Mpende na umjali sana mpenzi wako.

Feb 18, 2017
63
62
MPENDE NA UMJALI SAAANA MWENZI WAKO! NAKUHAKIKISHIA HAINA KUFELI

IPO hekima kwamba usioneshe unampenda sana mwenzi wako; awe mume au mke, rafiki au mchumba. Hekima hiyo inatoa angalizo kuwa anayependwa akijua, basi hujaa maringo, kiburi na dharau kwa anayempenda. Ooh, ni ile shukurani ya punda mateke!

Hata walioniita mjukuu waliamini hivyo. Waliniambia: "Tatizo la Anko wako Shivute anamwonesha mkewe anampenda sana." Walishauri kupenda bila kujionesha. Mapenzi ya gizani. Anayependa anaficha. Anayependwa hajui. Huo ndio upendo gani? Mateso!

Raha ya upendo ni kuuacha moyo uwe huru. Kuficha ni kuunyima moyo uhuru. Utajiumiza bure. Unapopenda onesha upendo. Anayependwa ajue kuwa anapendwa. Mjali sana na iwe dhahiri kwa unayemjali. Hiyo ni silaha ya hali ya juu kwenye uhusiano.

Hapa natofautiana na walioniita mjukuu. Nasema hivi; kupenda halafu kuficha upendo ni ushamba. Unataka ukamwoneshe nani upendo wako zaidi ya unayempenda? Hata hivyo, sikwambii upende tu, bali nakushauri upende ukiwa na akili timamu.

Ukimpenda na kumjali sana mwenzi wako haina kufeli. Nakuhakikishia utavuna moja kati ya faida mbili.

MOSI: Utauteka Moyo Wake.

PILI: Utauteka Upumbavu Wake.

MOYO WAKE

Ukimpenda na kumwonesha upendo mkubwa mtu mwenye akili timamu, utauteka moyo wake. Mwenye akili hutambua kuwa kupendwa ni tunu, hivyo huona bahati kupendwa. Naye huupokea upendo kwa moyo mkunjufu na kurejesha upendo.

Hapa namaanisha kuwa kumpenda mwenye akili timamu kisha ukamwonesha upendo mkubwa na kumjali, atakulipa upendo mpaka ushangae. Maana utakuwa umeuteka moyo wake.

UPUMBAVU WAKE

Upumbavu ni kifuniko cha akili. Ukimpenda mpumbavu ujue akili yake imefunikwa. Ukimwonesha upendo na kumjali sana, yeye atakuletea maseke. Atadhani huna pa kwenda. Atakudharau na kukufanyia visa vingi sana.

Ukishabaini unayempenda sana na kumjali anakufanyia vitimbi, ujue tayari umeshauteka upumbavu wake. Mpumbavu akipendwa upumbavu wake hudhihirika. Ukishabaini unayempenda ni mpumbavu, hapo utakuwa unajua cha kufanya. Nimeshakushauri; penda ukiwa na akili timamu. Vinginevyo, bora ushike kanuni ya walioniita mjukuu.

Onesha upendo. Nakuhakikishia haina kufeli.

Ndimi Luqman Maloto
 
Back
Top Bottom