Godwin Chilewa
Member
- Jan 27, 2018
- 6
- 12
Ni nani atakayetuondolea lile jiwe? Hili ndilo swali gumu zaidi walilojiuliza akina Mariam Magdalena, mama yake Yesu, na wale wanawake wengine ile siku ya kwanza ya juma. Nia yao ilikuwa kwenda kaburini, kumpaka mafuta Yesu (aliyeuawa na kuzikwa) ili kukamilisha taratibu za maziko ya kiyahudi. Lakini pamoja na nia yao njema, mbele yao vilikuwepo vikwazo lukuki vya kuwakatisha tamaa.
Kikwazo cha kwanza kilikuwa ni jiwe lililowekwa mlangoni mwa kaburi. Jiwe hilo lilikuwa kubwa mno, na walijua kwa vyovyote vile isingekuwa rahisi kuliondoa ili waweze kuingia ndani. Pili, kaburi lenyewe lilikuwa likilindwa na askari wa kirumi waliokuwa wakisifika kwa ushujaa wao. Askari hawa walikuwa hawalali wakati wa lindo, na hawanunuliki kwa urahisi.Tatu kaburi lenyewe lilikuwa limepigwa muhuri wa gavana (SEAL) ili kuzuia watu kulifungua. Pamoja na ugumu wa vikwazo hivyo kina Mariam waliamua kwenda kaburini kujaribu kila litakalowezekana ili watimize wajibu wao. Ashukuliwe Mungu walipofika kaburini walikuta jiwe limeviringishwa mbali, askari wamekimbia, na Yesu amefufuKa.
Leo hii sisi pia tunakabiliana na hali ileile waliyokuwanayo kina Mariam, na yamkini wengi wetu tumeanza kujiuliza swali lilelile! Ni nani atakaye tuondolea lile hili jiwe! Naama, jiwe la hali ngumu ya maisha linalowafanya wengi wetu kuishi maisha ya unyonge na umaskini. Jiwe la tamaa mbaya ya mali linalofanya vijana wetu wauawe kwa madawa ya kulevya, magonjwa ya zinaa, na wengine kunyongwa ughaibuni??. Na jiwe la talaka linalo sambaratisha ndoa na kuongeza watoto wa mitaani je?? Tena nani atakayetuondolea Jiwe la dhuluma za haki za wanyonge kwa kisingizio cha kutafuta mali, au kuleta maendeleo? Nani atakayetuondolea jiwe hili la mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa sababu za kisiasa, kiuchumi, na au kijamii? Nani atakayethubutu hata kulikaribia jiwe hilo kama lina muhuri (SEAL) wa gavana au mtu mwingine mwenye mamlaka? Nani, nani, nani?
Kwa mtazamo wa kibinadamu unaweza kusema hakuna! Haiwezekani...Jiwe ni kubwa mno! Lakini nikutie moyo ndugu yangu, kuwa lisilowezekana kwa mwanadamu, kwa Mungu linawezekana (Yeremia 33:3). Kumbe sisi pia tunao uwezo wa kuliondoa kila aina ya jiwe linalotusumbua, hata kama jiwe hilo linaonekana kubwa kupita kiasi. Nia ya kuliondoa jiwe hilo, na hatua za awali tunazochukua ni muhimu mno katika mafanikio yetu ya kimwili, kiroho na kiakili. Kumbuka kina Mariam waliamua kwendaW kaburini huku wakijua ukubwa wa matatizo yaliyokuwa mbele yao. Lakini kwa sababu walikuwa na nia moja, waliamua kuchukua hatua wakiamini Mungu atawawezesha. Sisi pia tunapaswa kuchukua hatua sahihi, zinazoweza kutusaidia kuboresha hali tuliyonayo pasipo kumkosea Mungu, au kutuingiza katika majuto.
Kumbe basi, ni vema kumuomba mwenyezi Mungu ili atupe hekima, na uwezo wa kuyashughulikia yale yanayotukera. Zaidi sana tuwaombee wale wenye mamlaka ili Mungu aseme nao na kuwaponda mioyo yao ili waweze kujua wajibu walionao kwa Mungu na kwetu pia (Methali 16:7).
Mungu akubariki
Rev. Godwin Chilewa