Mpenzi umenisaliti, naomba uende zako

Mpenzi umenisaliti, naomba uende zako

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Joined
Mar 16, 2014
Posts
227
Reaction score
246
Sitaki leso wala taulo naomba nilie mpaka machozi yote yakaukie kwenye paji la uso wangu. Siyo siri leo mlimwengu mimi naumia kwa ajili ya mapenzi. Sijaona sifa kukaa nalo kimya moyoni mwangu halafu linitese zaidi. Wakati tunaanza mahusiano yetu sikukuambia ila leo acha niseme nimeumia na ninazidi kuumia kwa sababu haikuwa kiapo chetu kuachana leo.

Ni wewe mpenzi uliyeniahidi kwamba utanipenda kwa moyo wako wote na jina langu ulikuwa ukilisifia kwamba ni zuri sana hata ulitajapo hupata ashki leo inakuweje mpenzi unakengeuka?

Mapenzi yetu hayajaanza leo uliniimbia kila nyimbo hadi nikaona fahari ya kujiona mimi ni mwanaume bora zaidi kati ya wanaume waliobora. Hukuishia hapo ukanipatia hata watoto na wao ukasema ni wema kama alivyo baba yao. Je wema wangu umepotea na ukasababisha na wa watoto upotee. Ukanikimbia ukaenda mbali ambapo sitaweza kukuona na huku ukinipaka masizi.Nini kimekusibu laazizi?

Sikutegemea kama binadamu ni msahaulifu kiasi hiki. Ni wewe uliyenipamba kwa majina yote mazuri na kila uliposafiri uliniahidi utaendelea kuyatukuza mahusiano yetu na kuwaeleza mataifa yote kwamba mimi ndio mpenzi wako na huwezi kuwa na mwingine. Nashangaa leo hizo ahadi zako zimeishia wapi? Ninaumia kwa sababu ni wajibu wangu kuumia kwa kumpoteza mpenzi kama wewe na nimeshangaa ghafla tu unanibadilikia, njoo mpenzi wangu turudiane huko unakoenda nafasi zimejaa. Ninachojua hasira za mkizi furaha kwa mvuvi. Njoo uniambie kosa langu ni lipi ili tuweze kurudisha rutuba na kustawisha mahusiano yetu kama zamani.

Kweli mapenzi matamu na hakuna kitu cha kuyafananisha na mapenzi kama unabisha niko tayari kwenda mahakamani haki ilipo. Sauti yangu imekauka na machozi yamekata huku nimefumba macho, kwa mbali masikioni mwangu nasikia nyimbo ulizokuwa ukiniimbia angali tuko wote. Zinanipa wazimu na kupandisha maruhani kwanini unikimbie wale uliosema utawapa sifa zangu leo hii ndio haohao umewakabidhi mtima wako na kisha mnaungana mnaanza kunisakama. Kama upo huko basi baki huko niache na watoto wangu tuishi kwa amani.

Basi acha mapenzi yaishe basi tanguliza hata uzalendo wa kuwa na mimi na kuwa tayari kwa lolote kuhakikisha tunadumisha penzi letu. Hima hima kabla hujavuka mto usitukane mamba, naona unajisahau sana mimi ndio nitabaki kuwa mpenzi wako bora kuliko wote hao unaowapapatikia. Ninakufahamu vizuri na ndio maana natumia lugha hii ya kwetu ili unielewe vizuri. Hao mabeberu wanakudanganya wanakuona wewe ni malaya usiyekuwa na msimamo leo umepata mpenzi Ufaransa kesho mara Ubelgiji kesho kutwa uko Sweden. Hawakupendi watakuzalisha na mwisho wa siku utabaki kurandaranda na kikubwa wanachotaka uwape siri zetu ili waje watupore mali zetu.

Hivi kweli una akili sasa hao watoto wako uliowaacha hizo mali zikipukutishwa wewe utapata faida gani. Siyo kwamba nakulaani ila najuta kuwa na mpenzi zuzu kama wewe ambaye huna shukrani hata utendewe lipi?

Mlimwengu mimi nitabaki kuwa hapa na yupo atakayenipenda zaidi kuliko wewe na ninajua hadi sasa ananipenda ndio maana yuko tayari kunilinda kwa gharama yeyote. Wewe mpenzi wangu unayesoma sasahivi waraka huu naomba huyo mumpuuze. Hata Mtume Muhammad na Yesu walipokuwa wanapigania mapenzi yao mtu wa hivi alikuwepo. Hivyo laazizi na nyongo mkalia ini wangu nakusihi usifanye kama huyu ambaye kanisaliti.

Niamini mimi utafurahia penzi letu maana mimi ni kati ya watu tuliobarikiwa kwa kuwa na kila aina ya uzuri uliosanifiwa na kusanifika na Mungu wetu. Huyo alipokimbilia wao wenyewe kwa adi na uvumba wanatamani waje waone uzuri wa jina langu linavyosadifu yaliyomo.

Nakuomba tuliza nafsi hapa ni kisima cha amani, hata upepo uvumapo hupeleka ujumbe juu ya mazuri yangu hukohuko walipo. Ninakusihi endelea kunilinda na kunipenda kwa moyo wako wote. Achana na huyo aliyenisaliti na kunitia maumivu wewe ndio unabaki kuwa mfariji wa moyo wangu pamoja na wanangu.

Mungu Ibariki Tanzania.

Mungu wabariki Viongozi wake

8/02/2021

Imesanifiwa na
Mohamed Ismail Rwabukoba
mohammedismail613@gmail.com
#mlimwengumimi
 
Mapenzi hayajawahi kumuacha mtu salama hata mara moja. Naamini kila binadamu aliyekamilika lazima aonje chungu ya mapenzi japo kwa mtindo ulotofautiana. Pole ndugu yangu endelea kumbembeleza umpendaye arudi muijenge familia mliyoianzisha.
 
Back
Top Bottom