Msamaha na viwango vyake hujenga afya, huboresha mapenzi

Msamaha na viwango vyake hujenga afya, huboresha mapenzi

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Joined
Dec 26, 2012
Posts
1,016
Reaction score
2,195
Mambo mawili, moja hatari lingine mateso. Umemtendea mwenzio makosa na hujafanya jitihada za kumaliza tatizo. Huwezi kujua anachokiwaza juu yako. Je, anajipanga kulipiza kisasi? Amesamehe au kupuuzia? Hapo kuna hatari, vilevile mateso ya kujitakia.

Umetendewa kosa, umeumia kwa uliyofanyiwa. Mkosaji haombi msamaha, hivyo kukupa mateso ya hisia. Ile hali ya kukosekana mwafaka kati yako na aliyekukosea, inakuwa sababu ya kupanda kwa kiwango cha hasira ambayo baadaye hugeuka chuki.

Mambo yote hayo mawili, kukosea na kukosewa (kutenda na kutendwa) yana athari kubwa kwa afya yako. Hii ikupe mwongozo wa kutambua umuhimu wa msamaha. Yaani kuwa na uthubutu wa haraka katika kuomba radhi pale unapokosea, vilevile utayari wako wa kusamehe unapoombwa radhi.

Kwa mujibu wa majibu ya utafiti katika somo la maendeleo ya binadamu, Chuo Kikuu cha Madison, WI, msamaha huongoza matokeo ya kuimarika kwa afya ya mwili na akili, zaidi huufanya uhusiano kuwa bora kuliko mwanzoni.

Bila shaka ungependa afya yako iwe nzuri na kwa vile utakuwa mwenye furaha kama uhusiano wako utakuwa bora, hakikisha maneno "Nimekusamehe" au "Naomba unisamehe", yanakuwa siyo magumu kutamka, ila yasiwe wimbo. Kwa nini yasiwe magumu lakini yasiwe wimbo? Nitafafanua.

MAKOSA KATIKA MSAMAHA
Msamaha ni somo pana ambalo huhitaji viwango vyake katika kuufikia. Haiwi tu "naomba unisamehe", mwingine anazungumza kwa kifupi tu "nisamehe", siku hizi Uzungu umekuwa mwingi, kwa hiyo mkosaji anasema "I am sorry." Eti ndiyo tayari mambo yamekwisha.

Mwingine kwa sababu ya kuzidiwa na hisia za mapenzi na heshima kubwa kwa mwenzi wake, anajikuta anatoa msamaha bila kuombwa au pasipo mwenzie kuonesha utayari wa kumwangukia. Ni kosa!

Kusamehe pasipo kuketi mezani na kupata suluhu ni makosa kwa maana mbili. Mosi; anayekosewa anakuwa anafuga donge moyoni ambalo linamtesa taratibu. Ni sawa na kuficha jipu kwa kuamini ni uvimbe tu wakati ndani yake kuna usaha umeoza. Siku likitumbuka, harufu itakuwa kali mno.

Zingatia msemo kuwa mficha maradhi kifo humuumbua. Usiseme hakuna tatizo na wakati unatambua lipo na linakuumiza ndani kwa ndani. Hisia zako za mapenzi zisikuongoze kuwa mwepesi kusema yameisha. Tambua kuwa kila kosa lina mahitaji yake ya msamaha. Usiwe mbishi kusamehe ila usisamehe kama mahitaji ya masamaha hayajafikiwa.

Pili; Unaposamehe bila kuketi mezani unamtengeneza mtu mwenye kiburi pasipo wewe kujijua. Vilevile unaunda dharau dhidi yako. Aliyekukosea atakuona wa bei rahisi kama hutaonesha msimamo wa viwango vyako vya kuombwa msamaha. Kesho na keshokutwa atarudia kosa kwa imani kuwa huna madhara kwake.

Niweke wazi kuwa ninaposema msamaha na viwango vyake, namaanisha makosa yenye uzani. Haina maana ya migongano midogomidogo ya hapa na pale kila siku, hapana hata kidogo! Sizungumzii mambo ya chumvi kuzidi kwenye mboga na mengine ya bahati mbaya, najadili yale hasa yanayoumiza na ambayo kwa hakika huhitaji msamaha.

