Mzee Paschally Mayega na Rais wake...

Mzee Paschally Mayega na Rais wake...

Noti mpya tz

JF-Expert Member
Joined
Mar 23, 2011
Posts
974
Reaction score
247
RAIS wangu kuna wakati nilimtembelea mwanamwema Primus nyumbani kwake Kinyerezi. Alinisimulia hadithi ambayo nami leo naona nikusimulie.

Alianza: "Hapo zamani za kale alikuwapo mfalme aliyetawala nchi kubwa yenye utajiri wa kila aina na watu wachangamfu mahiri, waliojituma vilivyo katika kufanya kazi za ujenzi wa nchi yao! Alikuwa mwangavu wa kuonekana naye alijaa uso wa furaha na kicheko. Alipenda mizaha iliyomfanya aonekane kama mtu aongozaye bila dira wala mwelekeo! Hilo liliwafanya watu wake washindwe kumwelewa!

Raslimali za nchi zilitapakaa kila sehemu ya nchi. Kwa ajili ya utajiri huo wageni wa nchi za mbali walikuwa wanapishana kwenda kuuchota. Wananchi walipouliza kulikoni utitiri wa wageni, jibu lilikuwa rahisi tu, ‘Wawekezaji'. Wamekuja kutusaidia.

Utajiri uliotanda katika nyumba ya mfalme na kwa familia yake huku yeye na viongozi waliomzunguka wakiwaimbia wananchi wimbo wa kukariri wa nchi yetu ni maskini, ulichukuliwa na masikini hasa wa mashambani na vijana wa mjini walikosa kazi, kama kejeli kwao!

Ulifika wakati mfalme alipatwa na ugonjwa, akaumwa sana! Aliugua kwa muda mrefu bila kupona! Watu wake walijaribu kila dawa lakini hakuna hata mmoja iliyoonesha hata dalili za kumpatia mfalme nafuu. Nchi yote ilizizima kwa ugonjwa wa mfalme!

Hata matumaini ya mfalme kupona yalipoanza kutoweka katika nchi, wazee wenye busara na hekima kutoka pembe zote za nchi ile, walikusanyika na kutafakari kwa pamoja namna ya kupata dawa itakayookoa maisha ya mfalme. Ugonjwa ule mkubwa uliotishia kuyamaliza maisha ya mfalme, ulikuwa ni ugonjwa wa kukosa furaha! Mfalme alikosa furaha moyoni mwake.

Baada ya tafakuri ya muda mrefu wazee wakakubaliana kwa pamoja kuwa, kwakuwa mfalme anaumwa ugonjwa wa kukosa furaha, basi atafutwe mtu mwenye furaha katika nchi ile kisha avuliwe shati lake avishwe mfalme. Mfalme atapata furaha naye atapona!

Ikaundwa timu ya kuzunguka nchi nzima kumtafuta mtu mwenye furaha ili avuliwe shati akavishwe mfalme naye apate kupona!

Mtu wa kwanza waliyemfikiria alikuwa ni waziri mkuu. Walivutiwa na unyofu wake. Wakiangalia historia alikotokea mpaka kuwa pale walijua kuwa anapaswa kuwa na furaha kubwa, wakamwendea. Baada ya majadiliano, aliwajibu kwa unyenyekevu akisema: " Waungwana, mfalme amenitoa mbali nami kwa kupona kwake niko tayari kwa lolote hata kama ni kuutoa uhai wangu. Ukweli ni kwamba kabla ya kuupata wadhifa huu nilikuwa kipenzi cha watu nami nilikuwa na furaha! Wananchi na mimi kwa pamoja tulifanya mengi ya kumtukuza Mungu! Tukasoma maandiko katika kitabu kitakatifu kanisani kwa mapenzi kama wana wa Baba mmoja! Leo neno dogo tu, liwalo na liwe limenifanya niwe chukizo kubwa mbele ya Waja wa Mwenyezi Mungu!

Nilipoona kuwa tumechoka na sikuona namna nyingine yoyote ya kuwadhibiti wananchi isipokuwa ‘wapigwe tu', sikutarajia kuwa neno moja lingeweza kumzulia mtu gharika ya laana kwa maisha yake yote yaliyobakia katika ulimwengu huu wa mateso! Bado naingia nyumba za ibada lakini siwazi tena makuu ya Mungu niwapo Kanisani bali wingu zito lililotanda mbele yangu. Mkuu wangu wa kazi alipoombwa na waungwana aitengue kauli yangu hatarishi aligoma! Hakuitengua mpaka leo naburutwa mahakamani! Huja sikukidhi haja au matarajio yake! Misafara yangu sasa inazuiwa na wananchi wenye hasira! Silaha yao ni zomezomea! Baada ya kuanguka kwangu maisha yangu na familia yangu yatakuwaje huko mbele ya safari? Katika msongo wa mawazo kama huu, waungwana niambieni mtu ataipata wapi furaha? Mwambieni mfalme mashati ninayo lakini furaha sina kabisa!

