kibogo
JF-Expert Member
- Apr 1, 2012
- 9,739
- 4,746
MWANZONI mwa miaka ya 80 nilipokuwa mwandishi wa habari kijana wa magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo, niliyekuwa nikiandika habari za bunge, hakuna mbunge aliyekuwa akinisisimua zaidi ya Padri Paulo Misigalo wa Tabora. Kwa sasa, mbunge anayenisisimua ni Alphaxard Kangi Ndege Lugola wa Mwibara (CCM).
Tofauti na Kangi Lugola, Mzee Misigalo yeye alikuwa na staili ya aina yake ya kuichachafya Serikali bungeni. Kinachomtofautisha Misigalo na wabunge wengi wa sasa ni kwamba alikuwa akifanya utafiti wa kutosha kabla ya kuwakabili mawaziri.
Siku anayopanga kuichachafya Serikali, Mzee Misigalo alikuwa akiingia bungeni na lundo la hati mbalimbali za ushahidi wa kile anachokusudia kukisema na kukijengea hoja – kuanzia kwenye vipande vya magazeti (press cuttings) hadi kwenye nyaraka, matamko na machapisho ya sera mbalimbali.
Alivitumia vitu hivyo kulithibitishia Bunge kuwa waziri fulani anadanganya, na kwamba anayoyazungumzia ni tofauti na miongozo au sera za Chama na Serikali.
Wakati akijenga hoja yake bungeni, Mzee Misigalo alikuwa na kawaida ya kunyanyua juu kutoka katika lundo hilo, kijitabu cha sera au mwongozo na kusoma vifungu fulani vinavyodhihirisha mkanganyiko wa waziri. Wakati mwingine alikuwa akisoma hata press cuttings za magazeti ya nyuma zinazomnukuu waziri fulani akitoa kauli tofauti na anazozitoa bungeni.
Enzi hizo Bunge lilikuwa la chama kimoja. Sina hakika kama mawaziri wetu wa sasa wa sampuli ya Stephen Wassira wangelipata muda wa kusinzia bungeni kama Mzee Misigalo angelikuwepo katika bunge hili la sasa la vyama vingi.
Ingawa enzi hizo walikuwepo pia wabunge wengine mahiri ambao hawakuogopa kuichachafya Serikali ya Mwalimu Nyerere – wabunge kama Leons Ngalai wa Rombo au Mzee Kaboboye wa Kigoma, Mzee Misigalo ndiye aliyenisisimua zaidi.
Bado nakumbuka alivyomkosesha raha waziri mmoja wa kilimo. Waziri huyo alikuwa amewasilisha bajeti yake ambayo msisitizo mkubwa ulikuwa katika kusambaza kilimo cha kutumia plau katika vijiji vyote. Aliliwasilisha suala hilo bungeni kana kwamba ni kitu kipya, na hapo ndipo alipomuudhi Mzee Misigalo.
Kilipofika kipindi cha wabunge kuchangia, Mzee Misigalo alianza kuchomoa kutoka kwenye lundo lake machapisho mbalimbali ya sera na miongozo ya Chama na Serikali na kusoma vifungu vinavyozungumzia suala hilo.
Kwa staili hiyo, alifanikiwa kuuanika hadharani ubabaishaji wa waziri yule. Mwisho wa yote ilithibitika kwamba kusambaza kilimo cha plau katika vijiji vyote nchini si ahadi mpya ya Chama na Serikali. Baadaye kwenye majumuisho yake, Waziri yule ilibidi akiri kwamba ahadi hiyo si mpya, na kwamba tatizo lipo katika utekelezaji tu!
Majuzi nilimkumbuka Mzee Misigalo wakati nikisoma postings mbalimbali kwenye mitandao za sifa anazomwagiwa Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kwa ‘kufanikiwa' kumaliza tatizo la ‘wafanyakazi hewa' serikalini.
Kwamba waziri huyu kijana ana timu ya mashabiki wake anaowatuma kumsifia mitandaoni na kumwaga picha zake kwa kila jambo la kumpandisha chati kisiasa analolitenda (kama vile kusaidia majeruhi wa ajali barabarani nk), si kitu cha ajabu kwa mtu anayependa sifa kupitiliza.
Cha ajabu, hata hivyo, na ambacho kwangu nafsi inakataa kukikubali ni pale wapambe hao wanapotia chumvi mno, na hivyo kuwapa wananchi matumaini makubwa mno ya kumalizika kwa tatizo (ufisadi) hilo lililodumu kwa zaidi ya miaka 20 chini ya serikali ya chama hiki tawala CCM.