Msamaha ni lazima kusudio lake la juu liwe kupata salama ya pamoja, kutibu hasira zilizopo pamoja na maumivu yaliyosababishwa. Mkosewa na mkoseaji, wote kwa pamoja waridhike kuwa nyoyo zimetakasika, hivyo kuwa tayari kusogea mbele.

Hauitwi msamaha kama kutakuwa na vinyongo. Mkosewaji awe anajiona bado hakuombwa radhi kwa namna ilivyotakiwa. Mkoseaji naye upande wake ajisemee kuwa alishurutishwa tu kuomba msamaha lakini haoni mahali ambapo alikosea. Hali ikiwa hivyo andika kuwa ni makubaliano ya danganya toto na siyo suluhu.

MSAMAHA NI NINI?
Msamaha kwa maana yake halisi ni ile hali ya kihisia, pale mtendwa anapokuwa hajisikii maumivu tena. Aliyekosewa anakuwa anajisikia amani kwa kiwango cha kumwamini tena aliyemkosea. Shaka inaondoka na upendo unarejea kuchukua nafasi yake.

Maana ya msamaha ni pamoja na upande uliokosea kutambua kosa lake na maumivu yaliyosababishwa kwa mkosewaji, hivyo kuomba radhi. Msamaha wa kweli huendana na mabadiliko ya kitabia kwa yule aliyekosea. Unaomba msamaha kisha unarudia vitendo vilevile. Wapi na wapi?

Msamaha unakuwa na afya pale ambapo hatma inajengwa na maelewano ya pamoja kati ya mkoseaji na mkosewa. Hatimaye lugha inakuwa moja, wasiwasi unaondoka. Kinyume na hapo hakuna msamaha, ni makubaliano tu yenye mtindo wa kufunika kombe mwanaharamu apite.

Mathalan, wapenzi wanaachana halafu wanasema wamesameahana ili kila mmoja aishi maisha yake, hapo ukweli hakuna msamaha. Kama tatizo linajadiliwa, upande wenye makosa unakiri na kuomba kusamehewa kwa kiwango kinachotakiwa, hapo hakuna budi kwa mkosewa kutoa msamaha. Katika msamaha wa kweli hakuna kuachana.

Kuachana maana yake ni kushindana. Kama msamaha uliombwa basi haukukidhi viwango vya kumshawishi aliyekosewa. Vema msamaha upewe nafasi kwa sababu kuachana hakutakuwa na maana ya kurejesha amani, bali kukuza vinyongo na chuki.

Aliyeachwa pamoja na makosa yake, naye huchukia kwa kuona ameonewa, aliyeacha pia hatapata unafuu wa hisia zake. Msamaha ni muhimu.

Tambua ya kuwa inawezekana kabisa kosa likawa dogo lakini aliyekosewa akaamua kulikuza. Hiyo ni tabia ya kupenda kunyenyekewa, kusujudiwa na kupigiwa magoti ambayo baadhi ya watu wanayo.

Anataka kumuona aliyekosea akijishusha kwake mpaka mwisho ndiyo amsamehe. Vema pia kutambua tabia ya uliyemkosea. Na kwa ambaye yupo hivyo atambue kuwa anakosea, itamgharimu.

Mwingine kosa dogo adhabu ya kifo. Unamkosea kitu ambacho unaamini kinahitaji mazungumzo mafupi na kupata msamaha, yeye anakikuza mpaka mnaachana. Ni vizuri kujiandaa kisaikolojia. Pima kiwango cha kosa na uombe msamaha kwa kadiri. Ukizidisha ni kosa!

Lazima uelewe kuwa mwingine alikuwa anakutega ili ufanye kosa aweze kuachana na wewe kwa sababu alikuwa ameshayaona maisha mengine mbali na wewe. Mtu huyo hata uombe msamaha vipi atakusumbua tu, zaidi atakusababisha maumivu ya hisia. Gundua mapema usidhalilike.

