Nani alimtosa Samwel Sitta?

assadsyria3

JF-Expert Member
Apr 9, 2013
6,904
4,050
WIKI iliyopita, Mzee Samuel Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo na Waziri katika serikali yetu, aliongea kupitia televisheni ya ITV kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisiasa katika taifa letu. Mzee Sitta ndiye alikuwa Spika wa Bunge la tisa kabla hajatoswa katika mazingira ya kisiasa yanayoendelea kuhojiwa na wengi, akiwamo yeye mwenyewe.

Kutoswa kwake katika kinyang'anyiro cha nafasi ya spika kinatafsiriwa na wengi kuwa ni "kuvuna alichopanda" yeye mwenyewe akiwa Spika. Mahasimu wake na baadhi ya wapenzi wake kisiasa wanamwona kuwa alishiriki fitna kwa utawala wa Kikwete na kuiangusha serikali hiyo kisha akawageuka wananchi na kuzima cheche za mabadiliko zilizoanza kuchomoza bungeni.

Sitta anaonekana hakuishia hapo bali aliligeuka kundi lake pale anapodaiwa kushiriki kuasisi Chama Cha Jamii (CCJ) na kisha kuwageuka pale alipodanganywa na Kikwete kwenda kuzindua ofisi yake kule Urambo.

Msururu wa usaliti wa Sitta haukuishia hapo, baada ya kutoswa yasemekana aliwatosa CHADEMA waliokuwa na makubaliano naye ili kumfanya awe mgombea urais wao.

Hata baada ya kuongea na kufafanua masuala mbalimbali, Mzee Sitta hajafanikiwa kushawishi upande wowote wa kisiasa. Bado anaonekana ni muasi ndani ya serikali, msaliti wa wanaharakati za kupinga ufisadi ndani ya CCM, na mtu asiyeaminika kwa vyama vya upinzani.

Nimeamua kuirejea makala niliyoandika wakati Samuel Sitta ametoswa katika nafasi ya Uspika. Kwa maoni yangu, makala ile bado ina uzito wa kumjibu Samuel Sitta ili afanye uamuzi wa busara katika siasa za siku za usoni. Endelea…

Kwa mara nyingine tena wingu zito jeusi limetanda juu ya Dodoma. Uchaguzi wa Spika umedhihirisha kwa mara nyingine kuwa mafisadi wana nguvu ndani ya CCM na yeyote anayebishia ukweli huu asubiri tena kwa pigo jingine la nguvu.

Samuel Sitta aliyechaguliwa kuwa Spika baada ya uchaguzi wa 2005, aliondolewa ghafla katika kinyanganyiro cha uspika kwa kile kilichodaiwa kuwaachia akina mama kuongoza mhimili huo wa dola.

Haitakaa iingie akilini kuwa hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kweli kwa kuwa vikao vitatu vilivyopita vya Kamati Kuu ya CCM havikuongelea suala hili la jinsia. Suala hili liliundwa ghafla siku chache kabla ya kwenda Dodoma, na kama nilivyojadili wiki iliyopita, kundi la mafisadi walimtanguliza Chenge ili kuongeza mpasuko ndani ya CCM ili kujenga mazingira ya kuwaondoa wote Chenge na Sitta katika kinyanganyiro cha uspika.

Kwa kuhisi hilo limebainika mapema mno kabla halijatokea, ndipo wakaja na kisingizio cha jinsia. Kwa bahati mbaya, pigo la hivi karibuni dhidi ya Samuel Sitta, ni pigo kwa CCM kuliko lilivyo pigo kwa Samuel Sitta.

Ni pigo kwa CCM kwa sababu sasa ufisadi ni sera iliyo na isiyo rasmi ya CCM. Unapomuondoa mtu kwenye madaraka kwa sababu tu, "aliendekeza mno mijadala ya ufisadi bungeni", ni wazi kuwa ufisadi si suala la kuongelewa ndani ya CCM.

Kwa chama kinachobeba neno "Mapinduzi" katika jina lake, uamuzi huu ni pigo kwa CCM. Uamuzi huu pia unamweka Samuel Sitta katika mgogoro mkubwa kiuamuzi. Inabidi ama akubali kuwa alikosea kupinga ufisadi katika chama kinachokumbatia ufisadi na kwa jinsi hiyo abaki ndani ya chama hicho, au ashikilie msimamo wake kuwa anapinga ufisadi na aondoke katika chama kinachokumbatia ufisadi. Lakini pia Sitta ajue ana mtaji mkubwa nje ya CCM na uamuzi wa kubaki ndani ya CCM ni kuula huo mtaji; ni sawa na mkulima kula mbegu.

