Malima amjibu Spika Sitta
Usiri wa Mikataba
na Esther Mbussi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, amesema mikataba ya uchumi na kibiashara inayosainiwa nchini, haiwezi kuwekwa wazi kutokana na ushindani wa kibiashara.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wandishi wa habari kuhusu usiri uliopo katika utiaji saini wa mikataba ya madini ambayo katika siku za hivi karibuni imekuwa ikipigiwa kelele za kutoifaidisha nchi.
Malima ametoa kauli hiyo siku moja tu baada ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kuhoji kuwepo kwa usiri katika kusaini mikataba ambayo haitoi fursa ya kutekelezwa kwa masilahi ya umma na badala yake wawekezaji wa kigeni ndiyo wanaofaidika.
Alisema kamwe mikataba hiyo haiwezi kuwa wazi wakati wa mchakato na utiaji saini lakini itawekwa wazi katika utekelezaji tu baada ya makubaliano hayo kuafikiwa.
Kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya viongozi wakihoji usiri wa nini na kwa faida ya nani? Ukweli ni kwamba huwezi kuweka wazi mkataba na mwekezaji katika hatua za awali kwani huwezi kujua nani atakuja na wazo kama la yule wa awali, kwa hiyo ni ushindani wa kibiashara na si vinginevyo, kitakachowekwa wazi ni utekelezaji, kwa wabunge na wananchi kwa ujumla, alisema Malima.
Alisema katika biashara kuna watu husikiliza nani anataka kufanya nini, kwa hiyo kuwekwa wazi kwa mikataba hiyo kunaweza kuathiri nchi kukosa wawekezaji kutokana na mwekezaji mwingine kuchukua siri au wazo la mwenzake na kumzunguka.
Kinachofanyika kabla ya kusaini mkataba wewe kama mwekezaji ni kupata maelezo yako, kwamba utafanya hili na lile, utalipaje kodi, na vitu kama hivyo, kwa hiyo kujianika kwako hadharani (mwekezaji), ni kumuwezesha mwenzako kutaka kufanya ulichokusudia, hakuna mazingira ya rushwa wala kuuza nchi katika suala la kusaini mikataba, alisema Malima.
Moja ya mikataba ya siri iliyowahi kufanywa ni ule wa mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick ya Uingereza, uliosainiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, aliyejiuzulu Februari mwaka huu, Nazir Karamagi.
Juzi, Sitta alisema kuna makubaliano baina ya serikali na ofisi ya Bunge yaliyofikiwa kuwa mikataba yote ya maendeleo waziri husika anapaswa kumpatia Katibu wa Bunge ambaye ametengewa masijala mahususi ya wabunge kuona mikataba hiyo.
Kuna mantiki gani kwa waziri kwenda ughaibuni na kutuambia kuwa anakwenda kusaini mkataba wenye masilahi yetu wananchi na baadaye akirejea atuambie walichokubaliana ni siri, hata kwa wawakilishi wetu, yaani wabunge? Tutapimaje kama masilahi ya nchi yamezingatiwa au mhusika amekwenda kuiuza nchi? alisema Spika.
Alisema wanaoendeleza dhana ya usiri dhidi ya mwenye mali ambaye ni mwananchi, wanalo jambo na wasakamwe ili waache mizengwe, usiri wa namna hiyo ndiyo unasababisha wanahabari kuandika habari za kuhisi au kile wanachokiamini kuwa ni sahihi.
Sitta aliishauri serikali kuweka utaratibu ulio wazi kwa kila wizara kuwa na dawati la taarifa, ambapo wanahabari na wananchi wataweza kupata habari za uhakika kuhusu utekelezaji wa majukumu yaliyo chini ya wizara hizo.