Moyo ukikosa baba, huachi kutangatanga!
Siyo pishi ni kibaba, moyo hugeuka janga,
Hakuna nyingine tiba, ya moyo unaotanga,
Moyo ukikosa baba, ni moyo uso na huba!
Moyo ukikosa baba, huwa na kidonda ndugu!
Ngumu kutoa mahaba, hujenga kama usugu,
Huumiza kama mwiba, hutegua kama tegu,
Moyo ukikosa baba, ni moyo uso na huba!
Moyo ukikosa baba, huwa ni moyo na chozi!
Usiokoma msiba, unagubisha majonzi,
Usipomjua baba, moyo huwa na simanzi,
Moyo ukikosa baba, ni moyo uso na huba!
Moyo ukikosa baba, siyo moyo wa kubeza,
Hili siyo jambo haba, jambo hili linaliza,
Mtu kumkosa baba, mbinguni ataapiza,
Moyo ukikossa baba, ni moyo uso na huba!
Moyo ukikosa baba, beti tano zinatama,
Simameni kina baba, mkaiponye mitima,
Wape haki wenye huba, nawasihi kina mama,
Moyo ukikosa baba, ni moyo uso na huba!
Na. M. M. Mwanakijijji (Tarumbeta ya Kijiji)
Nje ya Jiji la Detroit - Michigan