TIA AKILINI
Yupo ambaye kuombwa msamaha ni sifa na kwa sababu tayari anakuwa ameshafanya uamuzi, kila unapomtumia SMS hatafuta, atatunza ili afanye maonesho kwa wengine.

Pengine SMS hizo akawa anamuonesha au kumtumia mwenzi wake mpya kwa imani kuwa ndivyo anajiongezea thamani ya kupendwa. Fikiria kile ambacho umekiandika kwa unyenyekevu kabisa, mwenzio anakisambaza.

Mwingine ukipiga simu anaweka ‘loudspeaker' akiwa mbele ya mpenzi wake mpya. Matokeo yake kila unachokizungumza kinasikika. Maneno ambayo ungependa yawe faragha kwako na kwa yule unayemuomba msamaha, yanasikika kwa wasiohusika.

Usisahau mchezo wa kurekodi sauti, wewe unasema yako ya moyoni, mwenzako anakurekodi neno kwa neno na baada ya hapo anasambaza sauti kwa wasiohusika. Ni ushamba kwa anayefanya hivyo lakini kwa aliyerekodiwa huumia kwa udhalilishaji aliofanyiwa.

Chukua mfano wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond', alipomrekodi aliyekuwa mpenzi wake, Wema Sepetu (Miss Tanzania 2006), ambaye alimpigia simu kuomba mapenzi yao yaendelee. Diamond akasambaza ile rekodi. Udhalilishaji.

ALAMA ZA MSAMAHA KUFANIKIWA
Kuna alama tatu ambazo mkosewaji akizitimiza, hurahisisha mno msamaha kufanikiwa. Humfanya aliyekosewa kuwa mwenye furaha tena, vilevile imani na mzani wa upendo hurejea kwenye kiwango chake katika uhusiano.

Alama hizo ni;

MOSI: Aliyekosea kukiri kosa, kutambua na kukubali kuwajibika kwa maumivu aliyomsababishia mwenzake.

PILI: Aliyekosea kuachana na kile alichokosea. Yaani kujiweka mbali na sababu ya tatizo na kuahidi kwa maneno na vitendo kutorudia tena. Kuwa mpya!

TATU: Aliyekosea kufanya juu chini kuona maumivu yote aliyopata aliyekosewa yanaondoka na moyo wake unakuwa mweupe.

ALAMA ZA MSAMAHA KUTOFANIKIWA
Aliyekosea anaweza kuomba msamaha lakini hajabadilika kitabia, hapo ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwa matarajio ya kulainika zaidi. Ni wajibu wa mkoseaji kutambua umuhimu wa kubadilika badala ya kukimbilia kusema "naomba msamaha".

Na kama mkoseaji anakuwa anajitahidi kutafuta suluhu lakini mkosewaji haridhiki na bado ana maumivu, hapo kunakuwa na alama mbili ambazo ni;

MOSI: Mkoseaji anakuwa hajatimiza mahitaji ya msamaha au ameyatimiza yote kimakosa.
Mkoseaji anakiri kosa lakini jinsi anavyoomba msamaha ni kama siyo tukio analolijutia. Ni makosa kuomba msamaha kwa jambo kubwa kama vile ni kitu cha bahati mbaya. Au kosa ni uaminifu, lakini bado unaendelea na vialama vya usaliti.

PILI: Kuna mahitaji ya msamaha yasiyowezekanika. Pengine mkoseaji hajui madhara aliyomsababishia mwenzake. Hapo utambue kuwa hataweza kuomba msamaha wa kiwango kinachotakiwa.

Sababu inaweza kuwa mkoseaji hawezi kubadili tabia au hajui namna bora ya kumaliza tatizo na mwenzake. Kama hoja ni kutojua, basi mkoseaji lazima ajifunze, vilevile mkosewa naye atambue kiwango cha mwenzake.

UNAUJUA MSAMAHA WA KINAFIKI?
Umekosewa na unahisi maumivu, hasira, huzuni, woga, kuchanganyikiwa na hisia nyingine ambazo hazipendezi. Hapa ni wazi kuwa mwenye kukosewa ndiye hasa anayepaswa kufanya uamuzi wa mwisho. Anapofanya uamuzi kinyume na matakwa ya hisia zake huo unakuwa msamaha wa uongo.

