Sasa ni dhahiri kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaendelea kuipa dunia ya leo changamoto zisizo na kifani. El nino tayari imeanza kuleta madhara kwenye baadhi ya nchi na uharibifu wa mazao unatarajiwa kuleta uhaba wa chakula na bila shaka ongezeko la bei ya chakula hususan katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la sahara. Kwa wale wanaotegemea kushuka kwa mfumuko wa bei ambao kwa kiasi kikubwa unaendeshwa na bei za vyakula, basi watakuwa na muda mrefu sana wa kusubiri. Aidha mvua nyingi zinazotarajiwa kunyesha zinatarajiwa kuleta madhara makubwa kwa miundo mbinu yetu hafifu na dhaifu, jambo ambalo litaleta ongezeko la gharama za usafirishaji. Haya ni mambo tunayoyajua hivi sasa kuwa yana yumkini kubwa kutokea. Swali ni kwamba mawaziri hawa wapya na hasa wale wanaohusika na kilimo, miundombinu wamejipangaje kutuongoza katika changamoto hizi, na kupunguza athari kwa wananchi wa Tanzania kwa kiasi kikubwa kama si kuziondoa kabisa?