Mwandishi wa habari alivyomvurumishia rais Bush viatu

Hashpower7113

JF-Expert Member
Sep 26, 2011
1,353
2,142
Hebu vuta picha, mheshimiwa rais anazungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala nyeti yanayolikabili taifa. Vituo kadhaa vya runinga vinarusha tukio hilo moja kwa moja (Live), ghafla mwandishi mmoja wa habari anavua ‘mabuti’ yake na kumvurumishia mheshimiwa rais kwa lengo la kumjeruhi! Haiwezekani?

Basi kwa taarifa yako, tukio kama hilo limewahi kumkumba Rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush alipokuwa ziarani nchini Iraq.

Ilikuwaje? Desemba 14, 2008, Rais Bush akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Iraq, Nouri al- Maliki, walikuwa wakizungumza na waandishi wa habari ndani ya Ikulu ya Baghdad.

Katika hali isiyo ya kawaida, mwandishi ambaye baadaye alitambulika kwa jina la Muntadhar al-Zaidi alionesha kukasirishwa na kilichokuwa kinazungumzwa na Bush kuhusu madhara ya vita ya Iraq, akavua viatu vyake viwili na kuvirusha kwa nguvu kwa lengo la kumpiga Bush.

“Hili ni busu la kwa heri kutoka kwa watu wa Iraq, mbwa wewe!” alipaza sauti al- Zaidi wakati akirusha kiatu cha kwanza.

“Na hii ni kwa ajili ya wajane, yatima na wote waliokufa kwenye vita ya Iraq,” alisema huku akirusha kiatu cha pili.

Shukrani kwa mafunzo ya kijeshi aliyokuwa nayo Bush kwani alifanikiwa kuvikwepa viatu hivyo kwa ustadi mkubwa, vinginevyo vingemjeruhi vibaya kutokana na nguvu aliyoitumia al- Zaidi.

Muda mfupi baadaye, mwandishi huyo alikamatwa, kupigwa na kutolewa mzobemzobe kwenye chumba cha mikutano na kwenda kufungiwa kwenye chumba maalum.

Waziri Mkuu, Maliki alijaribu kukidaka kiatu kimoja ili kuzuia kisimpate Bush. Katika purukushani hiyo, Msemaji wa Ikulu ya White House, Dana Perino alibondwa usoni na ‘mic’ iliyogongwa na walinzi wa rais wakati wakihangaika kumuokoa asidhurike. Perino alipatwa na tatizo la damu kuvilia kwenye jicho.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Bush alisema ni tukio la kawaida na akaingiza mzaha kwamba kama watu walihitaji kujua zaidi, viatu vilivyotumika ni namba kumi.

“Sijakasirishwa na kilichotokea, naamini hii ni jamii mpya inayochipukia. Sidhani kama ni sahihi kuwahukumu wananchi wote wa Iraq kwa sababu ya mtu mmoja aliyenirushia viatu,” alisema.

Kufuatia tukio hilo, al- Zaidi alikamatwa na kuburuzwa mbeleya sheria lakini wananchi wa Iraq na mataifa mengine ya Kiarabu, walimuona kuwa shujaa wao, maandamano ya kushinikiza aachiwe yakaanza kufanyika nchi nzima, huku habari hiyo ikipewa uzito wa juu na karibu vyombo vyote vya habari.

Zawadi mbalimbali ziliendelea kumiminika kumpongeza al- Zaidi ambapo matajiri wa Kiarabu, waliendelea kuipa familia yake vitu vingi vya thamani, zikiwemo fedha na magari ya kifahari, likiwemo Mercedes Benz la milango sita.

Pilikapilika hazikuishia hapo bali kulichongwa pia sanamu kubwa ya kiatu kilichotumika kutaka kumpiga Bush na ikasimamishwa katikati ya Baghdad ikiwa ni jina la al-Zaidi ingawa iliondolewa na polisi muda mfupi baadaye.

Baada ya kesi yake kunguruma kwa miezi kadhaa, Machi 12, 2009, al-Zaidi alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani. Baadaye hukumu hiyo ilipunguzwa hadi kuwa mwaka mmoja jela. Septemba 15, 2009 akiwa tayari ametumikia kifungo cha miezi tisa, al- Zaidi aliachiwa huru baada ya kuonesha tabia njema gerezani.
 

Attachments

  • muntazer-al-zaidi-jpg.jpg
    muntazer-al-zaidi-jpg.jpg
    42.5 KB · Views: 61
  • Busha.jpg
    Busha.jpg
    14.6 KB · Views: 73
Ukijaribu hayo Africa unauawawa, sababu rais ni kama Mungu, tena si kwamba rais mwenyew ndo atasema ushugulikiwe la hasha vibaraka. Kiongozi yoyote aliyepevuka anajua kuna maamuzi mengi yanawakasirisha watu, so hapaswi kureact na individuals, hebu angalia Bush alivyojibu.
Kweli mkuu, kwa Afrika ukijaribu tu, basi you are gone for good! Wenzetu wamekomaa sana kisiasa
 
Back
Top Bottom