Walipokwisha kuyasikia hayo hawakungoja zaidi. Wakamwendea katibu mkuu wa chama. Naye kwa unyenyekevu aliwaambia: "Waungwana, nimeaminiwa wadhifa mkubwa sana na chama changu lakini Mwenyekiti wangu ameniwekea vijana wakunisaidia, waliokwisha muda wao wa kuwatumika! Nikiwa nao nafanana na mti moja mrefu mahali pasipo na miti, nashindwa kufanya msitu! Nafanya kazi hii kwasababu naipenda nchi yangu, na namheshimu sana mfalme wangu lakini sina furaha kabisa katika kifua changu! Mwambieni Mfalme kuwa mashati ninayo lakini furaha sina kabisa!

Walipokwisha kuyasikia hayo wakaona wawaendee wafanyabiashara maarufu walioko nchini. Wakamwendea mmiliki wa makampuni mbalimbali yakiwamo ya vyombo vya habari, magazeti na vituo vya radio na televisheni! Alikuwa na viwanda vya kusindika maji, kutengeneza soda na hata migodi ya kuchimba madini. Mkwasi mkubwa lakini mtu aliyekuwa karibu na watu hasa maskini na wasiojiweza! Alikuwa na utayari wa kusaidia wakati wote. Mtu maarufu sana kwa wananchi wenzake na kwa watu wa mataifa. Leo akikutana na balozi huyu kesho anakuwa na balozi wa nchi nyingine! Wote wakienda ofisini kwake kwa mazungumzo na mashauriano baina ya nchi yake na nchi za nje.

Alimpenda sana Mfalme wake hivyo habari aliyopelekewa ilimsononesha sana hasa baada ya kugundua kuwa hawezi kumsaidia mfalme kupona! Akawaambia kwa unyenyekevu: "Waungwana, ni kweli Mwenyezi Mungu amenijalia mali ya kutosha. Sina sababu ya kujisifia kwa sababu wananchi wenzangu wananijua.

Lakini nina uchungu mwingi moyoni. Mwenyezi Mungu alipoitunuku nchi yetu kwa gesi nyingi kupindukia wengine tukadhani umaskini wa Watanzania Mungu amesema sasa basi. Waziri wetu mwenye dhamana aliwaambia wananchi kuwa itatengenezwa sera nzuri itakayompa mwananchi mzawa kipaumbele katika uvunaji wa raslimali hii. Ninapomwona anageuka sasa na kuwapa mgongo wananchi naye kuwakumbatia wageni kama wengine walivyofanya, nyongo hunikata ini.

Anawaambia wananchi eti uwezo wao ni wakutengeneza juisi tu labda na kusindika maji ya kunywa! Akutukanaye hakuchagulii tusi. Hajui kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha! Wengine tulikotoka tulilala pamoja na mbuzi! Lakini leo tumefikia mpaka kuanzisha tuzo ili kuwasaidia wengine waondokane na umasikini. Hao anaowakumbatia, Mungu hakujui kwao akawawekee gesi mpaka aje awawekee huku kwetu?

Na kama waziri anaumia kutokana na mafanikio yangu, uchungu wake asiusukumie kwa wananchi. Wananchi wana haki ya kushiriki katika kufaidi neema hii ya gesi waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Kwanini awakejeli wananchi wote kwa maneno ya dharau yanayofanana na kuwatukana? Ni lini basi wananchi wa nchi hii watakuja kufaidi rasilimali walizojaliwa na Mungu wao? Kwakuwa siku hazigandi, Mwenyezi Mungu amemsikia!

Waungwana katika simanzi kama hii furaha kwangu itatoka wapi? Kamwambieni mfalme kuwa mashati ninayo, lakini furaha sina kabisa!"

Nao walipokwisha kuyasikia hayo wakayakung'uta mavumbi yaliyokuwa yamegandamana kwenye pindo za mavazi yao, wakaondoka zao!

Waliwaendea vijana na wazee. Kwa walimu na madaktari kulifunikwa na migomo. Wastaafu hawakuulizwa kwa maana hali ilikuwa dhahiri.

