Kuna mchakato umeanzishwa kuelekea kuandikwa kwa Katiba mpya. Kama tujuavyo, tayari kuna Rasimu ya Katiba hiyo mpya. Moja ya maeneo yaliyovuta hisia za Watanzania wengi ni muundo wa Muungano wa Serikali Tatu. Mimi niko mbali kidogo na nyumbani kwa hivi sasa. Hivyo, siwezi kutoa maoni yangu katika Mabaraza. Kwa ikhsani ya wanachama wa Jukwaa hili naomba niseme YA KWANGU hapa. Kwa kweli naona dalili za wazi za kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania endapo suala la Serikali Tatu litakubalika na kutekelezwa! Huu si uwanja ninaoweza kuutumia kusema mengi sana. Lakini Muungano unaofaa na wenye SALAMA kwetu ni huu wa sasa wa Serikali mbili au wa Serikali moja. Kwa sababu zinazoeleweka na wengi, hadi sasa Muungano wa Serikali Moja haujawezekana. Lakini tayari tumekuwa ndani ya Muungano wa Serikali mbili kwa miaka 49 sasa--umri wa mtu! Mamilioni ya wananchi wamezaliwa ndani ya Muungano huu wa Serikali mbili uliozaa nchi inayoitwa Tanzania. Kwa maana hiyo hao wote ni Watanzania. Ni watu wachache sana miongoni mwa hao, wakiwemo wale wa Visiwani wanaoweza kujiepusha na Utanzania. Kwa maana hiyo, mamilioni hao wamekuwa, na wanajitambulisha Watanzania popote walipo--wameshazoea! Wao na watoto wao na vitukuu vyao wanajitambulisha Watanzania. Siioni mantiki ya moja kwa moja na yenye mashiko ya kuondokana na utambulisho huu na mazoea haya kwa sababu tu ya tamaa za baadhi ya watu wachache kupenda madaraka. Hata Dunia imeshatuzoea hivyo kuwa sisi ni Watanzania. Tuna viti Addis Ababa na New York vinavyoiwakilisha nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama kumekuwa na matatizo katika Muungano uliopo suluhisho sio kuvunja Muungano. Ni kutafuta kwa dhati majawabu ya matatizo hayo bila kuuathiri Muungano uliopo. Hakuna ubaya wa kuandika Katiba Mpya. Lakini pia hakuna mantiki nzito ya kuanzisha Muungano wa Serikali Tatu--labda kama tumeamua kuuvunja Muungano wenyewe kabisa! Mwalimu aliwahi kuuliza na sisi tunamtafuta Goberchev wetu? Yaani tunamtafuta Rais atakayeporomoka na hiyo itakayokuwa Serikali Ya Muungano (ndani ya muungano wa serikali tatu)? Kila upande ukishakuwa na Serikali yake, nani ataijali mno hiyo Serikali ya Muungano? Katika hali hiyo, hatima ya serikali hiyo inayoning'inia ni nini? Nina wasiwasi, JK asijeingia katika vitabu vya historia ya Dunia kwa kuanzisha mchakato uliosababisha kuvunjika kwa Muungano wa Tanzania! Samahani wadau kwa kuingia na post yenye kuchosha, lakini kama nilivyosema awali, nimelazimika! Hodi!!