MwanaCCM halisi ni mtu jasiri sana, ni kada na askari shupavu

USSR

JF-Expert Member
Jul 15, 2015
9,896
22,664
Mwanaccm halisi ni mtu jasiri anayesimamia haki na usawa huku akihakikisha katiba, kanuni, miongozo na taratibu za CCM zote zinalindwa. Ukiona Mwanaccm akienda kinyume na haya, fahamu upo uwezekano aliingia kwenye chama kwa njia za haramu, hivyo hana mapenzi ya dhati.

Wanaccm hatupaswi kuwa waoga kusema kwenye mambo ya msingi ya kukiimarisha chama. Profesa Issa Shivji, mwanataaluma wa sheria, alisema, "Ndiyo maana Mwalimu JK Nyerere alisema, 'Mimi ningependa vijana wangu wawe wajeuri,' maana yake wajasiri wa kudadisi mambo." Mzee Joseph Butiku, mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu JK Nyerere, alisema, "Utawezaje kuwa seeker of the truth wakati ni mwoga? Hatutaki watu cowards, tunataka watu jasiri, uncompromised (watu wasiorubuniwa)."

Profesa Issa Shivji alisema, "Ukitaka mabadiliko, ukisifia tu mambo huwezi kuleta mabadiliko kwa sababu utakuwa umejitosheleza. Huna haja ya mabadiliko. Tukitaka kuleta mabadiliko, lazima tudadisi. Huwezi ukazaa makasuku tu, makasuku pia wanaweza kuimba. Haitakiwi wataalamu kuwa waoga."

Tukisoma Maandiko ya Biblia Takatifu Mathayo 10:28, maandiko matakatifu ya Mungu wetu yanasema, "Msiwaogope wauao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanamu."

Tukisoma Maandiko ya Biblia Takatifu Mhubiri 9:16, maandiko matakatifu ya Mungu wetu yanasema, "Ndipo niliposema, bora hekima kuliko nguvu; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi."

Wanaccm wenzangu, nayaandika yote haya kuwajengea moyo wa ujasiri kila mmoja wetu kwa nafasi yake kusimama imara na kuelezea na kuyapigania yale anayoyaamini yanaweza kuwa na tija kwa maslahi ya CCM. Tuache kutanguliza hasira za kipumbavu kwenye mambo ya msingi yenye mitazamo ya kukiimarisha chama na kuondoa changamoto zilizopo.

Tukisoma maandiko ya Biblia Takatifu Mhubiri 7:9, maandiko matakatifu ya Mungu wetu yanasema, "Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, maana hasira hukaa kifua cha wapumbavu."

Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli, sherehe za Uhuru Mwanza tarehe 09/12/2019 alisema, "Napenda niseme ukweli ndugu zangu kama mwanadamu."

Wanaccm wenzangu naamini kwa sasa tupo wanaccm takribani million kumi na sita (16), nafahamu uhai wa chama ni wanachama. Ipo haja ya kufuata miongozo yetu pasipo kuikiuka ili kuweza kupata wanaccm wenye moyo wa dhati ya kweli katika kupambania chama chetu. Tujikite kwenye ubora unaokidhi viwango kiutaratibu wa kisheria tulizojiwekea kuliko kuziviza.

Tunapozivunja taratibu zetu za kisheria kuhusu uingizaji wa wanachama, matokeo yake ni mabaya kwani tunakuwa tunaruhusu kunguni, inzi, na mende kuingia ndani ya CCM, na matokeo yake tumejikuta na changamoto nyingi zisizo na utatuzi. Badala ya kuumiza vichwa vyetu kuzitafutia ufumbuzi, tumejikuta watu wa kusifu kila jambo hata kama ni jambo la hovyo. Kujipendekeza nako kumeshika kasi. Mtu anaujua ukweli ila hawezi kuusema kwa kuogopa kuchukiwa.

Tukisoma kitabu cha Tujisahihishe uk 18 - 19, Mwl JK Nyerere anatukumbusha, "Makosa huzinyima akili uhuru wa kufanya kazi yake barabara. Huwa kama kutu inayozuia chombo kufanya kazi yake vizuri au kama uchafu unaokizuia kioo kuona vizuri. Ni wajibu wetu kujitahidi kadri iwezekanavyo kuzipa akili zetu uhuru wa kufanya kazi bila kutu au uchafu wa aina yoyote."

Tukisoma kitabu cha Mwongozo wa CCM 1981 uk 26-27 kifungu 37, maandiko ya Mwongozo yanatukumbusha kwamba "Mwanaccm ndiyo askari wa mstari wa mbele wa mapambano ya kujenga Ujamaa." Naamini wanaccm tulivyo tuna uwezo mkubwa wa kufanya mambo makubwa zaidi, endapo kwa umoja wetu tutaaamua kupambana na changamoto zinazotufanya kuwa na manung'uniko na matokeo yake tunazalisha chuki, unafiki, fitna, na majungu pasipo kukaa na kutafuta njia za kuziondoa changamoto hizo. Tufuate sheria zetu kwenye uingizaji wa wanaccm wapya ili tujiepushe na kuongeza kuwaingiza maadui wasio na nia njema na CCM wanaokuwa vyanzo vya migogoro kila kona.

