Massivve
JF-Expert Member
- Jun 4, 2015
- 274
- 368
Katika aina za Serikali, mojawapo ni Ochlocracy, ambayo maana yake Serikali ya kikundi kidogo kwa maslahi ya wachache. Ochlocracy huitwa pia Mob Rule Government au siku hizi huita Gangster Government.
Ochlocracy ni Serikali ambayo wenye mamlaka hutumia nguvu zao halali za dola kuwaonea raia wa kawaida. Hufanya uonevu huo kwa maslahi ya kundi lile dogo, lakini wakati wakitekeleza uonevu, hujinasibu kuwa wanafanya hivyo kwa maslahi ya umma.
Katika Ochlocracy, sheria huwa haziheshimiwi, isipokuwa amri za viongozi huwa ndiyo sheria. Mtendaji kwenye Serikali anaweza kuvuruga lakini Mkuu wa Nchi akamlinda kwa nguvu zote na mwenye kuchongoa mdomo akakiona cha mtema kuni.
Karne ya Pili, mwaka ukiwa 180 mpaka 192, Roma ilitawaliwa Mtawala aliyeitwa Commodus. Jina lake kamili ni Lucius Aurelius Commodus. Alianza akiwa mtawala mdogo wa Roma mwaka 177, wakati baba yake, Marcus Aurelius akiwa mtawala mkuu.
Mwaka 180, Aurelius alipofariki dunia, Commodus alichukua mamlaka kamili ya kuongoza Roma. Wakati huo utawala wa Roma ulijumuisha eneo lote la kuzunguka Bahari ya Mediterranean kwa Ulaya, vilevile Afrika na Asia. Ndiyo maana Misri na Syria zilikuwa sehemu ya utawala wa Roma.
Utawala wa Commodus ndiyo alama kuu ya Mob Rule Government na aliyesababisha yote ni msaidizi wake aliyeitwa, Marcus Aurelius Cleander, jina maarufu zaidi ni Cleander.
Historia inaonesha kuwa Cleander alikuwa mtumwa. Asili ya Cleander ni dola ya Phrygia ambayo ilikuwa Magharibi Kati ya Anatolia. Hivi sasa Anatolia ndiyo Uturuki.
Cleander aliuzwa Roma akawa mfanyakazi aliyebahatika kufanya kazi kwa Mtawala. Marcus Aurelius ambaye ni baba wa Commodus alimpenda sana Cleander, akamfanya mtoto wa nyumbani, ndiyo maana Cleander majina yake ya mwanzo ni Marcus Aurelius.
Commodus alipoanza kutawala Roma, akiwa mtawala pekee baada ya baba yake kufariki dunia, msaidizi wake wa karibu aliitwa Saoterus. Cleander alikula njama akamuua Saoterus.
Baada ya kifo cha Saoterus ndipo Commodus alimteua Cleander kuwa msaidizi wake. Nafasi hiyo ilimpa nafasi ya kuwa mtendaji mkuu wa Roma, vilevile mlinzi wa rasilimali za Roma.
Kwa nafasi hiyo, Cleander alifanya matukio mengi ya uonevu na uharamia lakini Commodus alimkingia kifua. Commodus alimpenda Cleander na hakutaka kusikia akisemwa vibaya.
Aliwauzia watu useneta wa Roma, alitumia jeshi kunyamazisha kila aliyempinga. Raia wa Roma wakawa wanaishi kwa wasiwasi mkubwa. Waliojaribu kupinga walinyamazishwa na hata kuuawa.
Rasilimali za umma aliuza kama mali yake binafsi, ofisi za Serikali aliweka aliowataka na kuwatoa aliowachukia. Watu walihoji mamlaka hayo alipata wapi? Commodus alikuwa kimya na alipolazimika kusema, alimtetea Cleander.
Juni 190 hali ilikuwa mbaya zaidi, Roma ilikabiliwa na njaa. Mkuu wa ugavi wa chakula na sarafu, Papirius Dionysius, alishusha lawama kwa Cleander kuwa aliuza chakula hovyo kwa ruhusa ya Commodus na alifanya mgawanyo mbaya wa sarafu.
Kutokana na lawama hizo, Seneti ya Roma ilipaza sauti, wananchi walikasirika na kuandamana kumfuata Cleander, maana waliona yeye ndiye tatizo, lakini alikuwa akilindwa na Mtawala wao.
Cleander baada ya kuona anavamiwa, aliagiza jeshi la Roma, Praetorian Guard kuua watu waliokuwa wakiandamana, kisha yeye akakimbilia kwa Commodus kujificha. Watu walimfuata na kumkata kichwa kabla hajafika kwa Commodus.
Habari zilimfikia Commodus ambaye alipokwenda eneo la tukio, alikuta Cleander ameuawa kwa kukatwa kichwa pamoja na mwanaye. Wananchi wa Roma walimwambia Commodus kuwa walimuua Cleander kwa sababu ndiye alikuwa tatizo kwenye utawala wake.
Hata baada ya kifo cha Cleander, wananchi wa Roma waliendelea kutokuwa na imani na Commodus kwa vitendo vyake vya kumwacha Cleander akitumia ukaribu wake na Mtawala kujinufaisha binafsi na kuonea watu waliokuwa hawana hatia.
Desemba 31, 192, mtu anayeitwa Laetus alitengeneza njama iliyohusisha wahudumu wa Commodus, wakampa sumu kwenye chakula. Hata hivyo, Commodus alitapika chakula chote. Wakamtumia mpigana myereka, Narcissus, kumnyonga akiwa bafuni.
Baada ya Commodus kuuawa, Seneti ya Roma ilimtangaza Narcissus kuwa adui wa umma kwa kumuua Mtawala wao. Hata hivyo, watu wengi walifurahi, wakasema Commodus hakuwa mbaya, ila aliwachukiza wengi alipomlinda msaidizi wake Cleander aliyeharibu utawala wake.
Maana yake ni kuwa Mtawala anaweza kuwa mzuri sana, lakini akimlea msaidizi wake ambaye ni tatizo kwa nchi, huvuna hasara kubwa katika utawala wake. Tujifunze kwa Commodus na Cleander.
By Luqman MALOTO