Nani atajibu hoja za Lissu?

Nani atajibu hoja za Lissu?

TIGOPESA

Senior Member
Joined
Apr 2, 2014
Posts
190
Reaction score
63
NIMEMSIKILIZA vema Tundu Lissu. Amesema bungeni na kwenye mikutano ya hadhara.
Wasiomwelewa, au wanaoogopa kujibu hoja zake, bila shaka kwa kutokuwa na majibu, wamekimbilia kusema kwamba Lissu ametukana waasisi wa nchi.
Lissu anauliza maswali magumu. Wanaojaribu kumpinga wanatoa majibu rahisi. Wanapozidiwa wanatoa matusi, au wanasingizia kwamba ametukana waasisi, hasa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Amesema nini? Leo nitajadili hoja mbili za Lissu ambazo hazijapata majibu kutoka kwa watawala au wafuasi na mashabiki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hoja yake ya kwanza ni kwamba historia ya Tanzania imepotoshwa. Anasema kuna mambo yasiyo ya kweli ambayo tumelishwa kwa miaka 50 kuhusu Zanzibar, Tanganyika na Tanzania. Wakubwa hawataki tuyaguse au tukosoe pale tunapobaini kasoro.
Kwa mfano, kuhusu uhuru wa Zanzibar, Lissu anasema mambo mawili, kwamba ingawa shuleni watoto wanafundishwa kuwa Zanzibar ilipata uhuru wake tarehe 12 Aprili 1964, ukweli ni kwamba uhuru wa Zanzibar ulipatikana tarehe 10 Desemba 1963.
Na ili kuthibitisha hilo, anasema Zanzibar ilipata uanachama wa Umoja wa Mataifa tarehe 16 Desemba 1963, siku moja na Kenya.
Mantiki ni moja. Nchi haiwezi kupata uanachama wa Umoja wa Mataifa kama ni koloni. Lazima kwanza iwe nchi huru. Kwa hiyo, isingewezeka Zanzibar ipatie uhuru 12 Januari 1964 wakati ilishapata uanachama katika Umoja wa Mataifa mwezi mmoja uliopita.
Lakini Lissu ana hoja ya nyongeza. Na hii ndiyo inayowakoroga watu wasiotaka historia isahihishwe.

Anasema uhuru wa Zanzibar ulikoma baada ya miezi mitano na siku kadhaa. Tarehe 22 Aprili 1964, siku waasisi wawili, Mwalimu Nyerere na Karume walipotiliana sahihi katika mkataba wa Muungano, ndipo uhuru wa Zanzibar ulipokufa.
Zanzibar haijawahi kuwa huru tena. Kwa lugha ya Lissu na baadhi ya wanaharakati, hasa Wazanzibari, Zanzibar iligeuka koloni la Tanganyika tangu siku hiyo, na haijawahi kujiondoa kwenye "ukoloni" huo, na ndiyo maana imekuwa inapigania mfumo wa serikali tatu.
Maneno haya ndiyo yanakera wahafidhina wa Muungano, lakini Lissu ana ufafanuzi. Nchi huru ina sifa zipi? Yaani, kwa kutumia mfano wa Zanzibar, ilikuwa na sifa zipi ilipokuwa huru kati ya 10 Desemba 1963 na 22 Aprili 1963?
Zanzibar ilikuwa na uhuru na mamlaka ya kuendesha uhusiano wa kimataifa. Ndiyo maana ilifungua ofisi za kibalozi katika nchi kadhaa, zikiwamo Uingereza, Misri, na Umoja wa Mataifa.

Sifa ya pili ni kuwa na udhibiti wa masuala ya uchumi, sarafu na fedha. Zanzibar ilikuwa mwanachama wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki pamoja na Tanganyika, Kenya na Uganda.
Lakini mwaka 1964 ilinyang'anywa mamlaka hayo, yakabaki kwa Tanganyika. Na kwa mujibu wa Lissu, jambo hili ndilo lilizua mgogoro wa kwanza kati ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume miaka miwili baadaye.
Ilikuwa hivi. Mwaka 1964 nchi wanachama wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki ziliamua kila nchi iwe na Benki Kuu yake.
Katika mjadala wa utekelezaji wa suala hilo, kwa mujibu wa Lissu, maofisa walioshiriki vikao hivyo kutoka Wizara ya Fedha ya Muungano (Tanganyika), walishawishi maofisa wa Kiingereza wa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kwamba Zanzibar isialikwe kwenye kikao cha uamuzi wa hatima yao na uundwaji wa Benki Kuu. Zanzibar ikaondolewa rasmi.

