Mufti ataka Ramadhani itumike kuombea amani

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
WAKATI Waislamu duniani kote wakitarajia kuanza kutekeleza moja ya nguzo tano za dini yao kwa kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limewataka Waislamu nchini kutumia mwezi huo, kuombea amani na utulivu.

Aidha, wametakiwa kuhimizana kufanya kazi hasa katika kipindi hiki ili kupata riziki za halali kama kaulimbiu ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’ inavyosema kwa kaulimbiu hiyo si tu ni ya Rais, bali ni agizo la Mwenyezi Mungu kupitia kitabu chake Kitakatifu cha Kurani.

Hayo yameelezwa na Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zubeir wakati akizungumza kwenye Kongamano la kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani, lililofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Mufti Zubeir alisema Rais Magufuli anaposema ‘Hapa Kazi Tu’ anakuwa amezungumzia dini moja kwa moja kwani hata katika Kitabu Kitukufu cha Kuran, Mwenyezi Mungu amesema anapendezwa na watu wanaofanya kazi.

“Kwa hiyo watu wahimizane kufanya kazi sana hasa katika kipindi hiki ili kupata riziki halali itakayowawezesha kupata mahitaji yao ya futari na daku,” alisema Mufti Zubeir. Aidha, aliwataka Waislamu kusaidiana ili kila mmoja afurahie mwezi wa Ramadhani.

Alisema mwezi huo ni kama chuo ambacho kila Muislamu anatakiwa kujifunza upendo, kusameheana, kupendana na mambo yote yanayompendeza Mungu. Aliwataka pia kutumia mwezi wa Ramadhani, kufanya sana ibada pamoja na kuomba dua na kuiombea nchi kuwa na amani, utulivu na mshikamano na kumuombea Rais Magfufuli ili Mungu amjaalie hekima na busara.

Naye Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum alisema Waislamu nchini na duniani kote wanatakiwa kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuachana na mambo yanayomkera Mungu na badala yake kuomba msamaha ili wasamewe madhambi yao.

Alisema mwezi huo si tu kwa ajili ya kujizuia kula na kunywa, bali kujizuia katika matendo yote mabaya yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu. “Funga ni tiba ya maradhi lakini pia inafundisha uaminifu na inaimarisha uchamungu, ni ibada ambayo ina siri kubwa sana kati ya mja na Mwenyezi Mungu,” alisema Shehe Alhad.

Aliwataka Waislamu kuendelea kuonesha uaminifu watakaounesha kipindi cha mwezi wa Ramadhani, hata baada ya mwezi huo kuisha kwani kipindi chote wanadamu wanatakiwa kumtii Mwenyezi Mungu.

Aidha, Shehe Alhad aliwasihi wafanyabiashara nchini kote kutopandisha bei bidhaa za vyakula ili kutoa fursa kwa Waislamu wote kupata mahitaji yao ya futari kwa gharama nafuu katika mwezi huo unaoanza leo au kesho.

Chanzo: Habari Leo
 
Back
Top Bottom