singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
Katibu wa NEC, Uenezi na Itikadi CCM Taifa, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa habari leo muda mfupi baada ya kumaliza kukagua uwanja wa michezo wa Namfua mjini hapa, mahali ambapo zitafanyika sherehe za kuadhimisha miaka 39 ya kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo kitaifa zinatarajiwa kufanyika mkoani Singida.Pamoja na mambo mengine,alisema kuwa CCM taifa imejipanga vema kuboresha viwanja vyake vya michezo kikiwemo cha Namfua ambacho taratibu za kumpata mkandarasi wa kukifanyia ukarabati mkubwa zinaendelea.
KATIBU wa NEC, Uenezi na Itikadi Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Nape Nnauye, amesema kuwa ana hofu kubwa kwamba vyama vya siasa vya upinzani sasa vipo hatarini kufa,kutokana na kasi kubwa ya kuwatumikia wananchi inayofanywa na CCM na serikali yake ya awamu ya tano.
Nape ambaye pia ni waziri wa habari na michezo,alisema kuwa kasi ya utendaji inayofanywa na rais Dkt. John Pombe Magufuli toka ameingia ikulu, imechangia vyama vya siasa vikose ajenda na sera ambazo zinaweza kuwashawishi wananchi kuviamini na kuvipa kura.
Katibu huyo ameyasema hayo leo muda mfupi baada ya kukagua uwanja wa michezo wa namfua mjini hapa,mahali sherehe za maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 39 toka kianzishwe.
“Kwa kweli kuna kila dalili ya kufa kwa vyama vya siasa vya upinzani wakati wo wote kuanzia sasa.Tunavipenda na hiyo tutafanya kila litakalowezekana ili kuhakikisha vyama vya siasa vya upinzani havifi,viendelee kuwepo kwa minajili ya kudumisha demokrasia”alisema Nape.
Kuhusu maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 39,katibu huyo alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi sherehe za maadhimisho hayo ambayo kwa mwaka huu,yatahudhuriwa na viongozi wengi kutoka andani na nje ya nchi pamoja na wananchi kwa ujumla.
“Sherehe za maadhimisho ya mwaka huu,zitakuwa za aina yake kwa sababu zitahusisha na kitendo cha CCM kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kushika dola kwa mara nyingine tena.Kwa vyo vyote wakazi wa mkoa huu na hasa wa mji wa Singida,wajiandae kunufaika na ugeni utakao kuja wakati huo…mgeni njoo mwenyeji akope”, alisema katibu huyo.
Alisema kuwa kuanzia mwisho wa mwezi huu,sherehe hizo zitatanguliwa na viongozi wa ndani na nje ya mkoa,kushiriki kazi za maendeleo zikiwemo za kilimo,ujenzi wa taasisi za umma ikiwemo maabara,vyumba vya madarasa,vyoo,kujimbua mifereji na kufanya usafi.
“Falsafa ya ‘hapa kazi tu’ itatawala sana katika sherehe za mwaka huu. Vitafanyika shughuli nyingi za maendeleo ya wananchi. Nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kila mmoja kwa nafasi yake,achape kazi halali kwa bidii na maarifa. Hili taifa litajengwa na mtu mmoja moja kwa kutimiza wajibu wake wa kuiletea maendeleo endelevu”, alisema Nape.