Kwa kuwa hilo limetokea na kwa kuwa maisha ya siasa lazima yasonge mbele, ni vema basi tukachambua kwa makini ni nani hasa alimtosa Samuel Sitta, Spika wa Bunge la tisa, aliyejibainisha kuwa mtetezi wa maslahi ya taifa.

Orodha ya wanaoweza kuwa walimtosa au kuchangia kutoswa kwake ni ndefu. Kuna chama chake - CCM, kuna mafisadi, kuna Jakaya Kikwete, kuna ‘makamanda' wa kupinga ufisadi, kuna Bunge, kuna Anne Makinda, na mwisho wa orodha yuko mwenyewe Samuel Sitta. Nitaeleza kila mmoja na kila kundi.

Kwanza, CCM ilimtosa Sitta

Ndicho chama chenye dhamana ya kumsimamisha kugombea nafasi ya uspika. Safari hii CCM ilimkataa Sitta na sababu si jinsia bali ilimwona kama mchawi aliyesababisha mpasuko uliokifanya chama kikose majimbo na kushuka kwa kasi katika kukubaliwa na wapiga kura.

Badala ya kumwona Sitta kama mtaji wa kukijengea heshima mbele ya jamii, kilimwona ni tishio-kikamtosa. Mbele ya safari kitagundua muda si mrefu kuwa hakikumtosa Sitta, bali kilijitosa chenyewe na kuwatosa Watanzania wengi wanaoteseka katika lindi la umaskini unaosababishwa kwa sehemu kubwa na ufisadi uliozagaa ndani ya nchi.

Pili, Mafisadi walimtosa Sitta

Mafisadi walimtosa Sitta kama inavyodaiwa kuwa aliwatosa katika kashfa ya Richmond. Mtu mmoja ameniambia kuwa majeruhi wote wa Richmond hawatakaa wamsamehe Sitta. Watapigana mpaka watakapoliona kaburi la Sitta.

Siyo kaburi la kisiasa kwa sababu hilo sasa linaonekana wazi, bali kaburi halisi la mauti yake. Safari hii walimwandaa fisadi mwenzao agombee ili kama akipita awasafishe, lakini kama fisadi hakupita na Sitta asipite.

Wameshinda maana Sitta siyo Spika. Ni mbunge na ataanza kujifunza kuomba mwongozo wa Spika kama wao. Huu ni ukurasa mwingine wa siasa za visasi unaoendelea kukitafuna chama cha Mapinduzi.

Siyo Sitta peke yake anayetafutwa na mafisadi. Wako wengi na wanajulikana. Serikali ya mafisadi watupu iko inaandaliwa na inafanyiwa kazi katika kila uchaguzi na kila uamuzi unaofanywa na serikali iliyo madarakani.

Mafisadi sasa wana wabunge (tena wengi), wana Ma-DC, RC, DED's, makatibu wa wakuu, wana usalama na makada mbalimbali wa CCM kila ngazi. Hawa kwa ujumla wao na kwa jina la mafisadi, walimtosa Sitta. Baadhi yao wameendelea kuandika taarifa za uzushi na kuzisimamia kwenye chama na serikali zikimwonyesha Sitta kuwa ni adui wa taifa.

Tatu, Kikwete alimtosa Sitta

Jakaya Kikwete alimtosa Sitta kwa njia nyingi. Kwanza kwa muda mrefu amekuwa na lugha mbili kuhusu Sitta na wenzake. Akikutana nao anawapa nguvu na kuwahakikishia kuwa yuko nao katika mapambano dhidi ya ufisadi. Lakini akikutana na mafisadi anawahakikishia kuwa yuko nao na wakati mwingine kuwaomba wamletee mapendekezo ya namna ya kumaliza masuala kadhaa.

Baadhi yetu tumeendelea kushangaa pale tunapoona taarifa zikiandaliwa katika ofisi binafsi za mafisadi na baada ya muda mfupi zinatoka kama taarifa maalumu za serikali. Ikulu sasa ina ofisi ndogo mitaani, kwenye internet café, kwenye laundry rooms, legal chambers, press rooms na hata katika ofisi za biashara.