Mwishowe wakawaendea viongozi wa dini. Majibu yao yalifanana. Walisema katika utawala ambao wananchi hawaridhiki kwasababu wanadhulumiwa kwa kunyimwa haki zao, kutekwa na kuteswa kinyama, kupigwa risasi za moto na mabomu, na hata kuuawa huku vyombo vya dola vikituhumiwa kuhusika furaha haiwezi kupatikana!

Kila siku wananchi wanajeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali na polisi wanakuwa kama hawapo. Kama wananchi hawajui kesho atakuwa nani, furaha wataipata wapi?

Wenye dhamana kama si sehemu ya unyama huu, wanapaswa kukiri kushindwa na kupisha wenye uwezo! Wakawaambia: "Rudini kwa mfalme mkamwambie kuwa Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha watu wake. Amwache Mungu atimize mapenzi yake! Mashati tunayo lakini furaha hatuna!"

Ikadhihirika kuwa katika nchi ile hakuwapo mtu aliyekuwa na furaha. Matumaini ya kupata shati la mtu mwenye furaha yakatoweka kabisa! Habari hizi zilipomfikia mfalme alisawajika naye akakata tamaa ya kupona! Nchi ikazizima, watu wakabaki wakisubiri amri ya Mungu!

Siku moja usiku Mwana Mfalme akitoka kwenye matembezi yake ya usiku akiwa na wapambe wake na walinzi walipita karibu na kibanda kimoja kibovu. Mchana ungeweza kumwona mtu aliyeko ndani ukiwa nje. Ndani yake walimsikia mtu aliyekuwa akijitayarisha kulala akisema: "Ee, Mwenyezi Mungu nakushukuru kwa kunijalia maisha yaliyo jaa furaha tele. Sasa napumzika kwa amani na nalala nikiwa na furaha iliyojaa moyoni! Ikiwa itatokea nikakuomba zaidi ya haya, Baba, nitakuwa nakukufuru ee Mungu wangu!"

Walipigwa na butwaa! Mtu mwenye furaha amepatikana! Dawa ya mfalme imepatikana! Mbio wakaenda wakamweleza mfalme. Naye bila kuchelewa akawatuma walinzi wake waende upesi wakamletee shati la yule bwana mwenye furaha!

Walipomfikia walimweleza shida yao na kumwomba awapatie shati lake haraka kwa sababu walidai hali waliomwacha nayo mfalme ilikuwa inazidi kuwa mbaya. Akiwa amevaa winda (pwani wangeita msuli, sehemu nyingine wanaita lubega). Kwa unyenyekevu mkubwa akawajibu akisema: "Waungwana ni kweli Mwenyezi Mungu amenijalia furaha kubwa sana kifuani mwangu! Ona mmenikuta nimelala raha mustarehe wakati wengine hawana pa kulala! Hii nyumba ni yangu. Nakula kila siku asubuhi na jioni (Chuoni wanasema anapiga pasi ndefu). Winda yangu hii mchana navaa ninapofanya kazi zangu au ninapokuwa kwenye matembezi. Usiku najifunika ndiyo shuka yangu! Ndiyo nguo pekee niliyonayo maishani mwangu. Sina uwezo wa kumiliki shati."! Walipoyasikia hayo maneno, walimwagika chini, wakabaki kujizoazoa tu hata wasijue sasa waende wapi!

Rais wangu kuna furaha gani kuongoza watu wasio na furaha? Kuwasikiliza watu wako, ukatimiza matakwa yao unapungukiwa na nini? Yamesemwa mangapi?

Mzee Abdulrahman Kinana kabla hajawa Katibu Mkuu wa CCM aliwahi kunitembelea nyumbani kwangu. Wakati anaondoka aliniachia neno ambalo hadi leo bado nalitafakari kama vile aliniambia jana. Alisema: "We, Mayega hela huna, lakini una amani kubwa sana kifuani mwako! Wewe ni mzalendo tu fulani unayeipenda nchi yako."

Ndugu Rais ndani ya chama chako una watu wazima wenye busara kubwa wengi sana lakini wengi huwatumii. Tunachoshuhudia hivi sasa katika hotuba zinazotolewa kwenye majukwaa katika ziara ya Katibu mkuu wa chama mikoani ni kelele tupu.

Katibu mkuu akihutubia, watu makini huiona busara ndani ya CCM. Anapofuatiwa na mtu wa kejeli, kashfa na porojo dhidi ya watu binafsi ambazo hazisaidii kutatua shida za wananchi, huchafua yote ya busara yaliyosemwa na katibu mkuu. Jioni wananchi huwaweka wote kwenye kapu moja la uongo, utoto hata upuuzi! Tatizo la chama liko kwa Mwenyekiti kuwang'ang'ania wanaoshusha haiba ya chama.

