muziki wetu unapotea | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

muziki wetu unapotea

Discussion in 'Entertainment' started by kilimasera, May 18, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  May 18, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  MARA nyingi nimekuwa nikijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu pale ninapowasikia watu ambao naamini hasa ni mashabiki wa muziki wa dansi wakilalamika juu ya kupotea kwa muziki huo, licha ya kuwepo kwa bendi ambazo zinajinadi kupiga aina hiyo ya muziki hivi sasa.

  Pengine wafuatialiji hasa wa muziki huu wanaweza kutambua ukweli wa jambo hili hasa kwa kulinganisha zama hizi na zile za Dar International, Moro Jazz, Cuban Marimba Bend ,Kimulimuli JKT, Tabora Jazz, Nyanyembe Jazz na nyingine nyingi ambapo wanamuziki mahiri kama Marijani Rajabu, Mbaraka Mwinshehe, Juma Ubao,Salum Abdalah, walitamba na kuufanya muziki wa Tanzania kujulikana kimataifa.

  Jambo la kujiuliza hapa ni kwa nini muziki wetu wakati huo ulikuwa unakubalika na jamii yote licha ya kuwa kulikuwa na upinzani mkali kutoka kwa muziki wa Zaire (sasa DRC Congo) ambayo nayo wakati huo ilikuwa na wanamuziki vigogo kama Tabu Ley, Luambo Lwanzo Makiadi (Franco) , Abeti Maskini, Mbilia Mbel, Mpongo Love, n.k.

  Ukweli wa hili utaujua ukigundua kuwa wanamuziki wa Tanzania kipindi hicho walikuwa hawapendi kuiga kutoka kwa wageni badala yake walisimama imara kupiga na kuulinda muziki wao, ndiyo maana ilikuwa vigumu kutekwa kimuziki na wageni.

  Ukirudi nyuma kidogo miaka ya 80 na 90 kulikuwa na msururu wa bendi za muziki huo hapa nchini ambapo licha ya wingi wake, zilisimama imara na kuendelea kutangaza muziki huu kimataifa zaidi ya ilivyokuwa mwanzo.

  Hakuna asiyefahamu ubora wa Bendi za Vijana Jazz wakati huo ikiwa na Hemed Maneti , Super Matimila chini ya gwiji la muziki Dk Remmy Ongara, DDC Mlimani Park ya Cosmas Chidumule, Juwata Jazz ya TX Moshi William, Tancut Almasi ya Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, Bima Lee ya kina Jerry Nashon ‘Dudumizi’ n.k, bendi ambazo kila moja ilipiga muziki wa dansi wa Tanzania kwa mtindo wa wake lakini bado ukawa juu kuliko ule wa kutoka nje.

  Lengo letu hapa si kuzitaja bendi hizo lakini kiukweli nyingi kati ya hizo zilikuwa hazifanyi hata matangazo ya barabarani, lakini wapenzi wake walikuwa wanajua mahali ambapo zilikuwa zinafanya maonyesho na kwenda kufurahia burudani ya muziki halisi wa dansi ambao leo haupo tena.

  Iko wapi leo Njata Njata , au ni wapi iliko Mwenge Jazz ‘Paselepaa’, Bantu Group ‘Kasimbagu’, Tancut Almas ‘Kinyekinye kisonzo’ ni wazi ukikumbuka haya kama ulikuwa mpenzi wa kweli wa burudani wakati huo lazima chozi litakutoka hasa ukiiona Sikinde ya sasa iliyobaki jina tu, huku ikishuhudiwa muziki wake kumezwa na aina ya muziki kutoka Congo DRC.

  Kwa sasa asilimia kubwa muziki wa Tanzania imemezwa na muziki wa Kikongo, kwani kila bendi hivi sasa baada ya wimbo kuisha kinachofuata ni rap ambazo zinachukua nafasi kubwa huku zikiwa hazina ujumbe wowote zaidi ya kusifia watu

  Hii ni tofauti na siku za nyuma ambapo mbali na kupata wimbo wenye mashairi mazuri yenye mafunzo kilichokuwa kinafuta baada ya wimbo kumalizika ni kuachia ufundi wa wapiga vyombo kumalizia burudani na kuwafanya mashabiki walioshiba ujumbe vichwani mwao kujimwaga ukumbini kuserebuka.

