Naifananisha CCM na mnara wa Babeli | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Naifananisha CCM na mnara wa Babeli

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by dosama, Jun 3, 2012.

 1. dosama

  dosama JF-Expert Member

  #1
  Jun 3, 2012
  Joined: Dec 25, 2010
  Messages: 786
  Likes Received: 12
  Trophy Points: 35
  “NCHI yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.” (Mwa. 11:1). Mwanzoni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilikuwa chama pekee cha siasa. Kilitapakaa nchi nzima na watu waliimba wimbo mmoja: ‘Kidumu Chama Cha Mapinduzi, Zidumu fikra za Mwenyekiti.’

  Hivi sasa watu hatuimbi tena wimbo huo kwani neno ‘kidumu’ limegeuka kuwa ‘Kigumu’ na hivyo wimbo huimbwa: ‘Kigumu Chama Cha Mapinduzi!’ Ndiyo, ni kigumu kwani sasa matajiri wamekishika vilivyo wakisaidiwa na viongozi mafisadi wanaoimba kijamaa na kucheza kibepari. Hata walioachishwa uwaziri wanapita wakilalama kuwa wameonewa. Wamesahau kuwa cheo ni dhamana.

  “Ikawa watu waliposafiri pande za Mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko, Wakaambiana, ‘haya na tufanye matofali tukayachome moto.’” Baada ya CCM kuenea nchi nzima, viongozi wakalewa madaraka wakisema ‘chama kimeshika hatamu,’ hivyo kikajitwalia viwanja vyote vya michezo na maeneo ya wazi kwa manufaa yake.

  CCM kikawatumia wanafunzi wa elimu ya juu kufungua matawi yake vyuoni. Ili kuhodhi madaraka yote, chama kikaanzisha ‘mkoa wa majeshi.’ Wakati ule asiyekuwa mwanachama wa CCM hakupata ajira katika jeshi lolote – Mgambo, JKT, Polisi wala JWTZ. Hata wafanyakazi wa serikali na mashirika ya umma walitakiwa kuwa makada wa chama. Hivi sasa CHADEMA wanalaumiwa kwa kuingiza siasa vyuoni na wahadhiri wanakatazwa kujiingiza katika siasa. Ama kweli chongo kwa Mnyamwezi, kwa Mswahili amri ya Mungu!

  Wakasema, “Haya na tujijengee mji, na mnara na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.” (Mwa. 11:4). CCM kikajitanua kwa mapana na marefu kikijitwalia fedha na mikopo kutoka benki za wananchi, na mpaka leo hazijarejeshwa. Matokeo yake mashirika ya umma yamekufa baada ya kufilisika. Machache yaliyobaki yanajikongoja.

  “Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. Bwana akasema, ‘tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao, ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.’ Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji” (Mwa. 11:5-8).

  Wananchi walipoona CCM kinakwenda arijojo (uendaji usio na mwelekeo mwafaka kwa kukosa kuongozwa au kupangiliwa vizuri) wakashitukia wanakopelekwa siko. Nahodha wake, Mwalimu Nyerere alikwishang’atuka na waliobaki wakaona kang’atuka na hekima zake. Wakaona mtu aliyekuwa ‘kikwazo’ kwao, sasa hayupo, hivyo wakalizika Azimio la Arusha na kuja na Azimio la Zanzibar, lililowapa viongozi ‘ruksa’ ya kufanya biashara.

  Walioona mambo yanakwenda mrama, wakaamua kujiondoa taratibu na kuunda upinzani ambao baadaye, kwa shinikizo la kimataifa, ‘ukaruhusiwa’ kwa shingo upande. Wapinzani wakapewa majina mengi: wachochezi, waroho wa madaraka, wasiokuwa na sera na kila jina baya, ili kuwakatisha tamaa na kuwaogofya wananchi waliojiunga na waliotaka kujiunga nao.

  Pamoja na vigaviga (sumbua mtu na kumkosesha raha, hangaisha mtu, tia mtu wasiwasi) hizo, wananchi wakasema liwalo na liwe, wakaanza kukitosa CCM na sasa mambo ni magumu mno. Makada na viongozi wake wanakikimbia kwa maelfu kujiunga na vyama vya upinzani kikiwemo CHADEMA wanachoamini kuwa mkombozi wa wananchi walionyanyasika kwa miongo kadhaa.