Ukumbuke kuwa Hati ya Muungano ilikuwa na mambo 11 tu. La 12 liliongezwa mwaka 1965. Tarehe 10 Juni 1965 Bunge la Jamhuri ya Muungano lilipoketi Karimjee, Dar es Salaam, lilileta muswada wa siri wa kurekebisha Katiba ya Mpito, ili kuongeza masuala ya Fedha, Sarafu na Benki Kuu katika orodha ya mambo ya Muungano.
Kwanini siri? Muswada huu haukuwa katika orodha ya shughuli za Bunge siku hiyo kama inavyotakiwa kiutaratibu. Wakati Bunge linaendelea, ndipo Makamu wa pili wa Rais, Rashid Mfaume Kawawa, alipomweleza spika kwamba "wakati umefika sasa tufanye lile jambo ambalo tulisema liwe siri."
Inasemekana lilijadiliwa na mbunge mmoja tu wa Morogoro Kusini, Kapilima, likapitishwa haraka haraka. Baadaye Bunge likapewa pumziko la dakika 15, ili kwanza muswada usainiwe na rais.
Ama ilipangwa au ilikuwa bahati mbaya, Rais Nyerere siku hakuwa Ikulu. Alikuwa safari. Kwa hiyo, aliyeombwa kuweka saini ni Rais Karume. Ikawa sheria pale pale.

Lakini katika kuonyesha kuwa Rais Karume alisaini kitu asichoelewa vema, mwaka mmoja baadaye ilipoanzishwa Benki Kuu ya Tanzania, Rais Karume alitaka Zanzibar pia ianzishe Benki Kuu ya Zanzibar.
Mwalimu Nyerere akamkatalia. Alipohoji kwanini, akaonyeshwa sahihi yake, kwamba suala hili ni la Muungano. Baada ya msuguano wa miaka miwili, Rais Karume alifanikiwa kuanzisha Benki ya Watu wa Zanzibar, ambayo ni benki ya biashara kama zilivyo nyingine. Si Benki Kuu!
Si hilo tu. Huko nyuma iliundwa Tume ya Pamoja ya Fedha ili kuweka utaratibu wa jinsi ya kugawana mapato. Haijawahi kufanya kazi.
Hata mwaka 1977 kwa ushawishi wa Rais Aboud Jumbe wa Zanzibar, liliingizwa pendekezo kwenye katiba, la kuwa na akaunti ya pamoja ya Jamhuri ya Muungano, ili kunufaisha nchi washirika kwa usawa.

Hadi sasa akaunti hiyo haipo. Zanzibar haijapata hata senti 10. Kila pesa inayotoka nje ya nchi kwa jina la Jamhuri ya Muungano ilipaswa kugawanywa sawa kati ya washirika. Pesa zote, isipokuwa za msaada wa bajeti, huishia Tanganyika.
Pesa za miradi ya maji, barabara, elimu, afya, kilimo na sekta nyingine, huingizwa kwa jina la Muungano, lakini huelekezwa kwenye miradi ya Tanganyika pekee. Kwa mantiki hii, Tanganyika ndiyo Tanzania, na inainyonya Zanzibar kiuchumi.
Kwa hiyo, kwa Zanzibar kupoteza kabisa udhibiti wa Sarafu na Benki Kuu, imekosa sifa nyingine ya kuwa nchi huru. Na hiyo ni sababu nyingine ya Wazanzibari kudai mamlaka kamili.

Ni sababu ya nyongeza kwao kudai kwamba nchi yao imegeuzwa koloni la Tanganyika. Ni hoja ya ziada kwao kudai serikali tatu.
Hii inatuleta katika hoja ya pili ya Lissu inayoleta ukakasi kwa baadhi ya watawala, na kufika mahali pa kusema ametukana waasisi. Ni hii iliyotajwa hapo juu, ambayo pia ilisisitizwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano.
Maana bila kuthibitisha hoja hiyo, ile ya Zanzibar kuwa koloni la Tanganyika itakosa mashiko.
Katika kuifafanua, Lissu anaturudisha kwenye historia. Kwamba asubuhi tarehe 26 Aprili 1964, siku ya Muungano, kabla Mwalimu hajaenda Mnazi Mmoja kuchanganya udongo, alitunga amri mbili muhimu, zikawa sheria pale pale.
Ikumbukwe kuwa Amri hizi (decree) hutungwa na watawala wa kijeshi, au walioingia madarakani kwa Mapinduzi, kama ilivyokuwa Zanzibar ya Karume.
Nchi yenye Rais aliyechaguliwa na wananchi kama alivyokuwa Nyerere, na yenye Bunge kama ilivyokuwa Tanganyika, haitarajiwi kuongozwa na, au kufungiwa, sheria za namna hii.

