MSUMBIJI: Tume ya uchaguzi imekiri kuwa kuliwepo na dosari kadhaa wakati wa uchaguzi mkuu

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,501
9,280
Tume ya uchaguzi nchini Msumbiji, imekiri kuwa kuliwepo na dosari kadhaa wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, ambapo rais Filipe Nyusi alichaguliwa kwa muhula wa pili.

Kauli hii ya tume imekuja baada ya chama kikuu cha upinzani nchini humo, RENAMO, Jumatano ya wiki hii kufungua kesi katika Mahakama ya Katiba kupinga ushindi wa rais Nyusi, kikitaka uchaguzi huo ufutwe.

Awali kituo cha umma cha masuala ya uadilifu CIP kimetowa ripoti inayosema, uchaguzi huo umekumbwa na taarifa za masanduku kujazwa kura kabla hata ya zoezi la upigaji kura pamoja na kuzuiwa kwa waangalizi kufanya kazi zao.

Chama tawala cha Frelimo kimetuhumiwa kufanya udanganyifu katika orodha ya wapiga kura waliojiandikisha katika ngome zake. Kituo cha CIP pia kinadai yalikuwepo pia majaribio ya kuwazuia waangalizi huru wa uchaguzi kufanya kazi zao kwa kuwanyima vibali vya kuingia kwenye maeneo ya upigaji kura katika mikoa kadhaa.

Kituo cha kusimamia uadilifu CIP kinasema wajumbe wake wameripoti visa vya kutokea jaribio la masanduku ya kura kujazwa kura na kwamba kuna watu kadhaa waliokamatwa wakiwa na karatasi za ziada za kupigia kura ambazo zilikuwa zimeshajazwa jina la chama cha Frelimo na mgombea wake wa urais.

Hatua hii ya upinzani kukataa kutambua matokeo ya uchaguzi huo, kunauweka pabaya mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya Chama tawala FRELIMO na Chama cha RENAMO ambacho kimetokana na waasi wa zamani.

Takwimu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi Nchini Msumbiji zinaonesha kwamba, Rais Nyusi alipata kura asilimia 73% ya kura zote halali zilizopigwa na mpinzani wake Bwana Ossufo Momade wa RENAMO akajinyakulia kura asilimia 22% za kura zote. Upinzani walikataa kukubaliana na matokeo haya kwa misingi kwamba, uchaguzi ulifanyika katika hali ya vitisho pamoja na “wizi wa kura”.

Hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kiliwekeana tena saini Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa.
 
Back
Top Bottom