Msomgamano Dar unalitia taifa hasara ya Sh1.46 trilioni | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Msomgamano Dar unalitia taifa hasara ya Sh1.46 trilioni

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MziziMkavu, Jul 7, 2012.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jul 7, 2012
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,617
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli​

  Florence Majani, Dodoma
  TATIZO la msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam jana lilizua mjadala mkali bungeni wakati wa mjadala wa hotuba ya makadirio ya matumizi ya Wizara ya Ujenzi, huku Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia akisema tatizo hilo hulisababishia taifa hasa ya Sh1.46 trilioni kwa mwaka.

  Miongoni mwa waliojadili kwa undani tatizo hilo ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe ambaye alitaja mbinu saba za kukabiliana na msongamano huo.

  Kadhalika, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi na Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, kwa nyakati tofauti waliitaka Serikali kuchukua hatua za kukopa fedha kwenye benki na taasisi nyingine za fedha ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara wakisema fedha zilizotengwa kwenye bajeti hazitoshelezi.

  Mbatia alisema msongamano huo hauna budi kutafutiwa ufumbuzi mapema kwa kuwa fedha nyingi zinaendelea kupotea huku maendeleo yakididimia.

  “... Muda unapotea na uchafuzi wa mazingira. Kwa kuwa hili ni janga na janga halisubiri kesho, hatuna muda wa kupoteza, tuanze kulishughulikia leo,” alisema na kuongeza kuwa tatizo la msongamano husababishwa na mambo mengi akiitaka Serikali kufanya kazi kama timu... “Waziri wa Ujenzi, Miundombinu, Mawasiliano na Uchukuzi na Waziri wa Utawala Bora, wakae pamoja na kupanga namna ya kutatua msongamano huu jijini.”

  Alisema, Bajeti ya trilioni 1.23 haitoshi kumaliza tatizo la barabara Tanzania, badala yake ujenzi huo utakuwa unakwenda nusunusu na kutofikia malengo kwani kiasi cha bilioni 150 zitatumika katika kulipa madeni.

  Mbinu saba za Mbowe

  Mbowe alisema mbinu zinazoweza kutumika kudhibiti msongamano huo ni kutoza ushuru magari yote yanayoingia katikati ya jiji na ya kibiashara kama vile Posta Mpya, Kariakoo na Mwenge.

  Alisema mbali na kusaidia kupunguza msongamano wa magari, hatua hiyo itaziwezesha mamlaka husika kukusanya mapato ambayo yatatumika kuimarisha miundombinu katika maeneo hayo.

  “Haya maeneo ya kibiashara yaliyo katikati ya miji ni kitovu cha miji na kwa kawaida yana idadi kubwa ya watu. Ili kudhibiti msongamano katika maeneo hayo ni lazima tutoze fedha kwa watu kuingia maeneo hayo. Hatutakuwa tumepunguza msongamano pekee, bali tumeongeza na mapato,” alisema.

  Mbowe alisema njia nyingine ni kudhibiti utaratibu wa maegesho ya magari akisema uliopo sasa hauzingatii sheria na umekuwa ukisababisha foleni.

  “Wakati mwingine magari yanapaki (egeshwa) sehemu yoyote bila kujali ni eneo gani la barabara, hili huchangia hata na ajali. Ni lazima tuandae mipango madhubuti ya kudhibiti maegesho haya holela,” alisema.

  Alishauri sehemu za watembea kwa miguu zitengwe tofauti na barabara za vyombo vingine kwa maelezo kwamba barabara zisizozingatia haki ya watembea kwa miguu husababisha matukio mengi ya ajali.

  Pia alipendekeza ujenzi wa madaraja ya juu kama lililopo Manzese ili kuwezesha magari kwenda kasi badala ya kusubiri watembea kwa miguu kuvuka kila baada ya muda mfupi.

  Kuhusu ujenzi wa barabara, Mbowe alisema miradi ya ujenzi imekuwa ikichukua muda mrefu kwa sababu ya ukosefu wa fedha jambo ambalo huligharimu taifa kwa miradi husika kutotumika kwa muda mwafaka.
  Kukopa benki

  Serukamba aliitaka Serikali ikope fedha kwenye benki ili ijenge barabara imara.

  Alisema nchi nyingine kama Kenya na Angola zimefanikiwa katika barabara kwa sababu zilichukua uamuzi mgumu wa kutafuta vyanzo vya fedha ili kuimarisha sekta hiyo.

  “Tukiigemea hii bajeti peke yake, kwa jinsi ilivyo finyu hatuwezi kumaliza barabara kama tunavyotarajiwa, nyingi zitaanza kujengwa na kuishia nusu huku nyingine zikijengwa bila kiwango,” alisema Serukamba.

  Mbunge wa Chonga (CUF), Haroub Mohamed Shamisi aliitaka Serikali kuhakikisha ina punguza tatizo la msongamano jijini kwa kuwa ni sehemu inayochangia mapato kwa asilimia kubwa kuliko miji mingine ya Tanzania.

  Aliitaka Serikali iunde mamlaka maalumu kwa ajili ya kusimamia jiji ili kuondosha rushwa na maslahi binafsi kwa sababu hivi sasa kila eneo lina mamlaka yake.

  “Unafikiri kwa nini Dar haiwi safi? Kuna watu jiji likiwa chafu wao wanapata hela zaidi. Iwepo mamlaka moja tu ya kusimamia matatizo ya jiji,” alisema Shamisi.
  
Alisema kinachoongeza msongamano huo ni ubovu wa barabara za pembezoni ambazo mara nyingi hujaa maji kutokana na miundombinu mibovu.

  Kuhusu barabara, mbunge huyo alisema Serikali haiwezi kukamilisha nyingi kwa fedha zilizotengwa katika bajeti hiyo na badala yake aliitaka kutafuta vyanzo vingine vya mapato...
  “Tukijenga barabara za muda mrefu tutaongeza mapato, kwa sababu jiji hili ni uso wa taifa,” alisema Shamisi.

  Akiwasilisha hotuba yake juzi, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitangaza kutenga fedha kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu (fly overs), kama moja ya hatua za kupambana na msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.

  Kwa ujumla wake, miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo ina thamani ya Sh899.063 bilioni lakini fedha ambazo zimetengwa katika mwaka huu wa fedha ni Sh37.578 bilioni tu sawa na asilimia 4.17 tu ya mahitaji hayo.

  Dk Magufuli alisema maandalizi ya ujenzi wa barabara za juu ambazo zimetengewa fedha za ndani Sh2 bilioni, unatarajia kuanzia katika eneo la Tazara, makutano ya Barabara za Mandela na Nyerere na ujenzi huo utafadhiliwa Serikali ya Japani kupitia Shirika lake la Misaada (JICA).

  Dk Magufuli aliitaja miradi mingine ambayo inalenga kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za pembezoni (ring roads) zenye urefu wa kilometa 98.15.

  Msomgamano Dar unalitia taifa hasara ya Sh1.46 trilioni

  Alisema mpango huo umetengewa Sh3.273 bilioni ambazo zitatumika kukamilisha kazi zilizobakia katika Barabara ya Kituo cha Mabasi Ubungo - Kigogo – mzunguko (round about) ya Kawawa – Bonde la Msimbazi – makutano ya Twiga na Jangwani.
   
Loading...