Nyerere alitunga mbili. Ya kwanza, ilikuwa Amri ya Masharti ya Mpito, ambayo iliagiza kwamba watumishi wote wa Serikali ya Tanganyika, kuanzia siku hiyo walijulikana kama watumishi wa Jamhuri ya Muungano. Haikuhusu watumishi wa Zanzibar.
Vile vile, iliagiza kwamba Mahakama Kuu ya Tanganyika ilikuwa inabadilika na kuwa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano. Ikaagiza pia kuwa nembo ya taifa la Tanganyika (ya bibi na bwana) igeuzwe kuwa nembo ya Jamhuri ya Muungano.
Amri ya pili, ambayo nayo ilitungwa asubuhi hiyo, ilijulikana kama Amri ya Katiba ya Mpito, iliagiza kuwa kuanzia siku hiyo, Katiba ya Tanganyika ndiyo iwe Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Tarehe 10 Juni 1964 ikatungwa sheria kwamba mahali popote palipotajwa kama Tanganyika paandikwe Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na mali zote zenye jina hilo zitangazwe kuwa ni za Jamhuri ya Muungano.
Yote haya hayakuihusu Zanzibar. Pole pole, Tanganyika ikawa ndiyo Tanzania, kisheria. Ndivyo ilivyovaa koti la Muungano. Na ndivyo imeendelea kutawala Zanzibar.
Na ndiyo maana watawala wa Zanzibar baada ya Aboud Jumbe wamekuwa "wanatengenezewa" ama Dodoma au Dar es Salaam, si Unguja!
Na katika kipindi chote hadi mwaka 1984, Tanzania haikuwahi kuwa nchi moja. Zilikuwa tatu – Zamzibar, Tanganyika (iliyofichika katika Muungano) na huo muungano wenyewe.

Lakini hoja ya serikali tatu ilipoibuliwa na Rais wa Zanzibar Aboud Jumbe mwaka 1983, hadi akafukuzwa, ndipo watawala waliposhtuka na kuingiza kifungu kinachotamka kuwa Tanzania ni nchi moja mwaka 1984.
Ndiyo maana Tume za Jaji Francis Nyalali, Jaji Kisanga, Jaji Warioba, na Wazanzibari wengi katika nyakati tofauti, wamekuwa wanataka serikali tatu.
Hali hii haiwezi kuendelea milele. Miaka 50 imetokana kwa watu kutafakari na kujipanga upya.
Kinachotafutwa sasa ni katiba mpya ambayo itasahihisha makosa ya zamani. Itengenezwe katiba mpya ambayo itaweka utaratibu mpya wa uhusiano usio wa shaka kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Itengenezwe katika ambayo itaweka utaratibu wa haki kati ya nchi zote mbili, utakaoivua Tanganyika koti la Muungano, na kuitoa mafichoni.
Ni utaratibu utakaoweka misingi ya uratibu wa mambo ya pamoja ambayo Watanganyika na Wazanzibari wanapaswa kushirikiana, huku wakiheshimiana.
Unatafutwa utaratibu ambao utafufua uhuru wa Zanzibar na kuiruhusu kujiendeleza bila kunyonywa na Tanganyika, ambayo chini ya muungano wa sasa, imehodhi mapato yanayopatikana kwa jina la Muungano na kuisababishia Zanzibar umasikini inaopambana kujinasua nao.
Juzi akiwa Pemba, baada ya kufafanua yote hayo, Lissu akahoji: "Kwa miaka 50 iliyopita, Wazanzibari wamekuwa wanataka Serikali ngapi?" Wananchi wakajibu: "Tatu."

"Aboud Jumbe alitaka ngapi?" "Tatu." "Maalim Seif alitaka ngapi?" "Tatu." "Jaji Nyalali alitaka ngapi?" "Tatu." "Jaji Kisanga alitaka ngapi?" "Tatu." "Jaji Warioba amependekeza ngapi?" "Tatu."
Nasubiri mtu atakayepangua hoja na kujibu maswali ya kihistoria yaliyoibuliwa na Lissu, moja baada ya jingine.
 
hakuna kitu muhimu katika maisha ya mtu kama kusema ukweli, ukweli wa Lisu ni pigo kwa wababaishaji wa siasa
 
Mkuu TIGOPESA hamna anaye weza kujibu haya maswali kutoka upande wa kijani, kwa sababu wale wenye uelewa na kujua haya mambo wamejificha kwenye mwamvuli wa kutetea kitumbua chao, na wengine walio wengi ni vilaza sana neno kujenga hoja kwao ni msamiati mpya. Ndio maana unaona wameamua tu kushikilia kuwa Tundu katukana wazee wetu.
 
Back
Top Bottom