96. Aidha, kwa basi la hadhi
ya juu (luxury bus) kushusha kutoka TZS
58.47 hadi TZS 47.19; punguzo la asilimia
19.29.
2.0 UTARATIBU WA KUFANYA MAPITIO YA
NAULI
SUMATRA iliyafanyia kazi maombi hayo kwa
mujibu wa Sheria ya Udhibiti Usafiri wa Nchi
Kavu na Majini (SUMATRA), Sheria ya Bunge
Na.9 ya Mwaka 2001, na Kanuni za Tozo za
Mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na
kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo
watoa huduma, watumiaji wa huduma
pamoja na wananchi kwa ujumla ili kupata
maoni yao. Ushirikishwaji huo ulifanywa
kupitia mikutano iliyofanyika tarehe 9 Machi,
2015 Mkoani Mwanza; tarehe 12 Machi, 2015
Mkoani Kigoma; na tarehe 18 Machi, 2015
Jijini Dar es Salaam. Maoni yaliyotolewa
katika mikutano hiyo yalizingatiwa katika
tathmini na Mamlaka.
Taarifa ya tathmini na mapendekezo ya
viwango vipya vya nauli iliwasilishwa kwa
Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA kwa ajili
ya maamuzi.
3.0 NAULI ZA MIJINI
Bodi ya Wakurugenzi ya SUMATRA ilikutana
Jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili, 2015 ili
kupitia taarifa ya tathmini na mapendekezo
ya viwango vya nauli kwa ajili ya maamuzi.
3.1 Masuala Yaliyobainika
Kufuatia tathmini iliyofanywa ya usafiri wa
mijini, BODI ilibaini kwamba:
1. Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka
ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati
viwango vilivyopo sasa vilipoanza kutumika
Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei
ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia
Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa
lita katika vituo ulishuka mpaka TZS
1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani
ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
2. Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili,
2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta
imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba
kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
3. Gharama za mafuta zilikuwa muhimu
kuzingatiwa pamoja na gharama nyinginezo,
ambazo zilifikia asilimia 70 ya gharama za
uendeshaji.
4. Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya
kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na
thamani ya shilingi na mabadiliko hayo
yalipaswa kuzingatiwa katika kukokotoa
viwango vya nauli.
5. Punguzo la ushuru wa forodha kwa uagizaji
wa mabasi mapya ulikuwa na faida katika
kuchochea uingizaji wa mabasi mapya nchini
ili kuboresha hali ya usafiri nchini. Hata
hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo
nchini kwa sasa hayakupata punguzo hilo
kwa kuwa yaliingizwa kabla ya Julai, 2014
punguzo hilo lilipoanza kutumika.
6. Mazingira ya uendeshaji na utoaji huduma za
usafiri mijini yanapaswa kuzingatiwa ili
kufikia viwango vya nauli ili kuifanya huduma
ya usafiri kuwa endelevu. Kwa upekee,
ongezeko la msongamano wa magari mijini
na athari zake katika utoaji wa huduma za
usafiri mijini zinapaswa kuzingatiwa.
7. Gharama za utoaji huduma za usafiri mijini
zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake,
ikiwa ni pamoja na punguzo la bei ya
mafuta, ili kufikia viwango vya nauli
vinavyostahili.
8. Baada ya kuzingatia vigezo muhimu katika
ukokotoaji wa nauli, punguzo lililojitokeza
katika viwango vya nauli kikomo ni kama
inavyobainishwa hapa chini:
Viwango Vya Nauli Kutokana na Ukokotoaji
Njia Nauli ya Sasa Nauli iliyokokotolewa %
0 - 10 km (+CBD) 400 376.77 5.8
11 - 15 km 450 448.62 0.3
16 - 20 km 500 485.34 2.9
21 - 25 km 600 583.34 2.8
26 - 30 km 750 742.74 1
3.2 Maamuzi ya BODI
Baada ya kutafakari viwango vilivyotokana na
ukokotoaji uliozingatia masuala muhimu
yaliyoainishwa, BODI imeridhia viwango vya
nauli vilivyopo sasa kuendelea kutumika.
Uamuzi huu unatokana na punguzo
lililokokotolewa Kuwa dogo ikilinganishwa na
viwango vilivyopo sasa. Aidha, viwango
vilivyokokotolewa iwapo vitapitishwa
vitasababisha usumbufu katika malipo.
1. Viwango vya Nauli Mpya kwa Watu Wazima
Viwango vipya vya nauli kikomo vya mabasi
ya mjini vilivyoridhiwa kwa watu wazima ni
kama ifuatavyo:
Viwango Vya Nauli Mjini Vilivyoridhiwa
Njia Nauli ya Sasa
(TZS)
Viwango Vilivyoridhiwa
(TZS)
0 - 10 km (+CBD) 400 400
11 - 15 km 450 450
16 - 20 km 500 500
21 - 25 km 600 600
26 - 30 km 750 750
1. Viwango vya Nauli Mpya kwa Wanafunzi
BODI imeamua kuwa nauli ya mwanafunzi
nayo ibaki kama ilivyo nauli ya sasa ambapo
mwanafunzi analipa TZS 200.