Hivi karibuni wamemsifu mno kwa kung'amua uwepo wa ‘watumishi hewa' serikalini na kuchukua hatua kuzuia mishahara yao, na hivyo kufanikiwa kuokoa karibu Sh. bilioni 54.
Ninavyojua mimi, hata kama ni kweli hatua zimechukuliwa na hatua hizo zimesaidia kuokoa fedha hizo, haziwezi kuwa zimechukuliwa kwa utashi wa Naibu Waziri, Mwigulu Nchemba pekee. Zitakuwa zimechukuliwa kwa utashi wa wizara nzima ambayo inaongozwa na Waziri Saada na si Nchemba.
Lakini wapambe hao wanavyomsifu Nchemba kwa kila hatua chanya inayochukuliwa na Wizara ya Fedha, utadhani wizara hiyo haina waziri, na badala yake inaongozwa na Naibu Waziri Nchemba.
Kwa mujibu wa wapambe hao, sasa tatizo la ‘wafanyakazi hewa' serikalini litakuwa historia kwa sababu ‘mwarobaini' umepatikana, na ‘mwarobaini' wenyewe ni Mwigulu Nchemba!
Nina hakika kama majigambo hayo yangelikuwa yanamwagwa bungeni, na katika bunge hilo angelikuwepo Mzee Misigalo, bila shaka angelichomoa machapisho mbalimbali kutoka katika lundo lake la hati kuthibitisha ya kwamba hiyo si mara ya kwanza kwa serikali kujigamba kuwa imemaliza tatizo la ‘wafanyakazi hewa'.
Hebu nifafanue kidogo. Tatizo hili la mishahara hewa serikalini si jipya, na vile vile ahadi kwamba ‘mwarobaini' umepatikana wa kulimaliza si mpya. Ni tatizo ambalo tumekuwa nalo tangu Mwalimu Nyerere alipoondoka madarakani na kumuachia nchi Ali Hassan Mwinyi.
Binafsi, sihitaji wala uwepo wa Mzee Misigalo au Kangi Lugola kukumbuka kwamba karibu mawaziri wote wa fedha waliopita walilizungumzia tatizo hilo bungeni na kuahidi kuwa ‘mwarobaini' umepatikana na hatua zimechukuliwa, na hivyo tatizo litakuwa historia karibuni!
Ukweli ni kwamba pamoja na hatua zilizochukuliwa huko nyuma na kupatikana kwa ‘mwarobaini' huo, tatizo la mishahara hewa serikalini limekataa kuwa ‘historia', na badala yake limekuwa kubwa zaidi kama inavyobainishwa kila mwaka katika ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG).
Ripoti ya mwisho ya CAG niliyoisoma ilionyesha ya kuwa Sh. trilioni 1.62 zinapotea kila mwaka kwa njia hiyo ya malipo ya mishahara ya ‘wafanyakazi hewa'. Ilianzia kwenye mamilioni ya shilingi, ikaja kwenye mabilioni, na sasa tuko kwenye trilioni 1.62. Na serikali ni hii hii ya CCM!
Sasa, anapojichomoza waziri huyu chipukizi na kuahidi ya kuwa amepata ‘mwarobaini' wa kumaliza tatizo hilo, lazima tuwe na shaka. Na shaka hiyo ndiyo inayotusukuma kumkumbusha (kama ambavyo angekumbushwa na Mzee Misigalo) kwamba majigambo hayo si mapya, na ndiyo maana tatizo limezidi kuwa kubwa hadi kufikia kiasi hicho kikubwa cha pesa.
Inabidi tumkumbushe pia ya kuwa huo ‘mwarobaini' anaosema ya kuwa ameupata – yaani kuingiza malipo ya mishahara moja kwa moja kwenye akaunti za watumishi badala ya kupeleka fedha katika Halmashauri nao si utaratibu mpya. Walishawahi kuutumia huko nyuma na tatizo halikwisha!
Wasio wavivu wa kufikiri wanatambua ya kwamba tatizo la mishahara ya ‘wafanyakazi hewa' ni sehemu tu ya tatizo kuu la ufisadi linaloitafuna Serikali ya CCM (ya sasa na zilizopita), na ambalo ni dhahiri kwamba sasa hakuna nia wala dhamira ya dhati kulitokomeza.
Na ndiyo maana, hivi sasa, huwezi kumsikia kiongozi yeyote wa ngazi za juu akizungumzia vita dhidi ya ufisadi. Si siri kwamba vita hii dhidi ya ufisadi ni vita isiyotakiwa ndani ya Serikali na ndani ya chama chenyewe (CCM).
