Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,742
- 40,874
Nilipoandika wiki kadhaa kuhusiana na baadhi ya mambo ambayo yanatukwaza baadhi yetu ambao tulimuunga mkono Magufuli ni jinsi gani Serikali inajichoma yenyewe mkuki mguuni na inataka kukimbia. Kwamba, kuna mambo mengi ya msingi yanalikabili taifa na badala yake wanatumia muda na raslimali nyingi kushughulikia mambo yasiyo ya msingi.
Watoto wetu wanakabiliwa na changamoto nyingi sana za kielimu na maisha nje ya shule. Wengi wa watoto wetu hawana mambo ya maana wanayoyafanya baada ya saa za shule na badala yake wengine wanajikuta wakiishi maisha ambayo hayajengi afya na safari yao ya kielimu. Mara ngapi tumewaona watoto wa umri wa shule wakiwa kwenye burudani ambazo zina maudhui ya watu wazima? Mara ngapi tumeona watoto wakisikiliza wakati wanamuziki wa ‘kizazi kipya’ wanaporekodi mitaani nyimbo zenye maudhui ya mambo ya ngono – kwa maneno na kucheza kwake? Mara ngapi tumeona vipindi vya redio vikirusha mipasho mchana kweupe mbele ya umati wa watoto na watu wazima na tunawaona watoto wanashingilia mipasho ya kingono?
Halafu serikali inaamini tatizo letu ni viroba? Hili nitalieleza wakati mwingine. Ninachotaka kusema ni kuwa tuna mambo mengi sana muhimu, mazito na ya msingi katika ujenzi mpya wa taifa letu; ujenzi ambao wengi wetu tuliamini kuwa unaweza kufanikiwa chini ya Rais Magufuli bila kujali uwepo wa CCM. Tuliamini kuwa uthabiti, umakini na uwezo wa Magufuli kusimamia nidhamu katika utumishi wa umma, kupambana na vitendo vya ufisadi na kuweka mambo ya msingi kwanza basi mambo ambayo hayakuwezekana miaka 50 iliyopita yumkini yakawezekana miaka hii mitano ijayo.
Nilisema katika makala iliyopita kuwa kwa serikali kuanza kujipiga piga mikuki na misumari miguuni ni vigumu kuona jinsi gani itaweza kuharakisha maendeleo kwani ni wazi itabidi ishughulikie vidonda hivi vya kujitakia au ivipuuzie ije kujutia baadaye.
Binafsi sijalitolea maoni suala la Lissu kutaka kugombea Urais wa TLS (chama cha wanasheria wa Tanzania bara) kwa sababu moja niliamini hakuna lolote la tofauti kwani miaka yote wamekuwa wakigombea na kuchaguana bila kuingiliwa na mtu yeyote. Tatizo kubwa ni kuwa inaonekana safari hii uchaguzi huu umevutia hata watu ambao walikuwa hawajui kuna TLS kufuatilia hasa baada ya Tundu Lissu kuonesha nia yake ya kugombea uongozi wa chama hicho.
Imetumika nguvu kubwa ya kujaribu kuzuia Lissu asigombee. Sioni sababu, mantiki, wala hoja ya msingi ya kufanya hivyo.
Serikali Haina kura za kutosha?
Inawezekana sababu ya kutotaka Lissu asigombee ni hofu ya kuwa endapo atasimama anaweza kushinda. Kwa maneno mengine inawezekana kuna hofu kuwa Lissu ana “kura za kutosha” kwenye chama hicho na hivyo serikali haina kura za kuweza kumzuia. Kama hili ni kweli, tatizo siyo la Lissu! Ni tatizo la serikali kama pamoja na mawakili wake wote waliopo serikalini haina kura za kuweza kuhamasisha mtu inayemtaka. Hii ni sehemu ya demokrasia. Lissu anaweza kushindwa uchaguzi huu ‘fair and square’ endapo atashindanishwa na mtu mwingine ambaye naye anamvuto wa hoja na misimamo na hivyo akawakilisha maslahi ya upande mwingine. Kwamba kuna uwezekano katika serikali nzima hakuna mwanasheria ambaye ana mvuto wa hoja kama Lissu ni jambo la kushtusha.
