Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,042
- 10,787
Kigogo msimamizi Bomoabomoa Dar aanguka ghafla ofisini kwake
Madaktari washindwa kubaini tatizo
Operesheni kubwa ya kubomoa nyumba zaidi ya 15,000 zilizojengwa katika maeneo yasiyostahili jijini Dar es Salaam, imekumbana na changamoto ya aina yake baada ya mmoja wa wasimamizi wa kazi hiyo kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Heche Suguti, kuanguka ghafla akiwa ofisini kwake na kuwahishwa hospitali akiwa hoi.
Chanzo kutoka ndani ya Nemc kimeiambia Nipashe kuwa Suguti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika baraza hilo, alianguka ofisini kwake majira ya saa 9:30 alasiri baada ya kurejea kutoka katika Mahakama Kuu kitengo cha ardhi kushughulikia kesi inayoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi dhidi ya wakazi 681 wa eneo la Mkwajuni, Kinondoni ambao wanapinga nyumba zao kubomolewa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Suguti kuanguka ghafla ofisini kwake eneo la Mikocheni, baadhi ya wafanyakazi wenzake (wa Nemc) walimsaidia haraka kwa kumbeba na kumpakiza kwenye gari na kumpeleka hospitali mbili tofauti ambako kote vipimo vya awali havikubaini tatizo.
“Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alilazwa kuanzia siku hiyo (Jumanne) na kutolewa leo asubuhi (jana) baada ya kupata nafuu… ila kwa kifupi ni kwamba afya yake imeyumba na hadi sasa madaktari bado wanachunguza kujua ni kitu gani hasa kinachomsumbua,” chanzo kiliiambia Nipashe jana.
Mkurugenzi wa Nemc, Bonaventure Baya, alikiri kuwa Suguti aliugua baada ya kuanguka ofisini Jumanne wiki hii na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan, lakini haoni kama ni sahihi kuzungumzia afya yake kwani hayo ni masuala binafsi.
“Nadhani ni uchovu ndiyo uliokuwa unamsumbua… hata hivyo, hayo ni masuala binafsi.
SUGUTI ANENA
Alipotafutwa kwa njia ya simu jana mchana, Suguti aliyekuwa akizungumza kwa taabu, alikiri kupatwa na tatizo asilolifahamu na kuanguka ofisini kabla ya kujikuta akiwa amelazwa katika wodi mojawapo ya Hospitali ya Aga Khan.
“Kwakweli sielewi kilichotokea. Nilipoingia ofisini kwangu baada ya kutoka kwenye kesi ya nyumba za watu wa Kinondoni, ghafla nikahisi kizunguzungu, giza kutanda na mwishowe nikaanguka… Sijui kilichotokea baada ya hapo ila fahamu ziliponirudia nikajikuta nikiwa hospitali,” alisema Suguti.
Alipotakiwa kueleza zaidi kuhusiana na tukio hilo, Suguti hakuwa tayari kwa maelezo kuwa bado hajisikii vizuri.
“Kwa sasa naomba uniache tu, sijisikii kuzungumza zaidi,” alisema na kukata simu.
SIMULIZI ZAIDI KUTOKA NEMC
Baadhi ya watumishi wa Nemc waliozungumza na Nipashe, walisema wamestushwa na tukio hilo kwani halijawahi kutokea hapo kabla kwa Suguti kuanguka ghafla na kuugua kiasi kwamba asijitambue wakati wakimuwahisha hospitali.
Mmoja wa watumishi hao alisema siku hiyo, baada ya kurudi ofisini akitokea mahakamani, Suguti alikuwa mzima wa afya.
“Hata hivyo, ghafla akaanza kulalamika kuwa anajisikia vibaya na muda mfupi baadaye akaishiwa nguvu na kuanguka sakafuni. Tulishtushwa sana, ndipo tukambeba na kumpeleka hospitali,” alisema.
Alisema kuwa awali walimpeleka katika hospitali moja yenye jina kubwa na baada ya kufanyiwa vipimo, majibu yalionyesha kuwa hasumbuliwi na ugonjwa wowote.
Hata hivyo, wakati huo hali ya Suguti bado ilikuwa mbaya na hivyo wakalazimika kumpeleka Hospitali ya Aga Khan.
“Tulipomfikisha Aga Khan, walimpa huduma za awali ikiwa ni pamoja na kumtundikia drip ya maji.
Hata hivyo, hali yake bado haikuwa nzuri na ndipo alipolazwa hadi jana,” kilieleza chanzo hicho na kuongeza:
“Cha kushangaza, bado haijafahamika ni ugonjwa gani hasa unaomsumbua hadi akaanguka ofisini na kuzidiwa kiasi kile. Mmoja wa madaktari alisema hana ugonjwa mwingine isipokuwa dalili za shinikizo la damu.
“Hata hivyo, wengi tumeingiwa na hofu na kuhusisha hali yake na operesheni ya bomoabomoa inayoendelea (jijini Dar es Salaam) huku yeye akiwa msimamizi, ikiwamo katika kazi ya kuziwekea alama za X nyumba zinazostahili kubomolewa kwa kujengwa mahali kusikostahili,” mmoja wa watumishi hao wa Nemc aliiambia Nipashe jana.
Mtumishi mwingine aliongeza: “Tangu tuanze operesheni hii tumekuwa tukipata vitisho vingi kutoka kwa baadhi ya watu wanaoguswa. Hili linatushawishi kuhusisha kuugua ghafla kwa Suguti na kazi tunayofanya… Hata hivyo, wananchi wanapaswa kutambua kuwa sisi ni watekelezaji tu wa sheria. Na tena siyo sisi tunaoamua kuwabomolea.”
Nemc kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam, walianza operesheni ya kuweka alama ya ‘X’ na kubomoa nyumba zilizojengwa kwenye maeneo yasiyostahili yakiwamo ya mabondeni kuanzia Desemba 17, mwaka jana.
NYUMBA 16,000 ZAWEKWA `X’
Zaidi ya nyumba 16,000 zimeshawekwa alama ya X katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ambazo zinatakiwa kubomolewa kutokana na kujengwa maeneo hatarishi.
UBOMOAJI WASITISHWA
Kazi ya kubomoa nyumba hizo imesitishwa kwa siku nne ili kupisha tathmini ya nyumba 681 zilizowekewa pingamizi Mahakama Kuu ya Ardhi kabla ya kuendelea tena kwa nyumba 16,532 zilizowekewa alama ya X hadi jana.
Mkurugenzi wa Nemc, Mhandisi Bonaventure Baya, alilieleza Nipashe kuwa nyumba zilizowekwa X jana katika maeneo ya Gongo la Mboto hadi Pugu ni 885.
“Kazi ya kuweka alama ya X inaendelea kabla hatujaanza kubomoa tena, leo tumeendelea kesho tunahamia maeneo ya Kigogo hadi Ubungo,” alisema.
Kuhusu bomoabomoa iliyosimama kwa siku mbili sasa alisema lengo ni kupisha tathmini ya watu waliokwenda mahakamani kabla ya kuanza tena kubomoa.
Nipashe jana lilipita katika maeneo ya Kigogo Bonde la mto Msimbazi na kushuhudia baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakiwa wameanza kuhama na kubomoa nyumba zao wenyewe.
Juma Mashilingi, mkazi wa Kigogo, alilieleza Nipashe kuwa ameamua kufanya hivyo ili kuipisha serikali kuendelea na azma yake ya kubomoa licha ya kuwa hawana pa kwenda.
“Hatuna namna dada, tutakwenda wapi? Serikali imeshasema ni bora tukaondoka wenyewe kiustaarabu kuliko kubaki na tukapoteza vitu,’ alisema Mashilingi ambaye ni mpangaji kwenye moja ya nyumba za maeneo hayo.
Bomoabomoa hiyo iliyoanza Januari 5 mwaka huu baada ya kusitishwa kwa siku 14, imezikumba nyumba zaidi ya 600 katika eneo la Kinondoni Mkwajuni.
Chanzo: Nipashe
Last edited by a moderator: