Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,285
MUUNGANO WETU NA NENO.
1
Neno limeota meno, lajazua tafarani,
Siyaoni mapatano, sote vipembe kichwani,
Mwana ashikwe mkono, asipotee njiani,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
2
Hakika nimekubali, heshima kwa muungano,
Usitafute kibali, hubiri utengamano,
Tuwashinde majahili, wanotaka utengano,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
3
Hekima zao wahenga, zimenikumbusha mbali,
Zanifikirisha ngenga, za wenzetu majahili,
Wanawaza kujitenga, sasa wamekuwa nduli,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
4
Niambie yafaani, maneno ya utengano,
Liwapi yenye thamani, nataka yako maono,
Zanzibar ya Sultani, au wetu Muungano?
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
5
Zanzibar si thamani, kuuzidi muungano,
Tanganyika izikeni, hatutaki utengano,
Mipaka ya wakoloni, isilete mapambano,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno,
6
Tanganyika ni Berlini, ni zao la wakoloni,
Zenj mno ithamini, ni fahari ya Sultani,
Tanzania ya Amani, na Nyerere tambueni,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
7
Tanzania imefuta, mipaka ya wakoloni,
Pomoya imetuleta, wa bara na visiwani,
Waasisi mwawateta, mna wazimu rasini?
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
8
Kila nikiyatazama, naona yako na meno,
Na kinywa mmehasama, ndimi kama msumeno,
Chombo chaenda mrama, yaacheni mabishano
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
9
Kiongozi huongoza, watu wakamfuata,
Tena huyasikiliza, yanoleta vutavuta,
Kwa hekima huyamaliza, bila kuwata utata
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
10
Mtawala hutawala, wananchi wakaogopa,
Akisema nyote lala, kitandani wajitupa,
Sasa wachoke kulala, wababe hutapatapa,
Halikidhi mahitaji, neno likiota meno.
Dotto Rangimoto Chamchua.(Njano5)
whatsapp/call 0622845394 Morogoro