Hebu jiulize: Kwa nini hakuna mtaka urais hata mmoja kati ya waliokwishajitokeza mpaka sasa aliyediriki kutamka ya kwamba vita dhidi ya ufisadi itakuwa agenda yake kubwa akiingia Ikulu 2015?
Jibu ni rahisi; nalo ni kwamba ndani ya CCM ajenda ya vita dhidi ya ufisadi ni ajenda ya kuikwepa kama ukoma kama mtu anataka ateuliwe kugombea urais.
Na inakuwa hivyo kwa sababu wenye nguvu za pesa na wenye uwezo wa kushawishi wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wakuchague ugombee urais, karibu wote ni washiriki wa ufisadi mkubwa wa aina moja au nyingine nchini.
Na kwa maana hiyo, mafisadi hao hawawezi kujikaanga kwa mafuta yao wenyewe – yaani hawawezi kutumia mabilioni yao ya pesa waliyoyapata kifisadi kumpigia chapuo au kampeni mtu ambaye akiingia Ikulu ataendesha vita dhidi ya ufisadi – yaani vita dhidi yao!
Hofu hiyo dhidi ya wafanyabiashara wakubwa mafisadi nchini ndiyo imewafanya hata wale wataka urais ambao ni waadilifu kidogo kuikwepa ajenda ya ufisadi. Wanajua fika kuwa wakithubutu tu kujihusisha nayo watapambana na mtandao mkubwa wa mafisadi hao kuanzia kwenye wamiliki wa vitalu vya uwindaji na wamiliki wa migodi hadi kwa wafanya biashara haramu za pembe za ndovu na madawa ya kulevya.
Nihitimishe kwa kuwaambia Watanzania wenzangu kwamba tatizo la ufisadi ni tatizo la nchi nzima - ni tatizo ambalo limelelewa na chama tawala CCM kwa miaka mingi kiasi cha kukubalika sasa kuwa ni sehemu ya utamaduni wetu mpya. Tuendako, mtu utaonekana mwendawazimu kuzungumzia vita dhidi ya ufisadi Tanzania!
Ndiyo maana majuzi wala sikushtushwa na kauli ya Spika wa Bunge la Katiba, Samwel Sitta, kwamba fedha za posho za wajumbe wa UKAWA ambao wamesusia kikao cha bunge hilo, hazitarejeshwa serikalini; bali watatafuta namna bunge hilo linavyoweza kuzitumia!
Kama huo sio ufisadi ni nini? Fedha ambazo hazikulipwa kwa wajumbe wa UKAWA kwa nini zisirejeshwe serikalini zisaidie kununua madawati kwa wanafunzi wetu wanaokaa chini? Kwa nini wajumbe wa bunge hilo wazimezee mate; ilhali walichalipwa posho zao stahiki?
Hiyo ndiyo Tanzania. Nchi ya vituko. Ni nchi ambayo, pamoja na umasikini wake wote, rais wake na msafara wake mkubwa anakaa Marekani kwa wiki mbili akiteketeza fedha za walipakodi wakati huku nyumbani wananchi masikini wanachangishwa fedha kujenga maabara ya shule za sekondari za serikali!
Vyovyote vile, tatizo hili au utamaduni huu wa ufisadi hauwezi kumalizwa na hatua za waziri mmoja tu katika wizara moja tu; kama wapambe wa Mwigulu Nchemba wanavyojaribu kutuaminisha.
Ufisadi unaweza kumalizwa tu au kupunguzwa kwa hatua za pamoja za serikali nzima na taifa zima. Na silioni hilo likitokea katika serikali hii ya sasa ya CCM au ijayo kama itakuwa pia chini ya chama hiki.
Vinginevyo, hatua za namna hiyo – yaani hizi za kina Nchemba zisizo za serikali nzima, huwa na kawaida ya kuwa na matokeo ya kipindi kifupi, na hivyo ndivyo itakavyokuwa pia kwa ‘mwarobaini' wake huo wa kupambana na tatizo la ‘wafanyakazi hewa' Tanzania.
Vyovyote vile, majigambo yake hayo na ya wapambe wake hao ya kwamba tatizo hilo litakuwa historia si mapya. Yeye (Mwigulu) anaweza kuwa ni mwimbaji mpya, lakini wimbo anaouimba ni wimbo ule ule wa kale ambao umeshawachosha wasikilizaji! Labda uimbwe na mwimbaji kutoka chama kingine cha siasa lakini si CCM hii.
Tafakari.
Chanzo:Raia Mwema