Mwanamke afundisha timu ya soka ya wanaume.

Achraf Hakimi

JF-Expert Member
Mar 3, 2010
875
1,779
Mwanamama aitwaye Donna Powell ametengeneza historia huko nchini Uingereza ya kuwa mwanamama wa kwanza kuwa kocha wa timu ya soka, na hii yote ni baada ya kushinda shindano la kumtafuta kocha mwananama wa kwanza wa timu moja ya nchini Uingereza iitwayo Fisher Athletic. Mama Powell alipewa jukumu hilo la kuwasaidia Fisher athletic kuepuka kushuka daraja baada ya kushinda mnada ambao zawadi yake ilikuwa ni kupata nafasi ya kufundisha soka kwa siku moja katika timu ya Fisher. Inaaminika kuwa Mama Powell ndiye alikua mwanamama wa kwanza kuwa kocha wa klabu ya soka ya wanaume. Lakini hii yote ilianzaje? na ikawaje hadi mwanamke huyu akajikuta akikabidhiwa jukumu hilo zito la timu hiyo ambayo ukiachilia mbali matatizo yake ya kifedha pia ilikua hatarini kushuka daraja. Mama Powell mwenyewe alinukuliwa akisema kuwa mabosi wa timu hiyo walifanya mkutano na kufikia uamuzi wa kufanya shindano la kumtafuta kocha wa kike kwa siku moja ikiwa ni njia ya kuchangisha pesa kwa ajili ya kuinusuru klabu hiyo. Mama Powell anakubali kuwa isingekuwa hilo shindano kamwe asingeweza kupata nafasi hiyo sababu kubwa ikiwa yeye ni mwanamke. Mwanamke huyo alielezea kwamba alishawahi kuomba kazi katika nafasi hiyo mara baada ya kocha wa zamani kuondoka lakini mabosi walifikiri kuwa anatania, lakini kipindi hiki Mama Powell alijipiga mfukoni akakusanya kiasi cha pauni 500 ili aweze kushiriki katika shindano lililomuweka hapo. Mama Powell ambaye kabla ya hapo alikuwa kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 11 iitwayo Red Lion Boys club amekabidhiwa mikoba ya kuifunga timu ya Eastleigh katika mechi yake ya kwanza akiwa katika benchi la ufundi la Fisher athletic. Tayari Mama Powell anakwambia alishafanya utafiti kuhusu timu pinzani na mpango wake wa kwanza ni kubadili mfumo wa uchezaji wa timu yake toka mfumo wa 3-5-2 na kuwa 4-4-2 sababu aliamini vijana wake wangecheza mfumo huo wangepata nafasi ya kumiliki mpira zaidi. Mwenyekiti wa klabu ya Fisher Martin Eddie alisema kwamba baada ya mwezi tu ndani ya msimu iliwalazimu kuwaachia wachezaji wote waondoke sababu walishindwa kuwalipa mishahara yao. Kocha wa zamani ilibidi aondoke na kuhamia timu nyingine wakabaki mabosi wawili akiwemo mwenyekiti na watu wachache waliojitolea kuisaidia timu hiyo. Mama Powell hakuamini kabisa kuwa Fisher wangeshuka daraja ingawa walikuwa katika nafasi ya pili toka mkiani wakiwa wamefungwa mechi 11 mfululizo!Mama Powell anajiamini sana juu ya uwezo wake na mara zote huwa yuko thabiti na msimamo wake kuwa Fisher haitoshuka daraja kamwe, anachukulia kazi yake kwa umakini mkubwa sana. Ingawa kifedha klabu hiyo haikua katika hali nzuri Mama Powell aliamini kuna njia nyingi sana za kuwahamasisha wachezaji katika vyumba vya kubadili nguo ama mazoezini. Kila mchezaji alijua baada kufungwa mechi 11 mfululizo kilichohitajika ni ushindi tu na wala si kingine. Mama Powell ambaye ana daraja la kwanza na pili la ukocha linalotambulika na chama cha soka nchini Uingereza si mgeni katika ulimwengu wa soka uliotawaliwa na wanaume, na alijua fika mikiki mikiki yote ambayo angekumbana nayo wakati akiwa katika benchi la timu ya Fisher, hii ilikua nafasi ya kung'ara kwa nyota yake. Anaelezea kwamba alishawahi kukumbana na makocha wa timu pinzani ambao waligoma kusalimiana naye mara baada ya timu yake kuwapa kichapo. Anasema wengi huwa wanakuwa wakijisikia wamedhalilishwa sababu ya kufungwa na mwanamke. Anamalizia kwa kusema kuwa anadhani ni muda umefika kwa wanawake kufundisha soka, kama wanaume wanaweza kwa nini wanawake wasiweze?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom