JUMATATU, DESEMBA 31, 2012 04:48 NA GUSTAPHU HAULE, KIBAHA
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba, amesema ni ndoto kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuingia Ikulu. Amesema kwamba hata kama CHADEMA wana nia ya dhati ya kuingia Ikulu, jambo hilo halitawezekana na badala yake wanachama wa chama hicho wanatakiwa kurudi CCM ambako ndiko walikotoka.
Nchemba aliyasema hayo juzi, Kibaha Maili moja alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara.
Kama CHADEMA wanategemea mwaka 2015 ndipo waingie Ikulu, wakidhani watapata nafasi ya kushinda, wajue CCM itawasambaratisha mapema na hivyo kubaki wakinyoosheana vidole wao kwa wao.
Nawaambia CHADEMA ifikapo mwaka 2016 itakuwa imekufa kabisa.
CHADEMA wanadhani kuingia Ikulu ni jambo jepesi, siyo rahisi kama wanavyodhani kwa sababu hawana nguvu za kuweza kuongoza.
CCM ni chama ambacho kimeota mizizi katika pembe zote za Tanzania, hivyo itakuwa vigumu kwao CHADEMA kuingia Ikulu.
"Nawaambia ndugu zangu wa CHADEMA, kwamba waache fikra za kutaka kuingia Ikulu mwaka 2015, kwani naamini hawataweza kwa sababu sisi tutawapiga mapema. Ni bora wakafanya kazi za kuwatumikia wananchi ili nchi yetu iwe na maendeleo na ikiwezekana waache kabisa kufikiria suala la uchaguzi wa mwaka 2015,'' alisema Nchemba.
Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, alisema CHADEMA wanatakiwa kutowadanganya wafanyakazi, kwamba wakiingia madarakani wataweza kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa kuwaongezea mishahara.
Alisema kwamba, suala hilo gumu kutekelezwa na chama hicho cha upinzani kwa kuwa hawana uwezo kwa kuwa hata mishahara ya viongozi wao wameshindwa kuiongeza.
"Mimi nafikiri muda wa kuanza kuwadanganya wafanyakazi kuwa wakiingia madarakani watawaongezea mishahara, hilo sio kweli kwani kama wanataka kufanya hilo ni vema wakaanza kuwalipa mishahara hiyo wafanyakazi wao, kwani mpaka sasa wapo baadhi wanalipwa Sh milioni 7 kwa mwezi wakati wengine wakilipwa Sh 60,000.
Kitendo cha CHADEMA kuwadanganya wananchi, kwamba ili maendeleo yaje lazima wahamie kwenye chama chao, siyo sahihi kwa sababu maendeleo yanakuja baada ya kila mmoja kutimiza wajibu wake.
Katika mazungumzo yake Nchemba, alisema kuna wabunge sana wa CHADEMA wana mpango wa kuhamia CCM wakati wowote.
"Mimi leo natoboa siri katika mkutano huu, nasema hivi, mpaka sasa wabunge saba wa CHADEMA wameshakuja kuomba ili wahamie CCM, lakini tumewaambia wasubiri kwanza wawatumikie wananchi katika kipindi cha miaka hiyo mitano na kisha warudi CCM ili waendelee na siasa,'' alisema.