Kesi yake hii hapa ...
JALADA la kesi inayomkabili mwandishi wa habari wa magazeti ya Nipashe na The Guardian,
Mwinyi Sadallah, limerejeshwa kwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mjini Mgharibi, Said Marekano.
Mwendesha Mashitaka katika kesi hiyo, Mgeni Jailan, jana aliomba mahakama iahirisha kesi hiyo, kwa vile jalada la kesi hiyo bado halijarejeshwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kutoka kwa Mkuu huyo wa Upelelezi mkoa.
Akijibu ombi hilo, wakili wa Sadallah, Hamid Mbwezeleni, alimwomba hakimu kupanga kesi hiyo kwa kuzingatia muda muafaka.
Baada ya kupokea maombi hayo, hakimu Rabia Hussein Mohammed aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 24, mwaka huu.
Mwandishi huyo amefunguliwa mashitaka pamoja na mkulima Ramadhan Mohammed Vuai, mkazi wa Kijiji cha Chwaka, Wilaya ya Kati Unguja.
Katika kesi hiyo, Sadallah, mshitakiwa namba moja, anatuhumiwa kuandika habari za uongo na kumkashifu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Amani Abeid Karume.
Watuhumiwa hao wako nje kwa dhamana ya sh 300,000 kila mmoja na wadhamini wawili kwa kiwango kama hicho cha fedha kwa maandishi.
Inadaiwa kuwa Sadallah alitenda kosa hilo Septemba 22 na 24, mwaka jana, kinyume na kifungu cha 48 (1) (c) na kifungu cha 47 (1) (a) cha sheria ya usajili wa mawakala wa habari, Magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988.
Kwa upande wake, anakabiliwa na shitaka la kutoa maneno ya uchochezi kinyume na kifungu cha 48 (1) (b) na 47 (1) (a) cha sheria ya usajili wa mawakala wa habari, magazeti na vitabu namba 5 ya mwaka 1988. Watuhumiwa wote walikana mashitaka yao.