1. VIWANGO VYA NAULI ZA MABASI YA
MASAFA MAREFU
BODI ilipokea tathmini kuhusu nauli za usafiri
wa masafa marefu.
4.1 Masuala Yaliyobainika
Kufuatia tathmini iliyofanywa ya nauli kikomo
za usafiri wa masafa marefu, BODI ilibaini
kwamba:
1. Bei ya mafuta ilikuwa imeshuka
ikilinganishwa na bei iliyokuwepo wakati
viwango vya sasa vilipoanza kutumika
Mwezi Aprili, 2013; ambapo kwa wastani bei
ya lita ya dizeli iliuzwa TZS 2,071.67 kufikia
Machi, 2015 wastani wa bei ya Dizeli kwa
lita katika vituo ulishuka mpaka TZS
1,665.38; mwezi Aprili, 2015 bei ya wastani
ilipanda kufikia TZS 1,779.57.
2. Mwenendo wa bei za mafuta kufikia Aprili,
2015 unaonyesha kuwa bei ya mafuta
imekuwa ikibadilikabadilika na kwamba
kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda.
3. Gharama za ununuzi wa mafuta zilikuwa
muhimu kuzingatiwa pamoja na gharama
nyinginezo, ambazo zilifikia asilimia 70 ya
gharama za uendeshaji.
4. Kulikuwa na mabadiliko katika viashiria vya
kiuchumi kama vile mfumuko wa bei na
thamani ya shilingi na kwamba mabadiliko
hayo yalipaswa kuzingatiwa katika kufikia
viwango vya nauli.
5. Punguzo la ushuru wa forodha kwa uingizaji
wa mabasi mapya lilikuwa na athari chanya
katika kuchochea uingizaji wa mabasi nchini.
Hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi
yaliyopo nchini kwa sasa hayakupata
punguzo hilo kwa kuwa yaliingizwa kabla ya
punguzo hilo kuanza kutumika.
6. Katika ukokotoaji wa nauli ni muhimu
kuzingatia madaraja ya mabasi kama
yalivyoelekezwa katika Kanuni za Huduma za
Abiria, 2014 (The Road Transport (Passenger
Service) Regulations, 2014 zinazoainisha
madaraja manne ya mabasi;daraja la
kawaida la chini, daraja la kawaida la juu,
daraja la hadhi ya kati na daraja la Juu.
7. Gharama za utoaji huduma za usafiri kwa
ujumla wake zinapaswa kuzingatiwa kwa
madaraja mbalimbali ili kufikia viwango vya
nauli vinavyostahili.
8. Udhibiti wa nauli unapaswa kujielekeza
katika madaraja matatu yafuatayo: (1) daraja
la kawaida la chini, (2) daraja la kawaida la
juu na (3)daraja la hadhi ya Kati ili kutimiza
wajibu wa kuwalinda watumiaji wenye kipato
cha chini.
4.2 Maamuzi ya BODI
Baada ya kutafakari tarifa iliyowasilishwa
BODI iliridhia viwango vipya vya juu vya nauli
kwa mabasi ya masafa marefu kuwa kama
vinavyoonyeshwa hapo chini:
Viwango Vipya vya Nauli za Mabasi ya
Masafa Marefu
Daraja la Basi Nauli ya Sasa
(TZS/Abiria/Km)
Viwango Vipya vya Nauli
Vilivyoridhiwa
(TZS/Abiria/Km)
Daraja la Kawaida la Chini
(Lower Ordinary bus -Lami
36.89 34.00
Daraja la Kawaida la Chini
Lower Ordinary Bus) - Vumbi
46.11 42.50
Daraja la Kawaida la Juu
(Upper Ordinary Bus)
- 44.96
Daraja la Kati
(Semi-Luxury Bus)
53.22 50.13
BODI pia imeamua kwamba nauli za mabasi ya
hadhi ya juu ( luxury bus) hazitadhibitiwa ili
kuchochea ubunifu katika utoaji huduma na
ushindani kati ya huduma za barabara na njia
nyinginezo za usafiri.
Mamlaka imeandaa majedwali ya nauli kwa
kuzingatia viwango vipya. Majedwali hayo
yanaweza kupatikana katika tovuti ya Mamlaka
www.sumatra.go.tz .
HITIMISHO
Viwango hivi vipya vinapaswa kuanza kutumika
siku 14 baada ya taarifa kutolewa kwa umma.
Hivyo basi viwango hivi vitaanza rasmi tarehe
30 Aprili, 2015.
Wamiliki wa mabasi pamoja wafanyakazi wao
wanaagizwa kutoza viwango vya nauli
vilivyoridhiwa na Mamlaka.
Aidha, abiria na wananchi kwa ujumla
wanahamasishwa kutoa taarifa SUMATRA
kupitia namba za simu za bure ambazo ni
0800110019 na 0800110020 pale wanapotozwa
nauli ya juu zaidi ya nauli kikomo iliyoridhiwa.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
SUMATRA
15 Aprili, 2015