MMILIKI wa duka la vifaa vya michezo la Urhul lililopo jijini Dar es Salaam, Kassim Dewji, amethibitisha kuwa kwenye michezo ya Ligi Kuu Baramsimu ujao, Bodi ya Ligi itatumia mipira aina ya Adidas Speed Cell Match Ball.
Dewji ambaye ni muuzaji wa vifaa vya michezo kwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) kwa kipindi kirefu, alisema kuwa watatoa mipira ya Adidas Speed Cell Match ambayo ni toleo bora lililofuata mpira wa Adidas Jabulani ambao ulikuwa mpira maarufu kwenye Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
Dewji alilieleza Mwanaspoti akisema: "Mimi si msambazaji wa mipira hiyo, mimi ni muuzaji kama wafanyabiashara wengine wa maduka wanavyofanya. Wasambazaji wa mipira wa TFF wameniagiza mipira ya ‘MatchBall, Speed Cell' ambayo inafanana na Jabulani kimuundo na muonekano wa nje.
"Ni Jabulani iliyoboreshwa zaidi.Hii mipira ni ya kisasa na itakuwa ni ya kwanza na kipekee kwenye ligi yetu. Mpira huo ni saizi namba tano na thamani ya mpira mmoja ni TSh 240,000 na tunapouza huwa tunawapelekea kwenye vituo mbalimbali kama anavyokuwa ameagiza mnunuaji wa mipira hiyo," alisema Dewji.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Silas Mwakibinga alisema:"Bado sijafahamu ni mipira gani haswa itatumika mpaka pale nitakapopewa taarifa na ni ipi imepatikana kwa sasa sifahamu."
Chanzo: MwanaSpoti