Mwekezaji mpya mradi wa gesi akwamishwa

Makaayamawe

JF-Expert Member
Feb 21, 2009
341
9
Mwekezaji mpya mradi wa gesi akwamishwa



Wakati malumbano ya Dowans yakiendelea..

WAKATI mvutano wa kununua au kutonunua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Dowans yenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 ukiendelea, kuna mwekezaji anayedaiwa kukwamishwa ambaye yuko tayari kutoa fedha za kufanikisha mradi wa uzalishaji wa umeme wa megawati 300 kwa kutumia gesi asilimia, Raia Mwema imabaini.

Habari zilizopatikana wiki hii zinasema kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Barrick, kwa niaba ya kampuni nyingine za madini, ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha mradi huo, lakini menejimenti ya Shirika la Umeme (Tanesco) imeshindwa kukubaliana na mapendekezo ya kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo kadhaa vya habari, mapendekezo hayo ni pamoja na kufunguliwa kwa akaunti ya pamoja kati ya Tanesco na Barrick, uamuzi ambao unapendekezwa na Barrick ili ijihakikishie kuwa fedha itakazotoa kwa ajili ya kufanikisha mradi huo daima zinabaki salama.

Inaelezwa kuwa Barrick imekuwa na wasiwasi huo dhidi ya Tanesco kwa kuwa tayari iliwahi kulipa shirika hilo pekee la kuzalisha umeme nchini dola za Marekani zaidi milioni 80 (zaidi ya Sh. bilioni 80), ili ipatiwe umeme wa uhakika katika migodi yake lakini Tanesco ikashindwa kufanya hivyo kama makubaliano yalivyokuwa.

Uchunguzi zaidi kuhusu kukwama kwa mradi huo unabainisha kuwa Tanesco imekuwa ikipendekeza kupewa fedha zote na mfadhili wa mradi (Barrick) na iendelee na kazi zote zilizosalia za ujenzi wa mradi, bila kujali kuwa Sh bilioni 80 zilikwisha kutolewa na Barrick.

Miradi ya umeme ambayo Barrick imewahi kutoa fedha ni pamoja na mradi wa umeme Kahama (dola za Marekani milioni 25), Buzwagi (dola za Marekani milioni 35) na mradi wa umeme mkoani Mara (dola za Marekani milioni 28).

Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Barrick, Teweli Teweli katika mazungumzo hayo alikiri kuwa kampuni hiyo kwa niaba ya kampuni nyingine za madini walipendekeza kwa Tanesco kufunguliwa kwa akaunti ya pamoja ili fedha hizo zitumike kufanikisha mradi wa umeme wa megawati 300.

“Ni kweli kwamba Barrick, kwa niaba ya kampuni nyingine za madini, tulipendekeza ifunguliwe akaunti ya pamoja, fedha mnaweka humo lakini mazungumzo haya yalishindwa kukamilika. Haya maelezo kwamba Barrick imekwamisha mradi huo si kweli kabisa,” alisema ofisa huyo.

Raia Mwema haikufanikiwa kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idriss Rashid ili azungumzie suala hilo.

Lakini wakati mvutano kuhusu mradi huo ukiendelea, Kampuni ya Artumas yenye jukumu la kuvuna gesi na kuuza kwa ajili ya kuzalisha umeme na shughuli nyingine, ilikwisha kufanya upembuzi yakinifu kuhusu uwezekano wa kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa kuzalisha megawati 300 za umeme kwa gesi kutoka Mnazi Bay, mkoani Lindi.

Taarifa zilizothibitishwa na Meneja Mkuu wa Artumas, Salvator Ntomola, zinaeleza ya kuwa kampuni hiyo ilitumia dola za Marekani milioni mbili kwa ajili ya upembuzi huo yakinifu.

Matokeo ya upembuzi huo yakinifu yanatajwa kuwa ni pamoja na mradi huo kuweza kukamilika na umeme wake kuingizwa katika gridi ya Taifa kwa kutumia njia kuu mbili.

Njia ya kwanza ni umeme huo kuingizwa katika Gridi ya Taifa katika kituo cha Dar es Salaam na nyingine ni umeme huo kusafirishwa na kuingizwa katika gridi ya Taifa katika kituo cha umeme Makambako, mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa ufafanuzi uliotolewa kwa gazeti hili na uongozi wa Artumus, mradi huo hauhusiani na mradi wa sasa wa uzalishaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambao umekamilika na umeme wake umeanza kutumika.