Hoja Zishinde Siyo Vihoja
Mojawapo ya mambo ambayo nimeyakataa muda mrefu sana ni kuwa hoja zenye nguvu ni lazima zishinde na siyo hoja za nguvu. Lakini baya zaidi tusikubali vioja, na “vihoja”* vishinde hoja. Mimi ni muumini kuwa katika demokrasia na katika uongozi ni muhimu kuweka hoja zishindane na zile zenye mantiki na zinazoshinda hoja nyingine ndio zikubaliwe. Vitisho vya aina yeyote havijawahi kuwa hoja; hiki ndicho Baba wa Taifa aliwahi kukiita “nguvu za hoja”. Kukamata watu, kutishia kuwapiga, kuwafunga au kuwanyanyasa ili wakubali hoja fulani ni “hoja za nguvu” yaani nguvu inakuwa hoja.
Lissu kama mwanasiasa na mwanasheria anaweza kabisa kupingika kwa hoja. Iwe mahakamani, iwe Bungeni, iwe nje ya Bunge. Lakini unapompinga kwa hoja ni lazima hoja yako iwe na nguvu ndani yake. Huwezi kumshinda mtu kama Lissu kwa kumkamata, kumfunga, kumpiga mikwara au kumnyanyasa kwani kwa kufanya hivyo hata watu ambao walikuwa hawafuatilia hoja yake wataanza kufuatilia na kusikiliza majibu yako juu ya ya hoja zake. Kwa mfano, Lissu akisema serrikali haiheshimu haki za binadamu na akatolea mfano ni jukumu lako katika kumpinga kwa hoja kuonesha ni jinsi gani serikali inaheshimu haki za binadamu na siyo kutolea mifano vitu vingine bali vile vile alivyovisema yeye; Lissu (au mtu mwingine) akisema Serikali au kiongozi fulani anavunja Katiba na akatolea mifano ni jukumu la wanaojibu kuonesha ni kwa nini kiongozi au mtu yule havunji katiba katika masuala yale yale; kumkamata Lissu kwa hoja yake bila kuijibu hoja hiyo ni kuipa nguvu hoja hiyo pamoja na kumkamata Lissu.
Lissu asiruhusiwe kugombea?
Mojawapo ya hoja mbovu ambayo imetolewa hivi karibuni ni hii ya kutotaka Lissu asigombee uongozi wa TLS kwa sababu ni kiongozi wa CHADEMA na kuwa kuna hofu ya kwamba TLS inageuka chama cha siasa. Hii ni hoja muflisi kwa kila kipimo. Serikali na CCM nayo ina washeria wengi na makini, kuanzia Waziri wa Sheria na Katiba ndugu yangu na rafiki yangu Mwakyembe hadi dadangu Tulia Ackson; ina wanasheria mikoa yote na wengi ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi. Inawanasheria wengine wabunge na wapo watendaji kwenye taasisi nyingi ambao nao ni wanasheria. Kuanzia TAKUKURU hadi Ikulu kuna wanasheria. Sasa, kwanini hawa wote asiwepo mmoja wao naye akagombea kwa hoja nzito ili apambanishwe na Lissu na watu wengine?
Kama Lissu akagombea na akashinda pamoja na upinzani wote ambao unapatikana ni wazi kuwa serikali imeshindwa hoja. Matokeo ya hili ni serikali ijitathmini kama mkakati wake ni sahihi. Hatuwezi kuwakataa wanaotupinga kwa kuwanyima nafasi ya kutupinga! Tunaweza tu kuwakataa wanaotupinga kwa kuwapinga kwa hoja zetu dhidi ya hoja zao za kutupinga. Mwenye nguvu mpishe; mwenye hoja mpishe! Kama huwezi kutetea hoja yako au uongozi wako kwa hoja maridhawa ni haki basi wanaokupinga waendeleee kukupinga kwa hoja zao hadi utakapopata watu watakaoweza kujenga hoja za kujibu mashambulizi.
Ukweli wa hili wengi tunaojua hasa wale ambao tuliwahi kuwa kwenye vilabu vya midahalo mashuleni (debates clubs). Labda siku hizi vilabu hivi havipo sana kiasi kwamba watu hawajifunzi tena jinsi ya kujenga hoja, kuchambua hoja, kupinga hoja, kuona makosa katika hoja (fallacies) n.k Watu wanaendeshwa kwa habari tu bila kufikiria hoja zilizoko nyuma.
