Mpendazoe-Uongozi unanunuliwa kama mbuzi mnadani

sulphadoxine

JF-Expert Member
Nov 1, 2010
2,257
644
MNAMO Juni 12, 2011, Mbunge wa zamani wa jimbo la Kishapu, Fred Mpendazoe, alizindua kitabu chake kinachoitwa “Tutashinda” mjini Dodoma. Ifuatayo ni sura ya pili kwenye kitabu hicho ambapo Mpendazoe anazungumzia vita dhidi ya ufisadi Tanzania na jinsi ambavyo "Uongozi unanunuliwa kama mbuzi mnadani:"

Tatizo kubwa na la muda mrefu katika nchi yetu, ambalo limekuja kujulikana miaka ya hivi karibuni, ni rushwa na ufisadi usio na kifani. Kumekuwepo mijadala mbalimbali ndani na nje ya Bunge kuhusu tatizo hili na athari zake kwa hatma ya taifa letu.

Katika kitabu cha "Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania," Mwalimu J.K Nyerere akigusia suala hili, amesema hivi: "Utajiri unaweza kupatikana kutokana na rushwa kwa watumishi wa umma au kutokana na wafanyabiashara ambao wanawania nafasi za kisiasa ili wawe wadeni wa Rais aliyeko madarakani."

Maana ya maneno haya ni kwamba kiongozi akipatikana kwa kupewa fedha na matajiri, atapaswa alipe fadhila kwa matajiri hao waliokifadhili chama chake au yeye mwenyewe wakati wa uchaguzi. Mwalimu Nyerere aliliona hili litatokea na kwa sasa ndilo tatizo kubwa linaloisumbua nchi yetu.

Mwaka 2000 mwezi Aprili, akizungumzia ufisadi, aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Jaji Joseph Sinde Warioba, alieleza kwamba: "Kuna mwenendo usiopendeza wa kuongezeka kwa kasi kwa pengo kati ya matajiri na maskini. Siasa inatekwa na matajiri. Ufisadi na rushwa ni vitu muhimu kwenye uchaguzi.

“Ufisadi unaigawa vipande nchi. Tunashuhudia katika kipindi hiki wingi wa wafanyabiashara wakijiunga kwa wingi na CCM kama wafadhili wa chama. Ni imani yangu kwamba hakuna mfanyabiashara hapa nchini anayeipenda CCM kwa dhati kiasi cha kutoa mwenyewe pesa zake mfukoni kwa chama hicho.

Wala hakuna wafanyabiashara wanaoingia kwenye siasa au wanaopenda kuwahudumia wananchi kwa dhati, bali wengi wao wanajiingiza kwenye siasa ili kulinda biashara zao tu."



Kauli hizo, ya Mwalimu Nyerere na ya Jaji Warioba, zinaonesha kiini cha ufisadi katika nchi yetu. Ufisadi mkubwa uliopo sasa katika siasa na serikalini ni zao la ufadhili. Wafadhili wamechukua nafasi kubwa katika shughuli za siasa na hakuna mfadhili anayeto fedha zake bila kuwa na malengo.

Kutokana na wafanyabiashara kujiingiza kwenye siasa, kukazuka sera isiyo rasmi ndani ya CCM kuwa nafasi za waweka hazina au makatibu wa fedha na uchumi katika ngazi mbalimbali zikachukuliwa na wafanyabiashara bila kujali uadilifu wao.

Matokeo yake ni kuwa watendaji wa chama wamekuwa mateka wa wafanyabiashara na wafanyabiashara wamekuwa na maamuzi kwenye vikao vya chama. Kwa hiyo, ufisadi umeshika kasi.

Aidha, ufisadi uliopo unaonekana kuchochewa na nguvu za matabaka yanayoibuka na kukua kwa kasi katika jamii yetu. Wapo wananchi matajiri sana na maskini sana. Pengo lililopo kimaisha ni kubwa na ndilo linalokwamisha maendeleo ya wengi katika taifa.

Nieleweke vizuri hapa, si kila tajiri ni fisadi kwani wapo waliotajirika kwa njia za haki ingawa pia ni rahisi kwa ngamia kupenya kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kuurithi ufalme wa Mungu.

Wataalamu wa sayansi ya jamii wanasema kwa sababu ya unyonyaji au uporaji wa uchumi unaofanywa kwa njia mbalimbali za kifisadi, kumekuwa kukiiibuka na kujengeka kwa matabaka katika jamii. Tabaka la kwanza ni la matajiri, ambalo humiliki sehemu kubwa ya uchumi wa nchi kwa njia za ufisadi au unyonyaji -- kwa lugha ya Kigiriki, tabaka hili linaitwa "oligarchy" (oligaki) (utawala wa serikali ya wachache) .

Oligaki wataweka Rais wao madarakani ili waweze kuendelea kupora utajiri wa nchi. Wataweka majaji wao na wanasheria wao kwenye mhimili wa mahakama ili wakiwa na kesi waweze kushinda. Wataweka watu wao kwenye vyombo vya usalama ili vyombo hivyo badala ya kulinda raia vilinde maslahi yao.

Matajiri hawa wataweka madiwani wao na wabunge wao ili maamuzi yanayopitishwa kwenye vyombo vikuu vya maamuzi ya nchi yalinde maslahi yao. Uwepo wa tabaka hili husababisha kuwe na matumizi makubwa ya fedha kwenye chaguzi na sheria kandamizi za uchaguzi.

Tabaka la pili ni lile la wateule wachache marafiki na ndugu wa Oligaki - kwa Kigiriki huitwa "aristocracy" (aristokrasi). Hawa ni watu waliowekwa na matajiri kwenye sehemu nyeti na muhimu kwa ajili ya kulinda maslahi yao. Watu hawa wako kwenye taasisi za fedha, balozi, serikalini na kwenye vyama vya siasa. Tabaka hili kazi yake kuu ni kutetea na kulinda maslahi ya matajiri ambao wameshika njia kuu za uchumi za nchi na hivyo huwa na sauti serikalini kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya matajiri.

Tabaka la tatu ni la watu wenye tamaa ya madaraka "timocracy" (timokrasi). Watu wa tabaka hili huunga mkono hoja za oligaki na aristokrasi, na hutamani siku moja waingie kwenye matabaka hayo.

Timokrasi ni tabaka la watu wasio na msimamo wowote, kwani wametawaliwa na tamaa na makuu, hivyo ni rahisi kuwasaliti wananchi. Timokrasi ni wanafiki. Mnafiki humtukuza yeyote kwa lolote, kwa matumaini ya chochote; ndivyo walivyo.

Tabaka la nne ni la wananchi maskini wanaoishi kwa matumaini ya kupata maisha bora ambayo huwa vigumu sana kupatikana katika jamii yenye matabaka hayo mengine.

Matabaka haya yanajengeka kwa kasi kubwa. Kuwepo na kuimarika kwa matabaka haya kunaweza kusababisha kuwa na serikali isiyotokana na wananchi na isiyowajibika kwa wananchi, hivyo kusababisha demokrasia kukoma na udikteta kushamiri katika maamuzi yanayohusu maslahi ya nchi.

Katiba yetu ya sasa inasema wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yote kutoka kwa wananchi na itawajibika kwao kupitia Bunge. Serikali ambayo msingi wa mamlaka yake ni wananchi na serikali inayopata madaraka kutoka kwa wananchi ni ya kidemokrasia.

Kwa tafsiri rahisi, ni serikali inayochaguliwa na wananchi na inaongozwa na wananchi kwa ajili ya wananchi. Kwa mwenendo unaoendelea sasa, kama hatutachukua hatua madhubuti, serikali haitakuwa kwa ajili ya wananchi na haitachaguliwa na wananchi na hivyo haitawajibika kwa wananchi.

Ukweli ni kwamba kuna matajiri au watu wanaotumia pesa kumiliki siasa na uongozi katika nchi yetu, ni jambo lililo wazi. Mathalani, kulikuwa na matumizi makubwa ya fedha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha Urais katika uchaguzi huo, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, akizindua Bunge Desemba 30, 2005, alisema, "Yameanza mawazo kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha.

“Tusipokuwa waangalifu, nchi nyetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo, maana unaweza kufadhiliwa na mtu ili ununue uongozi, ni vema sasa tulishughulikie suala hili."

Pia, Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake, aliwahi kuonya juu ya hatari ya watu wachache wenye pesa kujaribu kutafuta uongozi kwa manufaa yao. Alisema: "Tanzania halijawa taifa imara sana na adilifu kiasi cha kuruhusu matajiri kuingia kwenye uongozi wa nchi kama ilivyo Marekani na Ulaya. Wakati huo bado uko mbali sana na tukitaka kuuvuta kwa kamba huko ndiko kuliingiza taifa letu changa kwenye kiwango cha ufisadi," kama ilivyo sasa.

Nchi kuwekwa rehani kwa matajiri ni jambo la hatari sana, kwa maana serikali itaongozwa na matajiri na haitawajibika kwa wananchi. Demokrasia itakoma na udikteka utatawala. Jambo linalojitokeza hapa na ambalo ni matokeo ya matumizi makubwa ya fedha na rushwa kwenye uchaguzi, ni kupatikana kwa viongozi ambao hawakuchaguliwa na wananchi bali walinunua uongozi au waliotoa rushwa kushawishi wapiga kura wawape uongozi.

Serikali inayopatikana kwa rushwa haiwajibiki kwa wananchi. Hutumikishwa na matajiri walionunua uongozi na waliotoa rushwa. Serikali hiyo huwaabudu matajiri walioiweka madarakani, haiwezi kufanya maamuzi yenye maslahi kwa wananchi. Serikali hiyo hulinda maslahi ya watu wachache, haiwezi kuchukua hatua dhidi ya ufisadi.

Wakati nikichangia Muswada wa Sheria ya Fedha kwenye Uchaguzi mwanzoni mwa 2010, nilizungumzia tatizo la rushwa katika chaguzi na kutoa ushauri. Nilisema mabadiliko na maendeleo makubwa kwenye nchi yetu hayawezi kutokea bila ya mabadiliko makubwa ya kisera, kikatiba na kuhusu mifumo ya utendaji.

Tatizo la rushwa lililopo nchini limejikita ndani ya jamii na kwa hiyo sheria peke yake huenda isilimalize kwa haraka na kwa ufanisi kama tunavyodhani au kutegemea. Rushwa hutolewa na hupokelewa kwa siri. Fedha nyingi zinazotolewa na wanaotaka kununua uongozi hupokelewa kwa hiari na shauku kubwa na wapiga kura hufanyika kwa siri au kwa visingizio vingi.

Umaskini mkubwa walionao Watanzania wengi unasababisha wapokee rushwa kwa shauku. Mara nyingine, wananchi wenyewe huitaka, au huidai, au huiomba. Watoaji rushwa hupata urahisi wa kuitoa na katika hali hii ni vigumu kupata ushahidi wowote. Hivyo, sheria inaweza isizae matunda ya kuridhisha na badala yake inaweza ikasababisha madhara makubwa zaidi kuliko tunavyotegemea.

Nilishauri na bado nashauri kwamba, uhamasishaji na uelimishaji wa wananchi juu ya madhara ya rushwa iwe njia yetu kuu ya kupunguza au kuondokana na tatizo hili, hasa kama uelimishaji huo utatoa mifano inayoonekana wazi kwa wananchi ili waichukie rushwa. Naamini kuwa bila wananchi kuichukia rushwa, itakuwa kazi ngumu kuindoa kwenye uchaguzi.

Wananchi wote tukiichukia rushwa kwa dhati itaondoka haraka. Hapa niwaase Watanzania jambo moja ambalo naamini pasipo shaka yoyote kwamba tukilielewa na kulifuatilia litatusaidia katika kupunguza rushwa kwenye uchaguzi.

Zipo sifa kuu mbili au vigezo vya kumpata kiongozi, awe Rais, Mbunge, Diwani au nafasi yoyote ya kuchaguliwa. Sifa ya kwanza ni lazima tunayetaka kumpa uongozi awe na uwezo wa kuongoza na mchapa kazi kwelikweli.

Na sifa kuu ya pili, mtu huyo sharti awe hataki kabisa kuwa Rais, mbunge au udiwani -- huyo ndiye watu wamfuate, wamshauri, wamwombe ndipo atakuwa kiongozi bora, kwani atawaheshimu waliomwomba awaongoze.

Mwalimu Nyerere, katika kitabu chake, "Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania," anasema wanasiasa kwa kawaida hupenda kutawala hata kama hawana uwezo wa kutawala. Kwa hiyo, wako tayari hata kuhonga ili wachaguliwe kuwa watawala au wako tayari kuchakachua kura ili watangazwe washindi na wakishachaguliwa au kutangazwa washindi hawatoki bila kulazimishwa.

Wanaotaka sana uongozi kwa gharama yoyote mara nyingi ni wanasiasa ambao hawana uwezo wa kuongoza. Hata hivyo, wapo wanasiasa wanaoutamani uongozi kisha wakawa viongozi bora, kama aliyekuwa Rais wa Marekani John F. Kennedy, lakini nitahadharishe kuwa watu wa aina hiyo ni adimu sana duniani.
 
Back
Top Bottom