  Hakika hii ilikuwa maana halisi ya dansi. Hebu tuambizane ukweli ni nani ama ni bendi ipi leo inafanya haya niende ukumbi gani ambapo sitakutana na makelele ya rapu za kumsifia mfanyabiashara fulani wa magari ambaye hana anachokijua katika muziki zaidi ya kumwaga hela ukumbini ah ah! Kazi kwenu mnaojiita vijana!

  Hakika miaka hiyo ilikuwa ya ukweli kwa dansi la Tanzania kwani mbali na ubora wa bendi na wanamuziki waliokuwa hodari wa utunzi na upigaji vyombo wakati huo pia kulikuwa na Mashindano ya kutafuta bendi bora Tanzania yaliyojulikana kama (MASHIBBOTA), mashindano ambayo kwa kiasi fulani yalikuwa nguzo ya muziki huo ambayo kwa sasa yamebaki historia.

  Kutokufanyika ama kufa kwa mashindano hayo ulikuwa ni mwanzo wa kupotea kwa baadhi ya bendi zetu ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa zinategemea mashindano hayo kujiimarisha.

  Kwa mfano katika mashindano hayo kila bendi ilipiga wimbo wake yenyewe na miwili iliyochaguliwa na waandaaji. Hii ilisaidia kila bendi kuonyesha umahiri wake katika utunzi wa mashairi na upigaji wa muziki wa uhakika.

  Huu ni ukweli ulio wazi kuwa mashindano hayo yalisaidia kwa kiasi kikubwa bendi kuweza kuwatunza wanamuziki wake kwa kujua kuwa kupoteza wanamuziki kila mara kulikuwa kunaua uwezo wa bendi na hatimaye kufanya vibaya kwenye mashindano hayo jambo ambalo hakuna aliyelitaka.


  Ukifuatilia kiundani zaidi unaweza kuona utofauti uliopo hivi sasa kwani wanamuziki wa sasa licha ya kuonekana kukosa ubunifu wamekuwa wakihamahama hovyo kutoka bendi moja hadi nyingine. Hii imefanya wanamuziki wengi washindwe kufanya kazi nzuri kwa vile hawana uhakika wa kukaa sehemu kwa muda mrefu na kuwafanya wafanye kazi ya zima moto.

  Kwa maana hiyo ni vigumu kuandaa mashindano ya bendi bora za muziki wa dansi Tanzania wakati bendi zilizopo ziko nje na uhalisia wa muziki wa dansi wa asili ya nchi hii.


  “Nyimbo za sasa kama Big G, ukiila leo kesho huna hamu nayo tena ndiyo maana mimi mpaka leo napenda kusiliza nyimbo za zamani kama ‘Rangi ya Chungwa’ ambazo hata baada ya miaka mia naamini bado zitakuwa bora,” alisema shabiki mmoja mkazi wa kinondoni jijini Dar es Salaam.

  Kauli ya jamaa huyu inaongezea swali lingine kichwani hii inakuwaje kwa nini watu wapende nyimbo za zamani zaidi baadae nagundua kuwa tabia ya wanamuziki wa sasa wa Tanzania kusubiri kuiga kutoka kwa Wakongo ndiyo inayowakera watu na kuona muziki wao umepotea. Ukweli jambo hili ndiyo hasa kaburi la muziki huo.


  “Siku hizi kaka ni kama hatuna bendi wala wanamuziki kwani waliopo wanasubiri kwanza Wakongo waimbe halafu wao wafuatishe kwa kugeuza baadhi ya vitu, hii inatupa wakati mgumu sana mashabiki lakini kwa sababu hatuna sehemu ya kwenda inabidi twende hivyo hivyo,” alisema Seif Juma, mkazi wa keko jijini Dar es Salam nilipokutanae kwenye ukumbi mmoja wa burudani.