Mradi wa umeme katika mikoa ya Mtwara na Lindi unaozalishwa kwa gesi ya Mnazi Bay kwa sasa una uwezo wa kuzalisha megawati 12.

Kwa mujibu wa Ntomola, kutokana na kukamilika kwa mradi huo, gharama za uzalishaji umeme zimepungua kwa kiasi kikubwa.

“Dola za Marekani milioni 6.4 hivi sasa zinaokolewa kutokana na kukamilika kwa mradi huu. Uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi ni nafuu zaidi ikilinganishwa na umeme unaozalishwa kwa mafuta, ambayo huagizwa kwa fedha za kigeni kutoka nje ya nchi,” alisema Ntomola akiongeza ya kuwa kutokana na mwenendo wa mambo nchini, mradi mkubwa wa megawati 300 umepangwa kukamilika mwaka 2013.

Alisema uvunaji wa gesi pia umekuwa na faida kubwa kwa Serikali ikilinganishwa na uvunaji wa rasilimali nyingine ambazo ni pamoja na uchimbaji madini.

“Katika uvunaji wa gesi, Serikali imekuwa ikipata asilimia 70 ya faida inayotokana na shughuli za uchimbaji zinazoendeshwa na mwekezaji. Kwa hivyo baada ya kuondoa gharama zote, inabaki faida ambayo mwekezaji anachukua asilimia 30 na Serikali asilimia 70,” alisema Ntomola.

Hali hiyo katika gesi ni yenye faida kubwa kwa Serikali ikilinganishwa na uchimbaji madini ambako Serikali huambulia asilimia tatu tu ya mrahaba.

Watalaamu wa masuala ya uchumi wamekuwa wakipendekeza kuwa ni muhimu kwa Serikali kuwekeza zaidi katika miradi ya umeme kwa kutumia gesi asilia ili iweze kuvunwa kwa wingi na Serikali kupata fedha nyingi zaidi na pia Taifa kuwa na umeme wa uhakika unaozalishwa kwa gharama nafuu.

Kwa sasa Serikali kupitia Tanesco imekuwa ikihangaika na miradi ya umeme wa dharura unaozalishwa kwa gharama kubwa kwa kutumia mafuta.

Miradi hiyo iliyowahi kutumiwa na Tanesco ni pamoja na Dowans (megawati 100), Aggreko (40 megawati) na Alstom (megawati 40). Lakini pia shirika hilo limeanza kuwa na miradi ya umeme unaozalishwa kwa gesi, ambao ni mradi wa umeme Ubungo, unaoingiza megawati 102.5 katika gridi ya Taifa.
 
Ni miradi mizuri lakini hofu yangu ni aina za mikataba tunayoingia na watu hawa. Uwekezaji katika utility sector upo wazi sana, kwanini tusicopy strategies zilizotumika hapa UK?. Nasema hivi kwasababu, wanauzoefu wa 200years juu ya concession agreement kwenye sector hii ya energy. Uzoefu wao huu ni pamoja na matatizo mengi juu ya mikataba hii na mafanikio pia. Hivyo kwa sasa kuna taratibu nzuri tuu watanzania tunaweza kujifunza na kuzitumia tanzania.Nilisha andika sana juu ya swala hili. Nadhani hatuna dira nzuri juu ya jambo hili. We are still operating in a very traditional way which is not benefiting us rather than being a conundra.
 
...nasikitika sana maana tuna kila kitu cha kuondoa tatizo la umeme once and for all kwa watanzania wote maana proven reserve gas tuliyonayo nasikia inaweza kwenda for 50 yrs na nchi nzima ikawa na umeme...wananchi tumekosa leadership tuu hatuna tatizo la umeme Tanzania,na policy ya sasa ya umeme ni utapeli mtupu na hakuna serious investor anaweza weka pesa zake ndio maana investor wengi wanaokuja ni matapeli tuu ambao wanajua kabisa wakifuata sheria za umeme watakula hasara tuu ndio maana nao ni matapeli tuu wanaojua kucheza na system yetu ya walafi,sijui hata wabunge tulio nao kama ni smart wanaoweza kuandika bill iliyoenda shule...tumejaza bungeni watu wasio jua chochote na hawana idea wanafanya nini na hata kusoma wengine hawajasoma na hawaelewi hata namna ya kuweka policy yeyote ya maana...Tanzania haina shida ya umeme ni uongozi ndio unaleta mgao
 
Back
Top Bottom