  Kama ilivyokuwa kutoelewana lugha katika ujenzi wa mnara wa Babeli, ndivyo viongozi wa CCM wasivyoelewana sasa. Wanalaumiana wenyewe kwa wenyewe, wanatafutana kwa heri na shari, wanalumbana, kusutana na kutishana. Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama anakiri waziwazi kuwepo mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho na kufananisha hali hiyo na kundi la G8 na NATO.

  Hali hiyo imesababisha makundi ndani ya chama kilichokuwa mkombozi na tegemeo la wananchi, lakini sasa kimejitenga na wanyonge na kuwakumbatia mafisadi!

  Makundi hayo ndiyo yanayokimomonyoa CCM siku baada ya siku kwa kukimbiwa na makada wake. Ndiyo yanayokuwa na makundi ya wanaowania uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ndiyo yanayoleta ukanda, ukabila na sasa udini wa wazi kwenye mihadhara ya kukashifu dini zingine. Wanasahau kuwa imani hailazimishwi kama ambavyo huwezi kumlazimisha punda kunywa maji.

  Uchomaji wa makanisa kule Zanzibar ni mfano dhahiri. Moja ya makala zangu katika gazeti hili niligusia tukio hilo na mmoja wa wasomaji akanitumia ujumbe mfupi usemao: “Vurugu za Zanzibar hazisukumwi na wanasiasa wala udini bali ufukara unaotesa vijana wengi. Vijana wasio na kazi wanaoshinda vijiweni bila kujua watakula nini. Wanaokosa makazi bora na kutembelea kandambili kwa kukosa cha kuvaa. Wametumia mwanya wa mjadala wa uamsho kuonesha hasira zao kwa watawala.

  “Hivyo kiini cha vurugu Zanzibar ni hali mbaya ya uchumi hasa rocketing inflation, ukosefu wa kazi kwa vijana na kukosa dira ya maisha kwa kutelekezwa; na watawala kutowawekea mipango ya maendeleo. Hamna mwanasiasa au kiongozi wa Uamsho aliyeamuru wachome magari au Makanisa. Ni ghadhabu za vijana kukosa kazi na mwelekeo wa maisha. Kukamata viongozi kulichochea tu. Tatizo ni ufukara (uchumi legelege) -- 0767 33 78 71.

  Nikamjibu: “Kama ni hivyo, Makanisa yanahusikaje? Mbona hawakuchoma Misikiti na ofisi za Serikali? Au Makanisa ndiyo yanayosababisha ugumu wa maisha? Tafakari kwa makini.” Hakujibu ujumbe wangu; labda baada ya kutafakari kwa makini, dhamira yake ikamsuta!Hata hivyo, Mkurugenzi wa Tanzania Islamic Peace Foundation (TIPF), Sheikh Sadik Godigodi anakanusha vurugu hizo kufanywa na vikundi vya wahuni, akisema ni wanachama wa kundi la Uamsho na kuitaka serikali kukichunguza kikundi hicho akisema kuwa hata kikundi cha Al-Shabab cha Somalia kilianza kwa mtindo huo.

  Swali muhimu: Hiyo iitwayo intelijensia ya polisi hufanya kazi Bara tu na si Visiwani? Au ni intelijensia maalumu dhidi ya vyama vya upinzani ili kuzuia maandamano yao ya amani ‘yawezayo kuzusha vurugu’ kama inavyodaiwa kila mara?

  Wahenga walisema mwanzo wa mkeka chane mbili. Methali hii yatukumbusha kwamba hatupaswi kuudharau mwanzo wa jambo lolote. Pia yatukumbusha kuwa kila jambo au kila tendo lina msingi wake. Serikali izinduke sasa na kufuatilia mwenendo wa kikundi cha Uamsho, vinginevyo yasijekuwa makubwa kama alivyohadharisha Sheikh Godigodi kwani lisemwalo lipo, kama halipo li njiani!
   
Loading...