Mustakabali bora wa taifa ni watu wenye mwono sahihi

Mustakabali bora wa taifa ni watu wenye mwono sahihi

philosophy

Senior Member
Joined
Nov 11, 2012
Posts
104
Reaction score
42
MUSTAKABALI BORA WA TAIFA NI WATU WENYE MWONO SAHIHI

​
Kwa kila kitu au jambo lililopo, huwa halipo si tu lipo, bali lipo si kutoka kusikokuwepo, lipo kwa chanzo au sababu maalumu. Ndivyo ilivyo kwa vitu vyote ulimwenguni kuanzia kiwango cha chini kabiasa katika mlolongo wa uwepo hadi ngazi ya juu ya huwepo. Usababisho huu pia huelezeka katika uwepo wa binadamu na mambo yote yanayomhusu binadamu. Kwa maana hiyo, kama matokeo ni mabaya basi chanzo chake ni ubaya; na kama matokeo ni mazuri chanzo chake ni uzuri wenyewe. Kanuni hii inatupeleka katika hitimisho la kuwa kila matokeo huwa yanatokana na chanzo fulani, ikiwa ni kwamba chanzo kizuri au kibaya matokeo yake huaksi chanzo hicho.

Binadamu hufasiliwa kama kiumbe au mnyama mwenye akili na utashi kwa mujibu wa mwanafikara wa kipindi cha kati, Boethius. Lakini fasili hili imekuwa ndio nyenzo thabiti ya kumjua na kumweleza binadamu. Hivyo, akili humsaidia binadamu kufikiri, kuchambua na kutafakari mambo kwa kina na kwa ufasha na kuibuka na hitimisho juu ya hayo mambo, wakati huo, utashi ndio humsaidia binadamu kuchagua kile kilicho chema na bora ili kutimiza azma ya kupata furaha. Shughuli hii ndio humofautisha mtu na viumbe wengine.

Kwa kuwa kila binadamu utamani na kupenda kilicho bora na kizuri, ili aweze kuipata furaha. Basi msukumo huo humsababisha binadamu kuipenda na kuitafuta furaha. Kumbe, kila akifanyacho binadamu lengo lake ni kupata furaha. Kwa hiyo, binadamu huitafuta furaha kwa mwongozo wa akili yake mwenyewe. Na kwa kuwa kila akitendacho mtu huongozwa na akili yake, basi akili ya binadamu humpeleka mtu katika kutafuta furaha, na furaha hiyo huletwa na mambo mema tu. Kwahiyo, binadamu ni sharti afanye mambo mema tu ile aweze kupata ile furaha.

Hitimisho hili linatupeleka kuona ukweli katika kauli ya Socrates, kuwa "kujua mema ni kuyatenda, kinyume chake ni ujinga." Kwa hiyo maendeleo kwa binadamu ni mema na mazuri hivyo, ndio maana binadamu huhangaika kupata maendeleo.

Kwa watu wenye kutumia vema akili zao na utashi husahwishika kutenda yale ayaliyo mema ili wapate furaha ya maisha, na hivyo, kwa kuwa wanaujua ukweli huo, hakika hawatachoka kuzitafuta mbinu bora ili kuleta maendeleo kuanzia ngazi ya mtu binafsi hadi taifa kwa ujumla. Mahitaji yote ya binadamu na haki zabinadamu kutimizwa ni jambo jema. Kwa hiyo, elimu na mambo mengine humhusu binadamu kwa kumsaidia kupata maendeleo katika kila nyanja yoyote ya maisha. Kwa maana hiyo, maendeleo yafamilia, kijiji hadi taifa huletwa na watu wenye mwanga huo wa elimu ongozi ndani yake. Kinyume chake itakuwa ni sahihi.

Watu waliokomboleka kifikra, hutambua vema kabisa wajibu wao, ambao ni kutenda yale yanayotakiwa. Yale yanayotakiwa ni yele yaliyomema tu. Kwa kuwa kila mtu atakuwa amekomboleka kifikra, na ana maarifa ongozi ndani yake, basi mtu huyo atakuwa ana ufahamu wa kwamba anatakiwa kutenda mambo mema tu na kuzuia yale maovu. Ni kwa sababu yale mema yatampeleka kwenye kilele cha dhaimira yake ambayo ni kupata furaha ya maisha. Na kutenda maovu hakutompeleka katika dhamira yake. Kuendelea kwa njia yoyote ile, iwe ni ya ndani au nje ni jambo zuri na jema, hivyo, binadamu hatolipuuzi na atafanya kila jitihada kuhakikisha anafanya mambo mema yatakayompeleka kwenye maendeleo. Ndivyo ilivyo, kwa kuanzia na mtu mmoja mmoja kinafsi hadi taifa kwa ujumla.

Kwa sababu wanajumuiya hao, wamekwishakujua kuwa wema tu ndio unaoleta maendeleo yao yeyenye kuwapeleka katika furaha ya maisha yao, basi hawatokuwa tayari kumwona mpuuzi yeyote kati yao anafanya kinyume. Watakuwa tayari kumkemea au kuweka miongozo (kanuni/sheria) zitakazo waongoza kulinda utu wao kwa kutokizichafua dhamiri zao. Matokeo yake ni taratibu, miongozo, kanuni, sheria n.k ili kulinda matendo ya wanajumuiya hao. Sheria ama matamko hayo ya kisheria, tayari huwa ndio mwongozo kwa kila mwanajumuiya, na hivyo, hata pale wanapozitambua haki zao na kuamua kuzilinda, basi huamua kukubaliana na kuweka mkataba, kama Hobbes na Locke, wanavyoita kuwa ni mkataba wa kijamii. Mkataba huu huwachagua viongozi wenye kusimamia huo mkataba na kuulinda kwa maslai ya kuzilinda na kizihakikisha haki za rai hao.

Kwa maana hiyo, taifa la namna hiyo, huwa na viongozi ambao wametokana na jumuiya yenye watu wenye elimu ya juu kuhusu maisha, maadili, na umuhimu wa kuheshimu utu wa mtu, hivyo, kwa kuwa hawa viongozi wanayo elimu ongozi yenye ukombozi wa fikra ndani yao, basi watasimamia vema maslai ya taifa kwa manufaa ya taifa zima na taifa hilo huwa na maendeleo. Watafanya chini juu kuhakikisha wanalinda haki za raia wao na kupiga marufuku ukiukwaji wa haki hizo, huku wakiwa wabunifu kubuni mipango bora yenye kuleta manufaa kwa taifa lao. Viongozi hawa wametokana na jamii bora inayofuata utu, iliyoelimika na kuuona ukweli kwa undani wake, jamii yenye kutokukubali dhuluma yoyote inayoweza kulipeleka taifa katika utata wa kimaisha kwa namna yoyote ile; basi viongozi hao hawaezi kukengeuka kwa ajili ya maslai yao, kinyume chake watakuwa ni wasaliti wa msingi wao wa jamii ama watakuwa hawajaelimika kuhusu utu na maisha.

Palto, mwanafalsafa wa kipindi cha kale, alipendekeza katika falsafa yake ya uongozi/siasa kuwa, jamii au taifa inabidi liongozwe na "mwanafalsafa mfalme." Kwake yeye huyu kiongozi ni yule mwenye elimu ya juu sana ya maisha, ana uelewa wa mambo kwa ukiini wake, anajua jamii anayoiongoza inataka nini na inakosa nini…..na hivyo kwa kuwa anao ufundi wa uongozi ndani yake, hakika mwanafalsafa mfalme ataweza kuipeleka au kuiongoza jamii yake katika kilele cha mafanikio.

Hakika mawazo haya ya Plato yana ukweli mkubwa ndani yake. Nachoweza kuongezea kwake ni kuwa kiongozi wa namna hii hawezi kutokea kwa bahati bali yeye ni zao la jamii inayoaksi vigezo vya kiongozi huyo alivyotaja Plato. Kwa sababu ni zao la jamii yake iliyokomboleka kwa fikra na muono wa ndani kwa raia wake, basi kiongozi huyo atakuwa anaifahamu vema na kwa kina jamii yake na hivyo, kwa moyo wote wa uzalendo juu ya jamii yake na kwa kuwa ana elimu ya juu ya maisha, hatokuwa tayari kujipendelea au kupuuzia ukikwaji wa haki na dhuluma za haki za rai anaowaongoza. Huyu ndiye kiongozi bora kwa taifa bora ambaye uwepo wake ni jamii bora yenye ung'amuzi maridhawa kuhusu ukweli wa maisha na utu. Kwa hiyo hatima ya taifa bora itakuwa ni watu bora wenye mwono sahihi.
 
Back
Top Bottom