Nani anayechochea vurugu Zanzibar?

Nani anayechochea vurugu Zanzibar?

Kakke

JF-Expert Member
Joined
Dec 4, 2010
Posts
1,883
Reaction score
1,482
rajab.jpg
Barazani kwa Ahmed Rajab

Ahmed Rajab Raiamwema

KUNAFUKUTA chini kwa chini Zanzibar na wakuu wa serikali pamoja na wanasiasa wasipochukua hadhari tunaweza tukashuhudia marejeo ya matumizi ya nguvu, ugandamizaji wa wapinzani na ghasia kwa jumla.
Kwa ufupi, mafanikio yote yaliyopatikana tangu Oktoba 2010, hasa utulivu wa hali ya kisiasa, yanaweza yakenda arijojo.

Wiki iliyopita Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idi, akiwa Dodoma, alinukuriwa akisema kwamba "ametangaza vita kwa mtu yeyote anayepanga njama za kuvuruga mchakato wa Rasimu ya Pili ya Katiba".

Wakati huohuo alimkebehi Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha Civic United Front (CUF).

Siku chache kabla ya Balozi Idi kutoa hayo matamshi yake ya "kutangaza vita" Hamad alikariri tena msimamo wa chama chake kuhusu muundo wa Muungano. Akihutubia mkutano wa hadhara huko Kibandamaiti, Unguja, Machi 26, alisema kwamba chama chake hakitounga mkono muundo wa Muungano wa Serikali mbili na wala hotuba aliyoitoa Rais Jakaya Kikwete katika ufunguzi wa Bunge la Katiba.

Balozi Idi alinukuliwa akisema kwamba hali ikiendelea hivyo - yaani ikiwa Hamad ataendelea kudai pawepo Muungano wa Serikali tatu - basi Serikali ya Mapinduzi haitasita "kuwashughulikia" watu wote wa aina hiyo.
"Kuwashughulikia" maana yake ni kuwachukulia hatua zisizopendeza kama vile kuwatia ndani, kuwatesa au kuwafanyia mambo mengine ya kukirihisha.

Inasikitisha kusikia kwamba mtu mwenye hadhi kama ya Balozi Idi anatumia lugha kama hiyo ya vitisho wakati wa mjadala kuhusu Katiba mpya. Na huyu ni mwanadiplomasia wa siku nyingi mwenye uzoefu wa miaka mingi wa jinsi mambo yalivyo duniani. Anachotuambia ni kwamba ni sawa yeye kuutetea muundo wa Muungano wa serikali mbili lakini wenye kutaka muundo wa Muungano wa serikali tatu hawana haki ya kufanya hivyo. Ni wasaliti wanaostahiki "kushughulikiwa".

Matamshi kama hayo huashiria kwamba mwenye kuyatamka ana nia ya kuwadhuru watu wengine. Mamlaka nyingi za kisheria huviona vitisho aina hiyo kuwa ni vitendo vyenye kuhalifu sheria. Na wenye kutoa vitisho vya aina hiyo wanaweza wakafikishwa mbele ya mahakama na kushtakiwa kwa makosa ya jinai.

Wakuu wanapokuwa wanatoa vitisho vya aina hiyo huwa wanaamini kwamba lazima watumie vitisho na mabavu (utumizi wa nguvu) kuwatia hofu wananchi ili hao wananchi wasalimu amri na wakubali yale serikali inayoyataka.
Utumiaji wa nguvu na vitisho ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa kuwashurutisha watu, hasa wapinzani, wafuate msimamo au sera za serikali. Mbinu aina hizo hutumiwa sana na serikali katika nchi zenye mfumo wa demokrasia isiyopevuka. Mfano mzuri ni hapa kwetu.

Vitisho aina hiyo vinaweza hatimaye vikawa sababu ya kuzuka kwa mauaji ya kimbari, kukamatwa watu wasio na hatia kwa sababu za kisiasa, kutekwa nyara kwa wapinzani na baadaye kupotea wasijulikane walipo na mauaji ya wapinzani.
Tukiangalia historia ya hivi karibuni ya nchi kadhaa zenye mfumo wa demokrasia isiyopevuka tunaona kwamba viongozi wa serikali wenye midomo mirefu ya kutoa vitisho dhidi ya wapinzani, aghalabu, huwa ni viongozi walio dhaifu.

Viongozi hao huwa na tabia ya kuzidi kutoa vitisho vikali pale wanapohisi kwamba madaraka huenda yakawaponyoka, kwamba tawala zao zinayumbayumba na kwamba wapinzani wanaweza wakakishinda chama kinachotawala katika uchaguzi.