Unaitwa msamaha wa kinafiki (pseudo-forgiveness) kwa sababu mdomo unatamka kile ambacho moyo unapingana nacho. Unajua kabisa mwenzi wako anakudanganya na hamaanishi kuomba kutaka msamaha, wewe unakubali tu kisha unaendelea kuumia ndani kwa ndani.

Msamaha wa kinafiki unaweza kusababishwa pia na tabia ya mkosewaji kujifanya bingwa wa kupuuzia mambo. Badala ya kumuweka mezani mwenzake na kumweleza makosa yake, yeye anaacha yapite. Ndani kwa ndani yanamuumiza.
Yafuatayo ni mambo sita ambayo husababisha msamaha wa kinafiki;

MOSI: Mkosewaji anajifanya hajui, anapunguza au anayakataa maumivu aliyosababishiwa. Anaacha yanapita tu!

PILI: Mkosewaji kujilaumu kwa kosa la mwenzake. Yaani anajihukumu mwenyewe wakati alipaswa kumuweka mezani mkoseaji ili suluhu ipatikane.

TATU: Mkosewaji kuchanganyikiwa na kushindwa kujua asimamie wapi. Mathalan, anakiri mume wake ni tatizo lakini hajui afanye nini ili suluhu ipatikane. Mume naye kwa sababu haambiwi, hajui tatizo lake. Mke anasema anamsamehe mume bila ya anayesamehewa kujua kama kosa lake limejulikana na amesamehewa.

NNE: Mkosewaji kumuonea huruma mkoseaji kupita kiasi. Huu ni ugonjwa mkubwa kisaikolojia, unaitwa Stockholm syndrome. Mtu anamuonea huruma mtenda dhambi kwa sababu anampenda sana na anaamini wanapendana. Hata kumuuliza anashindwa kwa kuhofia kumuudhi.

TANO: Mkosewaji kujaa hofu kwa kuwafikiria watu wa nje kuliko wenyewe kama wahusika wakuu.
Mfano; mwenzi wako amekukosea lakini badala ya kushughulikia tatizo kwa maslahi yenu, unaanza kufikiria kile ambacho wengine watakisema baada ya kusameheana au kuachana.

Unawaza watu watawacheka? Hawatakubaliana na uamuzi wako wa kusamehe? Watakushusha hadhi? Kufikiria hisia za watu juu yako kwenye msamaha ni unafiki.

SITA: Mkosewaji kwa namna yoyote ile, kuamua kutumia njia ya mkato kufikia mwisho wa jambo badala ya kupita hatua zote zile ambazo zinaweza kutuliza hisia za maumivu aliyonayo.

ATHARI ZA MSAMAHA WA KINAFIKI
Tabia ya watu kufukia mashimo badala ya kutafuta suluhu ya migogoro yao, matokeo yake ni kuzaliana kwa nongwa zisizokwisha. Mtu kosa la mwaka juzi, ugomvi wa leo, yanaibuliwa yote ambayo ilidhaniwa yalikwisha.

Msamaha wa kinafiki huwa hauna suluhu ya kudumu. Kinachofanyika ni maegesho ya muda tu na siku mambo yakitibuka, hakuna kinachoweza kubakizwa. "Si unakumbuka uliwahi kufanya hivi?" "Unakumbuka kipindi kile niliamua tu kunyamaza."

Bundala ni msomaji wangu wa siku nyingi, siku moja aliwahi kunilalamikia kuhusu mke wake, kwamba huwa wanagombana na kusameheana lakini kila wanapotofautiana, hujikuta wanakumbushiana tofauti zao zilizopita.

Alinieleza kuwa tabia hiyo haipo kwa mkewe tu, kwani hata yeye hujikuta anamkumbusha mwenzi wake mambo ambayo yameshapita. Kwamba hawajawahi kugombana yakaisha bila kukumbushana migogoro iliyopita.