Rais wangu tusingoje mfalme wetu augue. Tutafute majibu mapema. Iweje wapinzani wote bungeni wawe wajinga, Ndugai peke yake awe ndiye mwenye akili? Kama Sugu alikataa kutoka bungeni, angelala ndani ya Bunge? Aliyepigwa ngumi sijui kichwa ajue hayo ndiyo matatizo ya kazi nyingine. Wote, wanaotii amri kama mbwa wa polisi anavyotii, hurudi nyumbani na ngeu!

Ndugu Rais wanaosema mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ni shemeji wanasema upuuzi. Lakini wanaweza wasiwe wapuuzi kama hawezi kazi kwasababu tu ni shemeji. Huu ni mwaka wa tisa sasa ameshindwa kumkamata askari aliyewaua kwa kuwapiga risasi wanawema ndugu watatu na dereva teksi, wafanyabiashara ya madini wa Ulanga.

Kionambali kwenye makala yake iliyopita aliandika kuwa, hata kama katika miaka kumi mtu aliwatengea Watanzania pilau njema lakini pakawapo na punje ndogo tu ya kinyesi katika sahani hiyo, wote watampuuza. Ataumbuka yeye! Ni wananchi wangapi wamenyanyaswa, kutekwa na kuteswa, kujeruhiwa kwa risasi na hata kuuawa huku Jeshi la Polisi likiwa ndiyo mtuhumiwa?

Ni wananchi wangapi wamemwagiwa tindikali na kujeruhiwa vibaya huku Jeshi la Polisi likishindwa kuwakamata wahalifu? Ni rahisi sana kwa wananchi kuamini kuwa wako wakubwa katika Jeshi la Polisi na katika vyombo vingine vya dola ambao ni wahusika wa uhalifu huu wanaowalinda wahalifu wasikamatwe, kuliko kuamini kuwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola ni dhaifu! Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Musa, awe wakwanza kutoa maoni kuhusu hili.

Baba kwanini usimtafute polisi mwenye uwezo na utashi, usiye na nasaba naye akusafishie Jeshi la Polisi na kulipanga upya usije ukaumbuka baadaye! Vinginevyo, wimbo wa rais wa, ‘nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuagiza Polisi kila tukio linapotokea utakuwa sawa na danganya toto!'

Kushauri tumeshauri. Kuonya tumeonya. Tuombe kwa maandiko yasemayo: "Batimayo aliomba kuona na alipoona aliona makuu ya Mungu! Bwana nipe macho ya rohoni nipate kuona yale yaliyopita, yaliyopo na yajayo kwa maana wakati wa mavuno ni karibu. Hapa nilipo nipo ugenini, ninaishi maisha ya taabu na shida. Wenyeji wangu wako mbinguni!

Source: Tanzania Daima
 

Attachments

  • 525691_426389837436728_807347031_n.jpg
    525691_426389837436728_807347031_n.jpg
    41.9 KB · Views: 129
Mzee mayega hao unaohangaika nao kila j5 ni sikio la kufa halisikii dawa. Ila usichoke mzee wangu ipo siku isiyo na jina kila kitu kitakuwa sawa
 
Hawa watafuta mwenye furaha wangeenda kwa kichaa au tuseme mwenda wazimu. Katika nchi kama hiyo uliyosema ni mwenda wazimu tu ndiye anayeweza kuwa na furaha!!
 
yaani anaeleza udhaifu wa viongozi wetu kwa mafumbo mafumbo.. dahh, sometime nahisi kama watanzania hatuko sawa.. yaani sheria zipo zinakiukwa , rasilimali za watanzania zinaondoka sisi tupobize na 10% za mikataba hiyo haramu, wazawa wanapuuzwa na wageni wanatukuzwa... , watu wanadhurika kila siku mikononi mwa polisi, watu wanauwa.. sheria zinapindishwa
 
yaani anaeleza udhaifu wa viongozi wetu kwa mafumbo mafumbo.. dahh, sometime nahisi kama watanzania hatuko sawa.. yaani sheria zipo zinakiukwa , rasilimali za watanzania zinaondoka sisi tupobize na 10% za mikataba hiyo haramu, wazawa wanapuuzwa na wageni wanatukuzwa... , watu wanadhurika kila siku mikononi mwa polisi, watu wanauwa.. sheria zinapindishwa
Mzee kajaliwa sana kueleza mambo, someni kitabu chake cha MWALIMU MKUU WA WATU.
 
Back
Top Bottom