Kushindwa kwa serikali kuyaridhia matakwa ya wananchi wake mara nyingi husababisha mfumo wa kisiasa katika nchi uoze. Kuoza huko ndiko kunakowafanya watawala wakimbilie kutumia nguvu dhidi ya wapinzani ili kuunusuru utawala wao.

Kwa kweli nchi kama zetu zenye demokrasia isiyo imara zimo hatarini kwani serikali zao hazioni ajizi kuwagandamiza wapinzani kwa vile zinawaona wapinzani kuwa ni kitisho kwa madaraka yao. Kwa hivyo, viongozi wao nao hutumia vitisho vya nguvu za dola dhidi ya wapinzani. Hali huzidi kuwa mbaya pale wapinzani wanapokuwa wanatoa madai yenye kuungwa mkono na wengi wa wananchi lakini yenye kwenda kinyume na sera za chama kinachotawala.

Mfano mzuri ni huu tunaouona sasa Zanzibar ambako, kwa mujibu wa Tume ya Katiba, wananchi wengi hawautaki Muungano wa serikali mbili.
Kila pengo linapokuwa kubwa baina ya madai ya wapinzani na msimamo wa chama kinachotawala basi huwa ni vigumu kwa pande hizo mbili kuridhiana. Na madai au matakwa ya wapinzani yanapokuwa yanaungwa mkono na wengi wa wananchi basi hapo kunakuwa hatari ya kuzuka hali ya kisiasa isiyo thabiti na uwezekano mkubwa wa serikali kuanza kuwakandamiza wapinzani, na wakati mwingine, hata wasio wapinzani.

Hali inakuwa hivyo katika nchi zenye mfumo wa kidemokrasia isiyokamilika kwa sababu taasisi za dola, kwa mfano, mahakama au jeshi la polisi, zinakuwa hazina nguvu au uwezo wa kujiamulia mambo yao bila ya kuingiliwa na wakuu wa serikali. Ndiyo maana baada ya Balozi Idi kutoa matamshi yake ya vitisho tumesikia ya kuwa Jeshi la Polisi la Zanzibar limeanza uchunguzi wa kukichungua kikundi kinachojiita ‘Gaza' kinachosemekana kwamba kimewatahadharisha wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar wasirudi kwao endapo wataisaliti Zanzibar kwa kukubaliana na muundo wa Muungano wa Serikali mbili.

Kamishna wa Polisi wa Zanzibar, Hamdan Omar Makame, ananukuriwa akisema kwamba tayari jeshi lake limekwishaanza kazi ya kuzipitia kanda za video za maandamano yaliyofanywa na kikundi hicho katika mitaa kadhaa Unguja hadi kwenye ule mkutano wa hadhara wa CUF huko Kibandamaiti. Dhamiri ya uchunguzi huo, alisema, ni kukichukulia hatua za kisheria kikundi hicho.

Shtuma zilizotolewa ni kwamba kikundi hicho kilibeba bango lililokuwa na hayo maandishi ya kuwataka Wabunge wa Katiba kutoka Zanzibar wataokubali muundo wa Serikali mbili wasirudi Zanzibar. Inasemekana kwamba bango hilo lilitembezwa mitaani na halafu likapokewa na Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo.

Kamishna Hamdan amesema kwamba ameagiza matamshi yote ya mkutano yapitiwe "ili kuangalia makosa ya jinai yaliyotendeka kabla ya kuchukua hatua za kisheria."

Kwa matamshi yake Kamishna Hamdan alikwishaamua kwamba makosa ya jinai yalitendeka hata kabla ya uchunguzi kumalizika.Tuseme Kamishna anajipendekeza kwa serikali au anatii tu amri ya wakuu fulani wa serikali tunayoambiwa kuwa ni Serikali ya Umoja wa Taifa?

Polisi ya Zanzibar haina historia nzuri. Huu ni ukweli usiofichika. Ukatili wa polisi dhidi ya wapinzani wa serikali unajulikana na jumuiya zote za kimataifa zenye kupigania haki za binadamu, zikiwa pamoja na Amnesty International na Human Rights Watch.

Ripoti mbalimbali za mashirika kama hayo pamoja na ripoti za wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuhusu haki za binadamu Tanzania zimetaja jinsi jeshi hilo la polisi lilivyokiuka haki za binadamu katika nyakati mbalimbali, hasa tangu kurejelewa nchini kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Ni dhahiri kutokana na mambo yanavyokwenda Zanzibar hivi sasa kwamba Maalim Seif Sharif Hamad na wafuasi wake wanategewa mitego iwanase. Majaribio yalifanywa na yanaendelea kufanywa ya kukihusisha chama chake na ugaidi wa kimataifa lakini majaribio hayo yameshindwa nguvu kwa kukosekana ushahidi. Jaribio la sasa ni la kukifunganisha chama cha CUF na hicho kikundi cha Gaza.

La kushangaza ni kwamba hao vijana wa kikundi cha Gaza wanachunguzwa na polisi harakaharaka wakati viongozi fulani wa CCM wamekuwa wakipanda kwenye majukwaa wakiwatukana wapinzani wao kwa matusi yenye kashfa tupu na hawakuchukuliwa hatua zozote, si za kisheria au hata za kukemewa na viongozi wakuu wa chama chao si huko Zanzibar wala si Dodoma.

Wakereketwa wenginewa CCM wamekuwa wakisema wazi kwamba Wapemba waondoke Unguja na warudi kwao Pemba, wakisahau kama Rais Ali Mohamed Shein na wakereketwa kadhaa wengine wa CCM nao ni Wapemba.

Hao wanaotaka Wapemba wafukuzwe Unguja nao pia hawakuchunguzwa wala kukemewa na viongozi wakuu wa CCM. Wala polisi hawakuwachukulia hatua yoyote ilhali matamshi kama hayo yanaweza kusababisha mfarakano mkubwa katika jamii na hata mauaji ya kimbari.

Huu sio tena wakati wa kutishana. Wala si wakati wa viongozi wa serikali kujaribu kuzipima nguvu zao. Kiongozi yeyote yule anayefanya hivyo anakuwa kama mtu anayekikabili kioo akiwa amefunga macho eti ili aweze kujiona anakuwaje anapolala.

Chanzo: Raia mwema
 
Hicho ndo chanzo cha kutaka kura ya wazi. Ili wote wanaounga mkono rasimu hii washughulikiwe, hasa wale wa kutoka Zenj.
 
Ngoja nikajiridhishe kama haya aliyoyaandika huyu Ahmed ni sahihi kabla sijaandika mengi..

Ahmed anasema "Kuwashughulikia" maana yake ni kuwachukulia hatua zisizopendeza kama vile kuwatia ndani, kuwatesa au kuwafanyia mambo mengine ya kukirihisha.......

hii tafsiri sijui kaitoa wapi? kwa nini hakudhania kuwa kuwashughuikia maana yake kuhakikisha anawafikisha kwenye vyombo vya sheria?
 
Haiji, ingekuwa kama utakavyo ni simpy angesema watachukuliwa hatua za kisheria.
 
Viongozi bado wanadhani wananchi wa leo ni wale wa miaka ya 80. Kuna walioamka na kujua nchi sio ya viongozi lakini bado viongozi hawalijui hili, wamelewa madaraka
 
Haiji, ingekuwa kama utakavyo ni simpy angesema watachukuliwa hatua za kisheria.

Faiza, kauli ya karibu na "Kumshughulikia" ni kama kusema "kukabiliana nae au nao" au kwa lugha za wenzetu "Deal with"... kauli hii haina maana hizo tu ambazo ahmed anataka watu waamini kama kutesa, kutia ndani n.k.......

Kauli kama hii inapotolewa na watu walio na mamlaka za kidola huwa inatafsifiwa mara nyingi kama jitihada za kuhakikisha sheria inafuata mkondo wake na kutimiza wajibu wa kisheria kutokana na watu kukiuka au kwenda kinyume na sheria.......
 
Muktadha ni watu "wanaotaka muungano wa serikali tatu", sasa hao wanaenda kinyume na sheria ipi? ni kutishana tu hakuna zaidi, hata utetee vipi.
 
Ngoja nikajiridhishe kama haya aliyoyaandika huyu Ahmed ni sahihi kabla sijaandika mengi..

Ahmed anasema "Kuwashughulikia" maana yake ni kuwachukulia hatua zisizopendeza kama vile kuwatia ndani, kuwatesa au kuwafanyia mambo mengine ya kukirihisha.......

hii tafsiri sijui kaitoa wapi? kwa nini hakudhania kuwa kuwashughuikia maana yake kuhakikisha anawafikisha kwenye vyombo vya sheria?

Wewe uko Marekani? kwani wale waliowahi kungolewa kucha vyombo vya sharia havikuwepo?
 
Cuf na mbinu zao chafu hawataweza kuichafua zanzibar kwa namna yoyote ile.
 
cuf na mbinu zao chafu hawataweza kuichafua zanzibar kwa namna yoyote ile.

Nawaomba waelewa wa protokali za zanzibar hasa kuhusu vyeo na madaraka (siniority) kati ya Maalim Shariff Hamad na Balozi Seif Idd. Nashindwa kuamini kama makamu wa pili anauwezo wa kimamlaka ya kumkemea makamu wa kwanza wa rais hadharani.
 
Muktadha ni watu "wanaotaka muungano wa serikali tatu", sasa hao wanaenda kinyume na sheria ipi? ni kutishana tu hakuna zaidi, hata utetee vipi.
Ukhti FaizaFoxy kwani wewe ni muumini wa serikali ngapi? Ijumaa kareem.
 
Faizafoxy ni muumin wa serikali tatu kwa jinsi anavomshughulikia hilo liccm
 
Ngoja nikajiridhishe kama haya aliyoyaandika huyu Ahmed ni sahihi kabla sijaandika mengi..

Ahmed anasema “Kuwashughulikia” maana yake ni kuwachukulia hatua zisizopendeza kama vile kuwatia ndani, kuwatesa au kuwafanyia mambo mengine ya kukirihisha.......

hii tafsiri sijui kaitoa wapi? kwa nini hakudhania kuwa kuwashughuikia maana yake kuhakikisha anawafikisha kwenye vyombo vya sheria?

Nakubaliana na Ahmed kwa alichokiandika kuwa "Kuwashughulikia"ni kuchukua hatua zisizopendeza,angesema watachukuliwa hatua za kisheria ingejulikana watapelekwa mahakamani ili kosa lao lijulikane.
 
Ngoja nikajiridhishe kama haya aliyoyaandika huyu Ahmed ni sahihi kabla sijaandika mengi..

Ahmed anasema “Kuwashughulikia” maana yake ni kuwachukulia hatua zisizopendeza kama vile kuwatia ndani, kuwatesa au kuwafanyia mambo mengine ya kukirihisha.......

hii tafsiri sijui kaitoa wapi? kwa nini hakudhania kuwa kuwashughuikia maana yake kuhakikisha anawafikisha kwenye vyombo vya sheria?

Unajua Zanzibar waandishi wa habari wakongwe wote ni PRO wa vyama vya siasa.
Ahmed Rajab, Hassan Khamis, Ali Saleh , pia akiambatana na huyu wa sasa wa Gazeti la Mwananchi Salma Said hao wote ni mfano wao!
So sio jambo la kushangaza kusikia akitoa tafsiri kama vile Kiswahili ni Lugha ya Family yake tu.
Ni sawa na huku Bara watu wanavolalamika waandishi wa habari wa magazet ya CCM.
Nimeshangaa pia kwamba analinganisha matusi Vs na kutishiwa mtu usalama wa maisha yake!
 
Nawaomba waelewa wa protokali za zanzibar hasa kuhusu vyeo na madaraka (siniority) kati ya Maalim Shariff Hamad na Balozi Seif Idd. Nashindwa kuamini kama makamu wa pili anauwezo wa kimamlaka ya kumkemea makamu wa kwanza wa rais hadharani.

Hee Sugu Mbunge anamkashifu rais wa Jamhuri.
Au hujawahi kusikia CUF wakati wa Amani Karume wakimkashifu katika majukwaa ?
ukiingia katika siasa jiandae hata kutukanwa na mtoto.
 
wazungu na masheikh wakitiwa Tindikali wazenji wanasema ni wabara ndio wanachafua utalii ila hapo leo kumeshaonesha mwanga kama wazenji wenyewe ndio hushiriki haya matendo.
 
Ahsantum Ahali yangu Ahmed Rajab kwa bayana zako. Lakin tuamini tu kuwa HAKUNA BATWIL YENYE KUSHINDA HAKI.

Nafikiri Balozi Idi anayaona huko Dodoma katika kamati za Bunge la katiba mpya. Kwani 2/3 majority kuhusu Ibara ya 1 na 6 vya rasimu ya katiba hususan vile vinavyokhusu aina na muundo wa Muungano, kutoka upande wa Znz haipatikani hivyo kuacha swali zito hapo.

Mbommbo Ngafu mwaka huu.

Tumpe Pole Balizi Idi
 
Ukhti FaizaFoxy kwani wewe ni muumini wa serikali ngapi? Ijumaa kareem.

Mimi nnapendelea kila nchi iwe na himaya yake kamili, kila mmoja afahamu mipaka yake, utaifa wake, uzalendo wake, haki zake, mapato yake, tamaduni zake. Si kulazimishana.

Ningependelea Serikali mbili zenye mkataba wa Muungano.
 
Mimi nnapendelea kila nchi iwe na himaya yake kamili, kila mmoja afahamu mipaka yake, utaifa wake, uzalendo wake, haki zake, mapato yake, tamaduni zake. Si kulazimishana.

Ningependela Serikali mbili zenye mkataba wa Muungano.
Ok vizuri sana ukhti sasa hapo si utakuwa kinyume na chama chako? Kwa hiyo hoja yako ni muungano wa mkataba kama wa Maalim au sio?
 
Back
Top Bottom