Tukisoma katiba ya CCM 1977 toleo 2017 uk 06-07 ibara 9-12, maandiko haya ya katiba yamefafanua wazi utaratibu wa kufuata ili kuwavuna wanaccm, ila ni kwa bahati mbaya sana katiba yetu inakanyagwa na kuvizwa kwa makusudi na baadhi ya wanaccm miongoni mwetu. Na matokeo ya kuiviza katiba kunatokea migogoro mingi, ila wanaotupiwa lawama ni watu wa chini, wakati makosa haya ya uvunjifu wa katiba yanafanywa na wale walio kidogo juu yetu. Tabia hii haiko sawa kwani inawonea wanyonge walio chini. CCM kwa sasa tuna wasomi wa kila nyaja, hatuhitaji wingi wa wanachama, tunahitaji ubora wa wanachama, ile tabia ya makokoro inatuletea watu wasio waaminifu na wasio waadilifu, wenye maslahi binafsi wachumia tumbo wasio wajali wenzao. Tubadilike tufuate sheria zetu. Tusizitumie sheria zetu kibaguzi kuwahukumu tu wanyonge wasio na watetezi, huku wavunjaji wa katiba zetu wakilindwa kwa nguvu zote, huu ni ubaguzi na upendeleo uliokatazwa na katiba zetu.

Tuendelee kusoma kitabu cha Azimio la Arusha na kitabu cha Mwongozo wa CCM 1981 tuyachukue yote yaliyo mazuri, kwani vitabu hivi vilipochapishwa, Baba wa Taifa alikuwapo na huku ndiko kumuenzi Mwl. JK Nyerere kwa kufuata maandiko.

Dkt. Bashiru Ally Kakurwa akiwa Kilosa 16/04/2019 alisema, "Ujumbe wangu lazima tusimamie Azimio la Arusha bila woga, hii ndiyo salama yetu CCM kubaki madarakani."

Tukisoma kitabu cha Mwongozo wa CCM 1981 uk 122 kifungu 134, maandiko ya Mwongozo yanatukumbusha, "Azimio la Arusha linasisitiza juu ya ubora wa wanachama badala ya wingi wa wanachama."

Tukisoma kitabu cha Azimio la Arusha uk 38, maandiko yanasema, "Halmashauri Kuu ya Taifa ilikutana Community Centre ya Arusha kuanzia Tarehe 26/01/1967 hadi 29/01/1967.

Tukisoma tena kitabu cha Azimio la Arusha uk 37 maandiko yanatuelezea, "Tangu chama kilipoanzishwa, tumethamini sana kuwa na wanachama wengi iwezekanavyo. Hii ilifaa wakati wa kupigania vita vya kumng'oa mkoloni. Hivyo ndivyo ilivyobidi TANU kufanya kwa wakati huo. Lakini sasa Halmashauri Kuu inaona kuwa wakati umefika wa kutilia mkazo kwenye imani ya Chama chetu na siasa yake ya Ujamaa."

Tukisoma kitabu cha Mwongozo wa CCM 1981 uk 142 kifungu 164, maandiko ya Mwongozo yanatukumbusha, "Mwanachama wa CCM kwa mujibu wa Mwongozo huu atapimwa kwa vitendo vyake vya kutekeleza siasa ya Chama katika maisha yake ya kila siku."

Gazeti la TAZAMA la tarehe 7-13/01/2020 uk 12 liliandika, "Mwaka 1992 lilivunjwa Azimio la Arusha na kuzaliwa kwa Azimio la Zanzibar na hapo ndipo Mzee Mwinyi alifungua milango na madirisha wakaingia mpaka inzi, mbu, mende, na kunguni ndani ya nyumba, wakapitia milangoni na wengine madirishani."

Tukisoma kitabu cha nukuu za Kiswahili za Mwalimu uk 16:

Mwl JK Nyerere aliwahi kusema, "Halmashauri kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo, maana si sera yao. Ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa hila na "janja janja" na mpaka sasa wanaendelea kudanganya wananchi kuwa sera ya CCM bado ni ya ujamaa na kujitegemea." Wanaccm wenzangu, tupende kujisomea na kujielimisha ili inapobidi kujenga hoja tuwe na uelewa mpana ili tukatae kuburuzwa na kuamrishwa mambo ambayo ni kinyume na katiba zetu.

Tukisoma kitabu cha nukuu za Kiswahili za Mwalimu uk 25:
Mwl JK Nyerere alisema, "Mtu yeyote mwenye akili akikupa mawazo ya kipumbavu na wewe una akili na unajua ni ya kipumbavu na ukayakubali, anakudharau. Sasa hatuwezi tukakubali mambo ya kipumbavu Tanzania."

Niwaombe Wanaccm na Watanzania wenzangu, tubadilike kimtazamo, tuache kutumiwa na kufanywa vikaragosi, vibaraka na vijibwa vya wajanja fulani. Tuamshe fikra zetu, tuumize bongo zetu kutafakari, tuwe wadadisi kuliko wasifiaji na watu wa kujipendekeza, tuamini, tutoe mawazo chanya ili yaweze kumsaidia Rais wetu Comrade John Pombe Joseph Magufuli kulipeleka taifa hili kwenye uchumi wa kati. Katu hatuwezi kufika huko kwa kujiweka rehani fikra zetu na kuwa watu wa kusifia tu na kujipendekeza na kuen-dekeza njaa. Tukatae kutumika kihovyo-hovyo.

Gazeti la Mwananchi la tarehe 25/12/2019 uk 03:
Professor Issa Shivji alisema, "Fikra ndiyo uhali wa binadamu, si uhai wa mwili, ni uhai kama binadamu."
Tukisoma maandiko matakatifu kitabu cha Fadhila za Dhikri uk 215:

Maandiko matakatifu yanatukumbusha, "Hakika kusikia, na kuona, na uwezo wa kufikiri, yote hayo yatakwenda kuulizwa." Wanaccm, tusimame imara japo tunajua mtu akiwa msema kweli hata kwenye vikao fulani huwa ni mtu wa kwanza kufyekwa. Tusiogope, Mungu wetu atatushindia. Tubarikiwe soote.

USSR
 
Back
Top Bottom