Mzozo wa Sophia Simba watua Z'bar

Regia Mtema

R I P
Nov 21, 2009
2,970
864
Mzozo wa Sophia Simba watua Z'bar
• Makamu wake asema ni tishio UWT

na Mwandishi Wetu


amka2.gif

SAKATA la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), limechukua sura mpya, baada ya Mwenyekiti wa umoja huo, Sophia Simba, kuelezwa kuwa ni tishio, ndiyo maana amekuwa akipigwa vita na baadhi ya wanasiasa tangu kushika nafasi hiyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Makamu Mwenyekiti wa UWT Zanzibar, Asha Bakari Makame, kutokana na madai kuwa jumuiya hiyo inakabiliwa na mgogoro wa uongozi.
Sophia Simba ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), katika siku za hivi karibuni ametikisa anga za kisiasa, baada ya kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya wabunge wenzake kwenye kikao cha kamati ya Mzee Ali Hassan Mwinyi kilichofanyika mjini Dodoma.
Akizungumza jana, makamu mwenyekiti huyo alisema ndani ya jumuiya hiyo hakuna mgogoro wowote, kwa kuwa viongozi wake wamekuwa wakifanya kazi zao kama timu.
Hata hivyo, alisema mwenyekiti wa jumuiya hiyo ni mtu mwenye uwezo mkubwa kiutendaji, ndiyo maana kuna wanasiasa wanamuona tishio na kumuwekea mazingira ya kumpiga vita.
“Hakuna mgogoro wa viongozi isipokuwa kuna watu wameamua kumpiga vita mwenyekiti baada ya kuona ni kiongozi madhubuti na tishio kwao,” alisema Asha Bakari katika mkutano alioambatana na Naibu Katibu wake, Salama Aboud.
Hata hivyo, alionya kuwa mgawanyiko ya wabunge usiingizwe UWT, kwani kazi ya jumuiya hiyo ni kufanya kazi kwa masilahi ya wanawake, kwa kuzingatia misingi ya kudumisha amani na mshikamano kwa wananchi wake.
Aidha, makamu mwenyekiti huyo alisema kimsingi Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Husna Mwilima, hajafukuzwa nafasi yake na bado ni kiongozi wa jumuiya hiyo.
“Husna bado ni katibu mkuu wa jumuia na hao wanaosema kafukuzwa wanaeneza majungu, kwa vile ndani ya UWT hakuna mgogoro wowote wa uongozi,” alisema.
Alieleza kwamba katibu mkuu huyo kabla ya kuteuliwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Kikwete, jina lake lilipendekezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sophia Simba, hivyo haiwezekani sasa ampinge kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Alisema kilichotokea wakati wakiwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la Wanwake katika kikao kilichofanyika Dodoma, katibu mkuu alitakiwa kutoka katika kikao, ili kutoa nafasi ya kujadiliwa na wajumbe na hatua hiyo haikuwa kama ndiyo amefukuzwa.
“Hatua hii ilichukuliwa kama utaratibu wa jumuiya, kwa vile kuna mambo yalikuwa yameshaamuliwa katika vikao vya nyuma, lakini yalikuwa hajafanyiwa utekelezaji wake na yeye kama katibu mkuu alikuwa ndiye mtendaji wa hayo,” alisema Asha.
Hata hivyo, hakusema ni mambo gani ambayo hayakutekelezwa ambayo yalisababisha yajadiliwe, lakini alisema bahati mbaya, vyombo vya habari viiliacha mambo yaliyokuwa yakijadiliwa na baraza hilo na kuingiza mambo binafsi.
“Mimi na mwenyekiti tulifanya kazi kubwa ya kuhakikisha vikao vinatekeleza mambo yake kama yalivyopangwa, kwa vile baadhi ya wajumbe walikuwa na jazba walifikia kutuambia kuwa tuache kikao tukalale,” alisema.
Aidha, alisema Sophia Simba hana uwezo wa kumfukuza katibu bila ya kupitia taratibu za vikao na kuwataka wanachama wa jumuiya hiyo kuamini kuwa hakuna mgogoro ndani ya jumuiya hiyo.
Kuhusu tuhuma za kuliwa fedha za mkono wa pole kwa waathirika wa mabomu Mbagala, alisema madai hayo hayana msingi wowote, kwa vile wao kama viongozi wanaamini fedha hizo zilitumika vizuri, hasa kwa kuzingatia wahusika walikabidhiwa vifaa na si fedha.
“Wakati madai ya kuwapo kigogo kutafuna fedha UWT yanatokea, mwenyekiti alikuwa nje ya nchi, nikawasiliana naye kwa simu, lakini baada ya suala lenyewe kuliangalia linaonekana halina ukweli wowote,” alisema katibu mkuu huyo.
Hata hivyo, alimtaka katibu aondowe wasiwasi kwa vile tuhuma zilizokuwa zimetolewa hazikumtaja mhusika.
“Jumuiya ya wanawake wa Tanzania inatoa wito kwa wanachama wake pamoja na wananchi kwa ujumla kutobabaishwa na kuyumbishwa na watu wasioitakiwa mema jumuiya hii,” alisema makamu mwenyekiti huyo.
Katika mkutano huo, UWT imempongeza Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kwa hatua yake ya kumkaribisha Ikulu Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kuwasilisha msimamo wake kwa kukubali kumtambua kuwa ni rais halali wa Zanzibar na kuwapo kwake kumetokana na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.
“Hatua iliyofikiwa na Maalim Seif inafungua ukurasa mpya ndani ya demokrasia ya kweli na hivyo italeta maendeleo kwa Wazanzibari wote,” alisema Asha Bakari.
Hata hivyo, alisema suala la serikali ya mseto haliwezi kuamuliwa bila ya kuzingatiwa matakwa ya kikatiba, kwa kuwa suala hilo linahusu Katiba ya Muungano, Zanzibar na CCM.
Alisema kama viongozi wakiamua suala hilo bila baraka ya wananchi, viongozi wanaweza kupigwa mawe, kwa kuwa Zanzibar ni nchi ya mapinduzi.
“Hatuwezi tukasema iundwe serikali ya mseto, tutauliwa, kwa sababu hii nchi imepatikana kwa mapinduzi na kama tulivyosema, hatuwezi kuunda serikali hiyo mpaka tukamilishe taratibu,” alisema makamu mwenyekiti huyo. Hivi karibuni Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Amani Abeid Karume, alisema kwamba suala lolote linalohusu maamuzi ya Zanzibar ni lazima liamuliwe na wananchi, kwa kuwa viongozi kazi yao ni kujadili na si kutoa maamuzi ya mwisho. Kauli ya UWT imekuja kutokana na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuendelea kutetea kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar, kwa kuamini kuwa ndio ufumbuzi wa matatizo ya kisiasa ya Zanziabr.
 
Back
Top Bottom