Nilimwambia Bundala: "Nenda katafute suluhu ya ukweli na jiepushe na misamaha ya kinafiki." Nilimweleza kuwa tatizo lao ni kuwa mambo ya nyuma yanajirudia kwa sababu hawakufunga mjadala. Waliegesha tu milango, kwa hiyo upepo ukivuma unafunguka.

Ni mwaka wa pili sasa tangu nilipomshauri Bundala, kila anaponipigia simu neno lake ni: "Kaka muongozo wako umefanya kazi kubwa sana."

Aliniambia baada ya kupata ushauri wangu, alikwenda kuketi mezani na mwenzi wake, wakazungumza kinagaubaga, wakaombana msamaha wa kweli. Siku hizi hakuna anayemkumbusha mwenzake tofauti za nyuma, maana walishayamaliza.

Nawe kama mwenzio ana tabia ya kukumbusha mambo ya nyuma au wewe ndiyo hulka yako, jaribu kutafuta namna ya kuketi na mwenzio, mzungumze kinagaubaga, mkishaombana msamaha wa kweli, tatizo hilo halitajirudia.

KANUNI YA KUSAMEHEWA
Unyenyekevu wako ni kilainishi cha msamaha. Unapokosea na ukitaka mwenzi wako asichelewe kupitisha msamaha juu yako ni wewe kujitahidi kuwa mpole kiasi cha kumwonesha mwenzio hakika unajutia ulichokifanya.

Na hata baada ya kukusamehe, ukitaka furaha ya mwenzi wako irejee haraka na kusahau mapema kile ulichomtendea ni wewe kuwa mnyenyekevu. Juu ya hapo ni wewe kuwa karibu yake.

Onesha unamjali kwa zawadi za hapa na pale. Usimwache mbali kwa muda mrefu bila kusikia sauti yako au kusoma SMS nzuri iliyosanifiwa kiufundi na vidole vyako.

Elewa kuwa anaweza kukusamehe lakini akawa mzito, hiyo ni kwa sababu kisaikolojia anakuwa amepata majeraha. Anakuwa kama anayeanza upya kwenye uhusiano wako na wewe. Ni jukumu lako kumrejesha kwenye upendo wake wa kawaida. Ukimjali atarudi haraka.

HITIMISHO
Msamaha ni muhimu sana kwako kiafya na kwa uhusiano wako. Jaribu kufikiria donge zito ambalo unakuwa umelimeza. Ile ni nyongo (tindikali) ambayo inakutesa mwenyewe ndani kwa ndani.

Unaweza kushangaa unakuwa na mwili dhaifu japo unakula vizuri, ngozi yako inakosa mng'aro, yote ni matokeo ya maumivu ya kisaikolojia. Umekosea omba msamaha yaishe, umekosewa, samehe ili maisha yenye furaha yaendelee.

Siku zote penda kutambua kuwa maisha yajayo ni yenye furaha na amani tele. Hutaifikia hiyo furaha na amani yako ijayo kama utakuwa na vinyongo visivyoisha. Maisha ni mafupi yenye kuhitaji ujiachie ukiwa na moyo usiobeba mizigo.

Pima ulinzi wako wa kisaikolojia, pambana na hasira, kama ni aibu imepita ikubali na uigeuze faida ya maisha yajayo. Zingatia kuwa watu wanakosewa na hujaanza wewe kukosewa. Utashinda yote kama utapenda kumtanguliza Mungu.

By Luqman Maloto

Naendelea kukualika kwenye darasa la mashauriano. Tujadili maisha na kutatua changamoto zetu za kila siku.
Na. +255 713 355 717

 
Nimeperuzi nikapata machache ambayo yananisibu ktk mahusiano yangu....

Pls summarize ili tupate key points kiwepesi maana sie wengine kusoma riwaya tulishaachaga
 
Kuomba msamaha ni muhimu. Tuendelee kuomba samaha punde tunapokosea au kukosolewa
 
Imenisaidia sana aisee,mahusiano yangu yatakua na hali nzuri tena
 
Sio kila kitu ni cha kusamehe. Vingine bila Adhabu mlengwa hawezi kupata akili.
Na pia kusamehe ni kipaji si kila mtu amejaliwa.
 
Back
Top Bottom