Msimamo wa Jakaya ulikuwa muhimu katika kumtosa au kumwokoa Sitta. Akiwa mmoja wa viongozi wa mhimili wa dola, Sitta alipaswa kukutana na Jakaya kabla hata ya kuchukua fomu ya kugombea.

Lakini Jakaya alimwacha huku akijua kile kitakachotokea Dodoma. Kama kawaida, baada ya kumtosa akatumia wana usalama kumchelewesha Sitta asifanye uamuzi wa kukiumiza chama.

Iliposhindikana alikutana naye mwenyewe na kumpa ahadi lukuki za kumfanya achelewe kufanya uamuzi. Kwa maoni yangu, Jakaya anamwandaa Sitta kwa pigo la mwisho litakalompeleka mwisho wa safari yake kisiasa na hata kimaisha.

Nne, makamanda wa ufisadi

Wale "makamanda" wa kupinga ufisadi bungeni, walio wazi na wale wa siri – wote walimtosa Sitta. Hawa ndio waliokuwa mtaji mkubwa wa umaarufu wa Sitta bungeni.

Ilitarajiwa watasimama na shujaa wao Sitta ili kulinda ajenda ya kupinga ufisadi lakini walishindwa hata bila kujitetea kwa dakika moja. Walimchochea Sitta aondoke kwenye CCM, lakini hao hao wakaenda kwenye kamati ya wabunge wa CCM na kummwagia kura na sifa nyingi Spika mpya, Anne Makinda.

Ikiwa kweli walikuwa na Sitta, walipaswa kupiga kura ya kutopiga kura (abstention). Hii si kura ya kumkataa Makinda, bali kura ya kukataa uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM. Walishindwa na kwa hiyo wakamtosa Sitta.

Hawawezi tena kusimama na kusema wanampenda Sitta na wanampenda Anne Makinda. Na zaidi hawawezi tena kuaminika ndani ya chama kuwa ni waaminifu. Sitta amemaliza zamu yake, kisu kikali kinawasubiri wao. Wajiulize Seleli, Kimaro, Shelukindo na Mpesya wako wapi?

Wao hao wamekwenda, zimebaki sifa zao. Kwa mara nyingine, makamanda hawa wamejionyesha kwamba ajenda ya kupinga ufisadi si yao, waiachie CHADEMA, wakae kimya na wawe wapole ili wanyolewe manyoya bila maji moto.

Tano, Anne Makinda

Anna Makinda namtilia shaka kuwa ni mmoja wa waliomtosa Sitta. Katika Bunge lililopita, huyu alikuwa Naibu wa Spika Sitta. Kikazi na kimaisha walikuwa karibu na hata ajenda ya kupinga ufisadi walishirikiana.

Uamuzi wake wa kuchukua fomu sambamba na ‘bosi' wake unanifanya ninuse mpango mchafu nyuma ya uamuzi huo na kuhisi mikono mirefu ya mafisadi ilifika Njombe. Kwa kuwa CCM hudai kuwa na utaratibu wa kuachiana nafasi, Makinda alipaswa kumwachia Sitta kwa kipindi angalau kimoja tu.

Anaweza kudai ni demokrasia, lakini wenye mashaka tutahoji hiyo demokrasia mbona haikutumika katika kumtafuta Rais, na haijatumika kwa kumtafuta Naibu Spika pale muda ulipoongezwa ili kumnyima nafasi, Jenesta Mhangama?

Sura halisi ya Makinda imejitokeza pale alipodai hajui nini maana ya ufisadi zaidi ya kuchukua mke wa mtu. Hata kwa maana hii mpya ya ufisadi anayoing'ang'ania Makinda, bado CCM inao mafisadi wengi wanaochukua wake na waume za watu na Makinda anawafahamu vizuri. Haijalishi wanawachukua wake au waume za watu kwa saa, usiku mmoja au moja kwa moja.

Mwisho, Sitta alijitosa mwenyewe

Tangu alipoamua kupambana na ufisadi alipaswa kujua kuwa anapambana na mfumo wa chama kinachomlisha. Katika hali ya kawaida si rahisi kuukata mkono unaokulisha.

Joto la mashambulizi yake lilipofikia hatua mbaya, alilazimika kulipunguza kwa kasi ya ajabu. Hali hii iliwaaacha wafuasi wake wa ndani na nje ya bunge katika mashaka makubwa kuhusu misimamo yake.