Mwacheni Lissu Agombee na Aongoze
Binafsi naamini kabisa kuwa kati ya wanasheria wote ambao wapo sasa hivi ni wachache sana wana ujiko na hadhi ya Lissu linapokuja suala la kutetea sheria, katiba, haki za binadamu na haki za kiraia. Sijaona mtu serikalini – na hili ni kweli – na nje ya serikali ambaye anaweza kulingana naye. Ninamfahamu Lissu kwa muda mrefu. Pamoja na kuwa sehemu ya kuvuruga CHADEMA kwa kumkubali Lowassa kuelekea uchaguzi mkuu 2015 bado naamini alifanya vile kama a “tactical option’ ya kujaribu kuiangusha CCM hata kama ilikuwa ni tactic mbaya ambayo wengine tuliona ingedhoofisha upinzani na siasa zetu nchini. Hata hivyo, pamoja na hilo rekodi yake linapokuja suala la sheria na utawala na kusimamia haki na katiba inapitwa labda na mtu mmoja tu – Marehemu Christopher Mtikila.
Ninaamini sasa hivi joho la kupigania haki za wananchi na zile za kibinadamu ambalo Mtikila alilivaa kwa karibu miaka thelathini limevaliwa na kuvaliwa vizuri na Tundu Lissu. Kumpa heshima na jukumu la kuongoza TLS ni kuwapa heshima wale wote ambao wamekuwa wakisimamia haki na demokrasia.
Kuifuta TLS sababu ya Lissu
Mojawapo ya mambo ambayo hayapaswi kutokea kabisa ni hili la kuifuta TLS ati kwa sababu Lissu anaweza kuwa kiongozi. Huu ni uamuzi mbaya na unaonesha kuwa usio na msingi. Kama nilivyosema hapo juu hoja ishinde hoja tu. Kama wanasheria wa Watanzania wanaamini Lissu anafaa kuwa kiongozi wao na wakampigia kura na akashindwa ni jukumu lao kukubali na kuishi na uamuzi huo. Kama vile wapo watu ambao walimpigia Magufuli kura na wakajua jinsi uongozi wake utakavyokuja nao wanaishi na uamuzi huo kwa miaka mitano ijayo. Lissu hawi kiongozi wa maisha wa TLS kama vile Magufuli siyo kiongozi wa maisha wa Tanzania. Wote wawili wanaweza kuwa wamechaguliwa kidemokrasia na wote wawili wanapaswa kuishi kutoka na maamuzi hayo ya kidemokrasia.
Baada ya Mambo Hayo Yote
Naombe kusema tu kuwa baada ya mambo haya yote mtu akiniuliza mimi nitasema tu kuwa wanasheria wanaokutana mkoani Arusha kuchagua kiongozi wao naamini wanapaswa kumchagua Tundu Lissu kuwa kiongozi wao kwa fikra za “liwalo na liwe”. Si kwa sababu ya kuikomoa serikali bali kwa kumchagua mtu ambaye ana uwezo, weledi na ameshakuwa tayari mara kadhaa kulipa gharama ya kuwa na msimamo fulani. Lissu ni zao la demokrasia, na ni tunda la utawala uliopo. Tukumbuke kuwa Lissu hajaanza kunyanyaswa leo kutokana na kupigania haki mbalimbali na ni gharama ambayo yeye mwenyewe amekuwa tayari kuilipa. Kwa kukubali kwake kuvaa Joho la Mtikila Lissu anastahili nafasi ya kuwaongoza wanasheria wa Tanzania.
Kama inabidi kuifuta TLS…
Kama inabidi kuifuta TLS basi chombo chochote kitakachoundwa baada yake ni lazima kiwe nje ya utawala wa serikali kabisa. Na ikiwezekana kiwe huru kabisa kama vyombo vingine vya kitaaluma ambavyo haviingiliwi na serikali zaidi ya kutajwa kwake kisheria kuwa vitakuwepo. Kuunda chombo cha wanasheria ambao kitasimamiwa na serikali kiasi cha kuamuliwa nani akiongozi itakuwa ni udhoofishaji uliopitiliza wa taaluma ya sheria nchini. Na wanasheria wanapaswa kupinga. Our learned brothers and sisters must eventually and categorically RESIST such attempts.
[HASHTAG]#Isupport[/HASHTAG]TL4TLS
* Vihoja – vihoja vidogovidogo vinavyojaribu kuchukua nafasi ya hoja nzito.