  Ukiyatizama kiundani madai ya Seif unaweza kukubaliana naye kwani kipindi hicho wanamuziki hata kama walikuwa wanataka kutupiana madongo ilikuwa vigumu kwa mtu wa kawaida kugundua kutokana na utunzi makini uliokuwepo zama hizo tofauti na sasa ambapo watu wanatukanana waziwazi.

  Kwa mfano wimbo wa ‘MV Mapenzi’ namba 2 wa DDC Mlimani Park ulitungwa kiufundi na kuimbwa kwa kuwatupia kijembe wanamuziki kadhaa walioamua kuikacha bendi hiyo na kwenda sehemu nyingine.

  Mbali na huo wimbo wa ‘Nimekusamehe Lakini Sitasahau’ wa Commando Hamza Kalala alioumba akiwa na Washirika Tanzania Star ‘Watunjata njata’, mbali na kuwa na mafunzo kwa jamii lakini pia alikuwa akirudisha majibu ya madongo aliyotupiwa na hayati Hemed Maneti kufuatia ugomvi ulioibuka baina yao na hatimaye Kalala kujiengua Vijana Jazz kwenda mmoja wa wanzilishi wa kundi la Washirika Tanzania Stars sambamba na Marehemu Eddy Shegy, Adamu Bakari “Sauti ya Zege’ na Abdul Salvador Father Kidevu.

  Kuzaliwa kwa Bendi za Washirika Tanzania Star, Bantu Group, MCA International ‘Munisandesa’, na nyingine nyingi ulikuwa ni msumari mwingine wa watu waliokuwa na nia mbaya na muziki huu wakati huo.

  Nyimbo kama ‘Julie’ ‘Baba Jeni’ ‘Nalila Masumanda’ Shakaza’ Penzi la kusuasua’ ulioimbwa na ‘gwiji la sauti’ Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ na nyingine ziliendelea kuwaficha wageni ambao nao wakati huo walikuwa na harakati kali za kupenyeza muziki wao kwetu.

  Mbali na kukosekana watunzi wa nyimbo zilizo bora pia muziki wa sasa umepoteza uasili, kwa vifaa vingi vinavyo beba jina la jazz kutokutumiwa tena , kwa mfano sasa hivi bendi nyingi zimekuwa havitumii saksafoni,trampeti ama tarumbeta, vitu ambavyo vilikuwa vinaongeza utamu wa muziki wa dansi.

  Hebu kumbuka enzi hizi za La Paloma Jazz, Cuban Marimba, Morogoro Jazz, Les Cubano, Vina vina Orchestra, Sukari Jazz, Kilombero Jazz, Malinyi Jazz, Kwiro Jazz, Mahenge Jazz, Kilosa Jazz, Les Cuban Atomic Jazz, Jamhuri Jazz, Tanga International, Amboni Jazz, Bandari Jazz, Watangatanga, Lucky Star, Black Star hizi zote zikiwa ni kutoka mikoa ya Tanga na Morogoro pekee lakini zilikuwa zinatamba na kujulikana nchi nzima.

  Kwa wewe msomaji na shabiki wa sasa ukitaka kujua umuhimu wa tarumbeta katika muziki hebu sikiliza wimbo wa Hayati TX Moshi William uitwao ‘Nyabasi mwana ngoreme’ kazi aliyoifanya akiwa na Juwata Jazz hapo utaelewa maana ya kile unachokisoma hapa na utaona tofauti ya kusikiliza muziki huo na ule unaopigwa na bendi za sasa ambao kwa asilimia kubwa ni wa aina moja.

  Usikose makala hii juma lijalo ili tuzidi kuona na kutafuta ukweli kuhusu muziki wa dansi wa Tanzania

  Kwa maoni nicheki hapa

  dismaten@gmail.com, ama 0712078264.
   
Loading...