Lakini pia, nafasi hii iliwapa mafisadi nafasi ya kumshughulikia bila yeye kuwa na mtetezi wa kweli. Katika masuala ya kupambana na ufisadi ni hatari kuchelewa kufanya uamuzi. Ufisadi una utamu wake na hasa kama unafanywa na mfumo tawala.

Mfumo unampa ulinzi, marupurupu, heshima ya kiitifaki, na maisha bandia mengine mengi. Ili kupambana nao, inabidi mpambanaji akubali kuyapoteza haya kwa muda. Sitta anaelekea kuchelewa kufanya uamuzi. Ahadi anazopewa zitamfunga hata kama akizipata na zitamfanya awe mfungwa wa kudumu kwa dhamiri yake na maisha mazima.

Kwa maana nyingine ni kuwa Samuel Sitta anapodai mafisadi ndio waliomtosa katika kinyanganyiro cha uspika ama amechanganyikiwa au anachelewa tu kuelewa kuwa mafisadi ni wale tu wachache anaowataja, bali ni chama kizima cha CCM akiwamo yeye mwenyewe. Kwa maana hii ya pili, Sitta kama fisadi wa kimfumo alijitosa mwenyewe katika kinyanganyiro hicho.
 
yaani makala ndefu yote hii unamzungumzia mtu. no wonder bongo bado ni maskini
 
Kwenye nini? Open up? Na kama kuna kutosa atakuwa amejitosa mwenyewe kwa unafiki wake.

Sent from my BlackBerry 9860 using JamiiForums
 
Halafu kunastory alivokua mkuu wa mkoa wa iringa miaka ya nyuma aliwahi kufumaniwa akiwa na mwanamke mwingne hotelini hapo iringa. Fumaniz hlo lilifanywa na mkewe
 
Mimi naamini Sitta alijitosa mwenyewe kwa kutojua mtandao wa ufisadi kwamba unaanzia "penyewe"! Ule ujumbe wa dakika 3 alioutoa baada ya hotuba ya SAKATA LA EPA pale bungeni, ili"mdhalilisha mkuu" akamweka kwenye target....!Sitta alionesha udhaifu kwa kukubali kuwa waziri wakati aliyemtosa kwenye u-spika kwa kisingizio cha nafasi kwa wanawake, akiwa mtoa cheo a.k.a kipozeo! Sitta bwana!
 
Sitta ni mnafiki mwizi na fedhuli...kajenga kwzo ofisi ya spika ya 3bilioni...who told him kuwa atakuwa spika milele....this guy is rotten nashangaa sana anapojiita mpambanaji...hawara yake kinondoni anahudumiwa na magari ya serikali by the time yeye spika bado anabwabwaja hapa eti anapambna....akae kimya bana
 
Hata baada ya kumtosa uspika wakaona ili kummaliza kabisa wampatie uwaziri wa africa mashariki siyo kwa kumpooza ila kwa makusudi ili asitoke kwenye kundi la mafisadi ili kiwe kigezo cha kumtosa uraisi SITA na wenzake anaotaka kushirikiana nao kwenye mbio za kutafuta uraisi wote ni mafisadi na CCM walishasoma alama za nyakati kama huyu sita atakuja kutaka kugombea uraisi ndio maana wakaona na yeye pamoja na kundi lake wawaingize kwenye kundi hilo la mafisadi
 
sitta ni zaidi ya mnafiki,juzi walikataza kujinadi yeyekataja list ya kujiaanda na Urais kwa kigezocha upambanaji, we muache tu aje kukutana na mamvi ndio haaujua mji
 
Halafu kunastory alivokua mkuu wa mkoa wa iringa miaka ya nyuma aliwahi kufumaniwa akiwa na mwanamke mwingne hotelini hapo iringa. Fumaniz hlo lilifanywa na mkewe

Ikiwa huna la kuchangia hapa, ni heri ungekaa kimya mzee!
 
Mtoa uzi nakupa tano ;Uchambuzi wako au hoja zako zimetulia nashauri mzee asome kwa makini ili ajipime na kuchukua hatua kabla ya 2015.
 
Alafu siku hizi kule bungeni hawampi tena nafasi ya kukaimu ikiwa waziri mkuu hayupo! siku hizi wanampa Shamsi nohodha! Lazima ateseke!
 
Back
Top Bottom